August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbowe: Haturudi nyuma

Spread the love

KAZI imeanza. Hivi ndivyo unavyoweza kusema baada ya Serikali ya Rais John Magufuli jana kusababisha vurugu kubwa Kahama mkoani Shinyanga, anaandika Faki Sosi.  

NI kwa mara ya kwanza ndani ya utawala wa Rais Magufuli, taifa linashuhudia vurugu za kisiasa zinazotokea kwa mgongo wa Jeshi la Polisi nchini.

Vurugu kubwa imetokea jana baina ya Jeshi la Polisi na wananchi kwenye mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kusababisha sintofahamu.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema amesema kuwa, pamoja na vitisho vya demokarsia nchini, chama hicho hakitarudi nyuma kudai haki.

Mbowe amesema kuwa, wataendelea kudai haki ya demokrasia nchini ndani ya mahakamani, bungeni, ndani na nje ya nchi.

“Huu ni mwendelezo wa serikali na mabavu. Hawataki vyama vingine vya siasa kufanya mikutano,” amesema Mbowe na kuongeza kwamba, watakwenda mahakamani na kuongeza.

Taarifa kuhusu vurugu hizo zinaeleza kuwa, Jeshi la Polisi lilitumia maji ya kuwasha pamoja na mabomu ya machozi kutawanya watu waliokuwepo kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa na Chadema mjini Kahama.

Mkutano huo ulikuwa ni uzinduzi wa ‘Dai Demokrasia’ ambapo Jeshi la Polisi liliingilia kati na kuuzuia ikiwa ni muda mchache baada ya Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam kuzuia kufanyika kwa mikutano ya hadhara ya kisiasa nchini.

“Jeshi la Polisi kupitia vyanzo vyake mbalimbali vya habari limebaini kuwa, mikutano hiyo ina lengo la kuwahamasisha wananchi kutotii sheria za nchi (Civil disorder),” ilieleza taarifa yaNsato Mssanzya, Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo, Makao Makuu jijini Dar es Slaam jana.

Vurugu hizo zilianza saa nane mchana baada ya polisi waliojiandaa kufika kwenye eneo la tukio na kisha kuuzuia kufanyika mkutano huo.

Hatua ya polisi kutoa maelezo ya kuzuia mkutano huo na kutaka watu watawanyike ilianza kuzua mzozo na hatimaye vurugu ambapo wananchi waliokuwa kwenye viwanja vya mkutano vya CDT walianza kupambana na polisi.

Hali hiyo iliwalazimu polisi kutumia mabomu ya machozi pamoja na maji ya kuwasha huku wananchi wakitumia mawe kukabiliana na mshindo wa polisi Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU).

Hayo yalifanyika ikiwa tayari Mbowe pamoja na viongozi wenzake wakiwa tayari wamewasili kwenye mkutano huo.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, Mbowe, Dk. Vincent Mshinji, Katibu Mkuu wa Chadema pamoja na wabunge waliosimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge walizingirwa na polisi huku wakimwagiwa maji ya kuwasha wakiwa kwenye magari yao.

Hali hiyo inaelezwa kuwazidisha hasira wananchia waliokuwa wamekwenda kuhudhuria ufunguzi huo na kusababisha kuwatupia mawe polisi.

Kabla ya tukio hili, yalianza majibizano kati ya polisi na viongozi wa Chadema kwa kutumia vipaza sauti.

Polisi walitumia kipaza sauti kilichokuwa kwenye gari lao kwa kusema “Tangazo, tunawataka wananchi mliopo kwenye uwanja huu muondoke kwa sababu mkutano huu si halali. Ondokeni eneo hili kwa ajili ya usalama wenu. Huu mkutano si halali.”

Julius Mwita, Katibu Mkuu wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) alishika kipaza sauti na kupuuza tangazo la polisi.

“Hapa polisi CCM wasituvuruge. Jamaa wametupa wenyewe barua ya uturuhusu tufanye mkutano wetu, leo wanakuja na washawasha zao kuzuia, ebooh!” alisema Mwita.

Wakati akipuuza tangazo hilo wananchi waliokuwepo kwenye uwanja huo walikuwa wakimshangilia.

error: Content is protected !!