May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbowe atuma ujumbe msiba wa mkwe wake akiwa gerezani

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

 

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ametuma ujumbe wa buriani katika msiba wa mama yake mkwe, Johara Mtei, baada ya kushindwa kushiriki mazishi yake kutokana na kuwa mahabusu.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Mbowe ametuma ujumbe huo akiwa katika mahabusu ya Ukonga jijini Dar es Salaam, anakoshikiliwa akikabiliwa na mashtaka ya kula njama za kufanya ugaidi, leo Jumapili, tarehe 22 Agosti 2021, na kusomwa na Dk. Rafael Kasonga.

Mbowe na wenzake watatu, wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama za kufanya ugaidi, kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini humo, ambapo yuko mahabusu tangu tarehe 21 Julai 2021, alipokamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, na kuhamishiwa Dar es Salaam.

Akisoma ujumbe huo katika ibada ya kuuaga mwili wa Johara, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Azania Front jijini humo, Dk. Kasonga amesema Mbowe anasikitika kukosa mazishi ya mkwewe, kutokana na kuwa mahabusu.

“Nasikitika kutoa taarifa hii nikiwa katika gereza la Ukonga, kwamba siwezi kumsindikiza mama kwenda kwenye safari yake ya mwisho. Kwamba siwezi kushiriki na familia katika kumshukuru Mungu kwa zawadi ya mama,”umesema ujumbe wa Mbowe uliosomwa na Dk. Kasonga.

Katika ujumbe huo uliosomwa na Dk. Kasonga, Mbowe amesema alimfahamu Mama Johara kwa miaka 30 na kwamba miongoni mwa tabia alizozionesha katika kipindi hicho, ni ukarimu na upendo pasina kugombana na watu.

“Alikuwa wa pekee sana, kwa miaka 30 nilimfahamu alikuwa mama mwema sana, alikuwa ni mkarimu aliyepitiliza, sijawahi kumuona akigombana na yeyote. Aliwapenda sana wanawe na nilithibitisha hayo,” umesema ujumbe wa Mbowe, uliosomwa na Dk. Kasonga.

Johara alifariki dunia tarehe 20 Agosti 2021, katika Hospitali ya Aga Khan, mkoani Dar es Salaam, alikokuwa anapatiwa matibabu.

Mwili wa Mama Johara unatarajiwa kuzikwa Jumanne, tarehe 24 Agosti 2021, nyumbani kwake Tengeru mkoani Arusha, majira ya saa 5.00 asubuhi.

Johara ni mama wa Dk. Lilian Mtei, ambaye ni mke wa Mbowe.

error: Content is protected !!