Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mbowe ashambuliwa Dodoma, avunjwa mguu
Habari za SiasaTangulizi

Mbowe ashambuliwa Dodoma, avunjwa mguu

Spread the love

MWENYEKITI wa taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, ameshambuliwa na watu wasiojulikana, usiku wa manane wa kuamkia leo Jumanne, tarehe 9 Juni 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Mbowe amekutwa na kadhia hiyo, akiwa anarejea katika makazi yake yaliyopo eneo la Area D, jijini Dodoma.

Taarifa zilizothibitishwa na majirani zinasema, Mbowe alifika nyumbani kwake majira ya saa nane usiku, akiwa na dereva wake, aliyefahamika kwa jina la Willifred Urassa.

“Huyu bwana (Freeman Mbowe) ameshambuliwa na watu watatu ambao walikuwa wamebeba silaha. Alikutana na watu hao kwenye ngazi, wakati anaelekea ndani kwake,” ameeleza mmoja wa mashuhuda ambaye hakupenda kutajwa jina lake.

Anasema, kati ya watu hao watatu, mmoja alimdhibiti dereva wake, na kwamba mara baada ya kumjeruhi Mbowe, dereva wake alimchukua bosi wake na kumfikisha hospitali.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Mbowe amevamiwa na watu watatu ambao wamemkanyaga kanyaga na kumvunja mguu wake wa kulia.

Nacho Chadema kimethibitika taarifa kuwa Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni (KUB) na mbunge wa Hai, mkoani Kilimanjaro, ameshambuliwa na watu wasiojulikana.

Kupitia mtandao wake rasmi wa Twitter, Chadema kimeandika: “Mwenyekiti wa Chadema taifa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB), Mhe.@freemanmbowetz ameshambuliwa na kujeruhiwa na watu wasiojulikana wakati akirejea nyumbani kwake jijijini Dodoma.”

“Amekimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu. Tutawapatia taarifa zaidi baadae…”
Kupatikana kwa taarifa hizi kumekuja siku moja, tangu aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki na mmoja wa wanasiasa mashuhuri nchini, Tundu Lissu, atangaze nia ya kugombea urais kupitia Chadema.

Aidha, kupatikana kwa taarifa za shambulio dhidi ya Mbowe, kumekuja miaka mitatu, tangu Lissu ashambuliwe kwa risasi, nyumbani kwake, Area D, mjini Dodoma.

Lissu alimiminiwa risasi zaidi ya 30 na 16 kumpata mwilini mchana wa tarehe 7 Septemba 2017 na kupelekwa hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu ya awali, na baadaye kusafirishwa kwa ndege hadi Nairobi, nchini Kenya.

Kwa sasa, Lissu yuko Ubelgiji alikopelekwa kwa matibabu yaliyotokana na shambulio hilo la risasi. Alipelekwa huko tarehe 6 Januari 2018.

Baadhi ya wabunge wa Chadema wakiwa hospitali wakifuatilia hali ya Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe

Licha ya Lissu mwenyewe kuthibitisha amepona na hatumii dawa, bado hajarejea Tanzania mpaka sasa, kufuatia kuhofia usalama wake.

Hata hivyo, jana Jumatatu, Lissu akiwa Ubelgiji alitangaza nia ya kuwania urais ndani ya Chadema akiomba ridhaa kimpitishe ili agombee urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Giles Muroto amethibitisha Mbowe kuvamiwa.
Amesema, jeshi lake, linafuatilia taarifa hizo, lakini halijaweza kutoa taarifa zaidi. MwanaHALISI linaendelea kufuatilia hatua kwa hatua, taarifa kuhusu kuvamiwa kwa Mbowe.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!