October 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbowe apewa saa 72 za uangalizi

Spread the love

FREEMAN Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), yuko chini ya uangalizi wa kawaida kwa siku tatu katika Hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Alhamisi 2020 na Tumaini Makene, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano Chadema, Mbowe yuko katika uangalizi huo, kuanzia asubuhi ya jana tarehe 10 Juni 2020.

Mbowe amewekwa kwenye uangalizi huo baada ya kufanyiwa upasuaji kwenye mguu wa kulia, uliovunjwa baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Jumanne tarehe 9 Juni 2020, nyumbani kwake Area D jijini Dodoma.

Mbowe alivamiwa na watu watatu wasiojulikana, ambao walimshambulia na kumsababishia majeraha katika mwili wake, pamoja na kumvunja mguu wa kulia.

Kupitia taarifa yake, Makene amesema Mbowe anaendelea kupata uangalizi wa ziada chini ya madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Aga Khan.

“Hata hivyo, madaktari wamesisitiza sana mgonjwa apate muda wa kutosha wa kupumzika angalau kwa saa 72 kuanzia asubuhi ya jana, hasa kutokana na maumivu makali aliyonayo sehemu mbalimbali ya mwili wake,” amesema Makene na kuongeza:

“Hali inayowahitaji wataalamu kuwa na muda wa kutosha na mgonjwa kuweza kumfanyia uchunguzi wa kina.”

Makene amesema, kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, amewekwa chini ya uangalizi baada ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya ziada, tangu alipofikishwa hospitalini hapo, siku ya Jumanne.

“Mbowe anaendelea kupata uangalizi wa ziada chini ya madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Aga Khan, baada ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya ziada tangu alipofikishwa hospitalini hapo juzi jioni.

Uangalizi huo ambao unahusisha saa 72 za kupumzika, umefuatia upasuaji wa mguu wake wa kulia na uchunguzi wa ziada wa maeneo mengine ya mwili, uliofanyika jana Jumatano ambao bado unaendelea,” amesema Makene.

Ofisa huyo wa Chadema amesema, hadi sasa haijajulikana Mbowe atafanyiwa upasuaji mara ngapi baada ya huo wa kwanza kukamilika, au matibabu yake yatachukua muda gani.

“Pamoja na kwamba hatuna uhakika atalazimika kufanyiwa upasuaji mara ngapi, au uchunguzi na matibabu ya ziada yatachukua muda gani na yatabaini nini, tunayo matumaini kuwa Mwenyezi Mungu atamsaidia kupona kwa haraka na kumrudisha katika siha njema wakati madaktari wakitimiza wajibu wao wa kumtibu,” amesema Makene.

error: Content is protected !!