October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbowe amshangaa IGP Sirro kuwepo madarakani

Spread the love

 

KIONGOZI wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe amesema, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro hapaswi kuwa ofisini kwa matendo yanayofanywa na jeshi analoliongoza. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mbowe amesema hayo leo Ijumaa, tarehe 18 Machi 2022, makao makuu ya Chadema, Kinondoni jijini Dar es Salaam, wakati akitoa maazimio ya kamati kuu ya chama hicho iliyokutana jijini humo juzi Jumatano, 16 Machi.

Mara baada ya kumaliza kuzungumza, ameulizwa maswali mbalimbali na waandishi na moja ya swali aliloulizwa na waandishi anazungumziaje kauli ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyoitaka Serikali kutizama upya mwenendo wa jeshi la polisi.

Akijibu swali hilo, Mbowe amesema, “Kauli ya CCM kwamba jeshi lijitathimini ni kauli tumeihubiri miaka na miaka, nashangaa leo Sirro yuko ofisini. CCM chama kinachoongoza nchi kinasema jeshi lijitathimini, Sirro yujo ofisini? Kwa mazingira ya kawaida lazima ujiuzulu.”

Mbowe amedai, Jeshi la Polisi limechafuliwa na baadhi ya askari polisi wanaowafanyia ukatili raia ikiwemo kuwabambikia makosa.

“Hayo mauaji mmeyasikia yamefanyika Mtwara, siwezi kuzungumzia sababu sina ushahidi, nayo ni sehemu ya ukatili unaofanywa, yawezekana sio mkakati wa jeshi zima lakini ni wa polisi mmoja mmoja,” amesema Mbowe.

Mbowe amedai, alipokuwa mahabusu ya Kituo cha Polisi cha Oysterbay, jijini Dar es Salaam, Julai 2021, aliwakuta vijana takribani 40, ambao wamekamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za udhururaji, ambao walikaa wiki tatu bila ya kuwa na mawakili au familia zao kujulishwa.

Amedai, alipoamua kuwasaidia kwa kuwapa mawakili, alihamishwa upesi kwenda Gereza la Ukonga,jijini humo, huku mtoa taarifa akihamishwa kituo cha polisi.

Kamati kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan iliyokutana Ijumaa iliyopita Ikulu jijini Dodoma, pamoja na mambo mengine ilitoka na mazimio dhidi ya Jeshi la Polisi.

CCM kilisema utendaji wa Polisi hauridhishi, kutokana na matendo yanayofanywa na baadhi ya maofisa na askari wake kuwa kinyume na mwongozo wao wa utendaji kazi.

“Kamati Kuu ya CCM, imeielekeza Serikali kuangalia upya mwenendo wa Jeshi la Polisi nchini, ambao hauridhishi na kulalamikiwa na wananchi kutokana na matendo yanayofanywa na baadhi ya maofisa na askari wa Jeshi hilo, kinyume na mwongozo wa utendaji kazi wa Polisi,” alisema Shaka Hamdu Shaka, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM akizungumza na waandishi wa habari akitoa maazimio ya kikao hicho.

CCM ilitoa maagizo hayo kwa Serikali ikitanguliwa na kauli aliyoitoa Rais Samia dhidi ya Jeshi la Polisi tarehe 4 Februari 2022 akiwa Magu, Mwanza wakati akielekea Mara kwa ziara ya kikazi.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Ilikuwa ni muda mfupi baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuf Masauni kushindwa kuzungumzia mauaji yaliyotokea mkoani Mtwara ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis mkazi wa Luponda, Nachingwea, Lindi, anayedaiwa kuuawa na polisi na kuporwa Sh milioni 70 Mtwara yaliyodaiwa kufanywa na polisi huku wakiunda tume kujichunguza.

Baada ya Masauni kuzungumza, Rais Samia alisema: “Kuna mauaji yametokea Mtwara na kwa taarifa zilizopo ni Jeshi lako ndilo limefanya mauaji.

“Kwa maana hiyo, taarifa niliyonayo, Jeshi limetengeneza kamati ya kufuatilia mauaji hayo, haiwezekani Jeshi lifanye mauaji, Jeshi lichunguze lenyewe,” alisema Rais Samian a kuongeza:

“Waziri Masauni nataka Jeshi lako lijitafakari, wanaone kama kinachotokea ndiyo misingi ya Jeshi la Polisi au vinginevyo.”

Hivi karibuni, IGP Sirro alisema kuna baadhi wanamchukia kwa utendaji wake.

“Wakati mwingine unaweza kumchukia mtu, ukamchukia mtu kama Sirro lakini usichukie taasisi, unaweza kumchukia Sirro kwa sababu labda kakukwaza, lakini si taasisi,” alisema na kuongeza:

“Sirro anaweza kutoka, lakini umuhimu wa taasisi ukabaki palepale, Sirro anaweza kutimiza wajibu wake, lakini ukamchukia kwa sababu ya wajibu wake, mchukie Sirro kama Sirro, lakini si taasisi, kwani inafanya kazi kubwa,” anasema.

error: Content is protected !!