July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbowe ametoka magereza na mtaji wa kisiasa

Spread the love

LICHA ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kusota kwenye kuta za gereza la Ukonga kwa siku 226, ametoka akiwa karata ‘turufu’ ya kisiasa.

Mbowe na wenzake watatu akiwemo Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa (Adamoo) na Mohammed Abdallah Ling’wenya walishtakiwa kwenye shauri namba 16 la mwaka 2021 lililohusu makosa ya Ugaidi kwenye hati ya mashtaka iliyobeba kichwa cha shauri la uhujumu uchumi.

Siku alizokaa Mahabusu Mbowe ni sawa na saa 5424 au sawa na dakika 325,440 au sekunde 19,526,400 ambapo katika maisha ya kawaida tu hakuna mtu angependa kukaa hata kwa dakika moja tu.

Mbowe kama viongozi wengine waliopita kwenye mateso, amenufaika na huruma ya umma ‘Public Sympathy’ ambayo kwa mwanasiasa ni mtaji wa kujiimarisha zaidi.

Mathalani, Rais wa sasa wa Zambia Hakainde Hichilema ni miongoni mwa wanasiasa waliotoka kwenye kuta za magereza hadi Ikulu; Nelson Mandela, kutoka kuwa mfungwa kwa miaka 27 jela hadi kuwa Baba wa Taifa la Afrika Kusini.

Hata hivyo, karata hiyo inaweza isiwe na nguvu kama haitatumika vizuri. Zimebaki siku nyingi sana kutoka leo hadi kufikia mwaka 2024 kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na upepo wa kisiasa unaweza kubadilika siku yeyote na hapo kati kunaweza kukatokea matukio mengi makubwa na kila jipya likaua la nyuma. Mfano tukio la kushtakiwa Mbowe kuliliondolea umaarufu tukio la Kushambuliwa kwa risasi 16 kwa mwanasiasa Tundu Lissu Septemba 2017 Area ‘D’ jijini Dodoma.

Lissu alikuwa maarufu tukio la kushambuliwa lilimuongezea umaarufu nje na ndni na kupata Huruma ya Umma na ndiyo maana hata chama chake waliona ni mtu anayeweza kulenta upinzania katika Uchaguzi Mkuu na kumteua kuwa mgombea wa urais.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanaeleza kuwa kwenye siasa huruma ya Umma inaweza kumfanya mwanasiasa kushinda wapinzani wake kwenye uchaguzi kwa kura ziitwazo kura za maruhani ambazo zinatokana na wapiga kura wasiokuwa wanachama wa chama chochote cha siasa.

Pia mwanasiasa huyo anaweza kuvuna kura kutoka kwa watu wengine waliokuwa kwenye vyama vingine vya siasa kwa kuona mwanasiasa huyu anaonewa au yupo upande wa haki ndio maana anafanyiwa hayo yote.

Njia pekee ya Chadema kuendelea kutumia tukio la Mbowe ni kuendelea na ziara za kisiasa nchi nzima na yeye awe ndio kinara wa ziara hiyo.

Pili ni kushinikiza jukwaa la mikutano ya hadhara kurejeshwa jambo ambalo halina mchakato mrefu wala upinzani mkubwa kama ule mchakato wa kusaka Katiba mpya.

Tatu ni kuunga mkono jitahada za wapinzani wengine ambazo zilishaanza kutoa taswira ya mafanikio kama vile jitihada za makusudi za kusaka tume huru ya uchaguzi ambapo mchakato wake unaonekana kama umeshawiva.

Mbowe pia ana mtaji mwingine wa kupata Coverage ya vyombo vya habari vya ndani na nje hivyo kwenye matukio yatakayoandaliwa na chama hicho yataendelea kumuuza na chama chake.

Aidha Mbowe na Chadema wanatakiwa kubuni njia nyingine za kuwafikia watanzania wote wakiwa tayari wana mtaji wa mapokezi makubwa mikoani.

Chadema ina fursa ya kuomba pesa kwa mataifa na mashirika yaliyowiwa kwenye kukuza demokrasia kwenye nchi za Afrika. Hoja ya kuomba pesa hizo ni ileile tu kwamba chama kilikua kikishughulishwa na kesi ya Mwenyekiti hivyo kimepoteza uwezo wa kujiendesha hasa kufanya ziara na mikutano.

Mbowe ataweza kuwa karata ya kuwauza wagombea mbalimbali wa chama chake mbele ya wananchi. Chadema kitaweza kujiimarisha na kuendelea kuwa chama kikuu cha upinzani nchini.

Utamaduni wa siasa nchini huenda sambamba na matukio karata hii inaweza isidumu hasa ikiwa haitumiki inaweza kupitwa na wakati na wanasiasa wa upande mwingine wakaamua kutengeneza matukio ya kimkakati. Makala haya yameandaliwa na Mwandishi Wetu… (endelea)

error: Content is protected !!