FREEMAN Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amesema, Halima Mdee, Zitto Kabwe na Shaibu Akwilombe ni miongoni mwa watu waliomsukuma kubadili uamuzi wake wa kugombea urais Tanzania katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Mbowe ametoa kauli hiyo, tarehe 4 Mei 2021, akielezea historia yake ndani ya Chadema katika kipindi cha ‘Zungumza na Tundu Lissu’ kinachorushwa mtandaoni.
Akielezea historia hiyo, Mbowe amesema 2005, Chadema walimuomba awe mgombea urais wake, lakini alikataa kutokana na ukosefu wa rasilimali fedha na watu, katika kuendesha mchakato wa uchaguzi huo.
“2005 wakanipendekeza niwe mgombea wa urais, sikuwa nimejiandaa na chama kilikuwa hakina nafasi ya kuwa na wagombe wa urais, lakini watu walilazimisha wakisema ili chama kikue inabidi na sisi kwa mara ya kwanza tusimamishe mgomba urais.”
“Wakasema Mbowe si yupo, huyo huyo anafaa, wakati huo chama hakina fedha, timu ya kampeni ya urais wala gari. Wakasema Mbowe mgombea urais, nikakataa kabisa,” amesema Mbowe.
Amesema, baada ya kugoma kuwa mgombea, Akwilombe, Mdee na Zitto walimfuata na kumshinikiza akubali wito huo, kwa masharti ya kwamba akikataa wataondoka ndani ya Chadema.

“Baadhi ya viongozi wa chama akiongozwa na Shaibu Akwilombe akiwa Naibu Katibu Mkuu, Mdee na Zitto, wakanifuata wakaniambia lazima ugombe urais. Kama hugombei, tunaondoka Chadema, nikajikuta nakuwa mgombea urais toka 2005,” amesema.
Tayari Mdee amefukuzwa ndani ya Chadema kwa tuhuma za usaliti kufuatia hatua yake ya kukubali uteuzi wa ubunge viti maalum 2020, huku Zitto akiwa Kiongozi wa ACT-Wazalendo baada ya kufukuzwa na chama hicho mwaka 2014. Akwilombe alihamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mbowe amesema, uamuzi wa Chadema kumuomba awe mgombea urais katika uchaguzi huo, ulichukuliwa baada ya waliyemteua mwanzo, Prof. Mwesiga Baregu, kukataa kugombea kutokana na sababu za kifamilia.
“Wakati huo tukapendekeza Prof. Baregu kuwa mgombea wa chama, akaenda kuiambia familia yake kwamba nimeteuliwa kuwa mgombea urais. Mama akamwambia, ukiendelea na hiyo kazi tuna achana leo, mwisho Prof. Baregu akajitoa, tulisikitika sana,” amesimulia Mbowe.
Katika uchaguzi huo, Mbowe alichuana na wengine tisa akiwemo Jakaya Kikwete (CCM), Prof. Ibrahim Lipumba (CUF), Augustine Mrema (TLP) na Sengondo Mvungi.
Katika uchaguzi huo, Mbowe alishika nafasi ya tatu baada ya kupata kura 668,756 (5.88%), Prof. Lipumba alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 1,327,125 (11.68%) na Kikwete akiibuka mshindi baada ya kupata kura 9,123,952 (80.28%).
Leave a comment