June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbowe adaiwa kufikishwa mahakamani kimyakimya, asomewa shitaka la ugaidi

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

 

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam na kusomewa mashtaka ya ugaidi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje Chadema, John Mrema, mwanasiasa huyo amefikishwa mahakamani leo tarehe 26 Julai 2021.

Taarifa hiyo imedai kuwa, Mbowe alifikishwa mahakamani hapo kimya kimya, bila ya kuwa na uwakilishi wa wanasheria au familia yake.

“Tumepokea taarifa za hivi punde kuwa, mwenyekiti amefikishwa katika Mahakama ya Kisutu na amesomewa mashtaka ya ugaidi.

“Hii ni pamoja na ukweli kuwa, familia na mawakili wake walijulishwa kuwa wanampeleka hospitali na hivyo alifikishwa mahakamani kimyakimya bila kuwa na uwakilishi wa wanasheia wala familia yake,” imedai taarifa ya Mrema.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Chadema, Mbowe baada ya kusomewa mashtaka hayo, alipelekwa mahabusu katika Gereza la Ukonga jijini Dares Salaam.

Mbowe alikamatwa na Jeshi la Polisi, akiwa katika Hoteli ya Kingdom jijini Mwanza, usiku wa kuamkia tarehe 21 Julai 2021, akijiandaa kushiriki kongamano la kudai katiba mpya, lililoandaliwa na Chadema.

Baada ya kukamatwa jijini Mwanza, alisafirishwa na kukabidhiwa kwa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kwa ajili ya mahojiano dhidi yatuhuma za ugaidi zinazomkabili.

error: Content is protected !!