September 25, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mbivu, mbichi kesi ya Mbowe Jumatatu ijayo

Spread the love

 

HATMA ya kusikilizwa ama kutosikilizwa  kesi ya uhujumu uchumi, yenye mashtaka ya kula njama za kufanya ugaidi iliyoko katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, itajulikana Jumatatu, tarehe 6 Septemba 2021. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Hatma hiyo itajulikana baada ya mahakama hiyo, mbele ya Jaji Elinazer Luvanda, kutoa uamuzi wa mapingamizi matatu, yaliyowasilishwa na Mawakili wa utetezi, wakiongozwa na Peter Kibatala akisaidiana na Jeremiah Mtobesya, wakipinga wateja wao wasisomewe hati ya mashtaka kwa madai kwamba, ni batili kutokana na kuwa na mapungufu kisheria.

Tarehe ya kutolewa uamuzi huo, imepangwa leo Ijumaa, tarehe 3 Septemba 2021 na Jaji Luvanda, baada ya kupokea hoja za pande zote mbili, dhidi ya mapingamizi hayo yaliyowasilishwa Jumatano iliyopita mahakamani hapo.

Katika mapingamizi hayo, mawakili wa utetezi wanadai hati ya mashtaka haioneshi nia ya washtakiwa kutenda kosa la kula njama za kufanya ugaidi, huku lingine likiwa ni makosa kujirudia katika hati ya mashtaka na la mwisho ni taarifa zilizomo katika hati hiyo, kuwa na kasoro.

Mawakili wa utetezi waliweka mapingamizi hayo wakiomba mahakama hiyo, iwaache huru washtakiwa kwa madai kwamba hati ya mashtaka inakosa nguvu ya kisheria kusikilizwa mahakamani hapo.

Wakijibu pingamizi la hati ya mashtaka kutoonesha nia ya washtakiwa kutenda kosa, Jopo la Mawakili wa Jamhuri, wakiongozwa na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Robert Kidando ns Nassoro Katuga, wamesema halina nguvu kisheria.

Wawakili hao walidai, mbali na Sheria ya Kuzuia Ugaidi kuwa na uwezo wa kutafsiri makosa hayo, mahakama hiyo ina uwezo wa kutoa tafsiri iwapo mashtaka yaliyomo katika hati ya mashtaka, ni makosa.

Katika pingamizi dhidi ya mashtaka kujirudia katika hati hiyo, mawakili wa Jamhuri wameipinga wakidai hayajajirudia, kwani kila shtaka linasimama peke yake kwa mujibu wa sheria.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema na wenzake wakiwa mahakamani

Mawakili hao wa Jamhuri, wameiomba mahakama hiyo itupilie mbali mapingamizi hayo, ili kesi husika iendelee kusikilizwa.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni, Halfani Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Lingwenya.

Mbowe na wenzake wanashtakiwa kwa mashtaka sita , ikiwemo la kula njama za kufanya ugaidi na shtaka la kutaka kudhuru viongozi wa Serikali, akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya,  yanayowakabili wote,

Na shtaka la kufadhili vitendo vya ugaidi,  kwa kutoa fedha za kufadhili ugaidi, linalomkabili Mbowe peke yake.

Washtakiwa hao wanadaiwa kufanya makosa hayo kati ya tarehe 1 hadi 5 Agosti 2021, katika maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro na  Morogoro.

error: Content is protected !!