January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbio za urais 2015: Nani maarufu kuliko chama?

Kamati Kuu ya CCM

Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM, wakiwa katika moja ya vikao vyake

Spread the love

VITA vya kusaka urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), vimezidi kupamba moto. Tayari wanaotajwa kuwa “rais watarajiwa,” wameunda mitandao ya kumchafua yule na kumjenga huyu.”

Wengine wametembelea baadhi ya mikoa na wilaya kutafuta uungwaji mkono. Wengine wameanza kupanga safu ya kuingia ikulu.

Wapo walioanza kutafuta viongozi mashuhuri kutoka mikoa yenye wapigakura wengi “hasa eneo la kanda ya Ziwa Viktoria” kushawishi na ikibidi hadi kutumia “nguvu za giza” katika kutimiza mradi wao huu.

Kwa bahati mbaya, siyo mwenyekiti, Rais Jakaya Kikwete, makamu wake wawili – Philip Mangula (Bara) na Dk. Alli Mohammed Shein (Visiwani) – katibu mkuu, Abdulrahaman Kinana na viongozi wengine wa chama hicho tawala, walioweza kulishughulikia suala hili kikamilifu.

Wote wameishia kuunda kamati na tume; na kutoa matamko kupitia idara ya uenezi.

Hii ni kwa sababu, chama hakina ajenda maalum kwa wagombea wake. Wenye ajenda ni wagombea; chama kinachotegemea ajenda kutoka kwa wagombea wake, kinahatarisha uhai wake. Hii ni kwa sababu, ajenda ya wagombea yaweza kuwa kabuli kwa chama!

Chama cha aina hii, hasa kinapokuwa chama tawala, kinapoteza mvuto. Kinakuwa chama mfu. Hakina sifa wala uhalali wa kushughulikia wale wanaokiuka maadili na miiko iliyowekwa na chama. Umaarufu wa chama ukishuka, huku umaarufu wa wagombea ukiwa umepanda, ni dalili ya chama hicho kushindwa kuongoza mabadiliko katika jamii.

Pale chama kinaposhindwa kuongoza mabadiliko kwa kuachana na mazoea, kinaangukia katika hatari ya kubadilishwa. Hii ni kanuni ya vyama vya siasa; yaani ama chama kiongoze mabadiliko au chenyewe kibadilike.

Umaarufu wa chama huporomoka pale chama kinapokosa ujasiri unaotokana na uadilifu wake. Dalili hii huonekana pale chama kinapokosa uthubutu wa kufanya maamuzi na kubaki na kigugumizi kisichokwisha, huku kikitetemekea umaarufu binafsi wa wanachama.

Aidha, umaarufu binafsi wa wagombea usiotokana na umaarufu wa chama, waweza kushughulikiwa pale chama kinapokuwa na watu wenye uthubutu wa kiuadilifu ndani ya chama husika.

Uthubutu wa chama kama taasisi hauwezi kufanywa na kundi, bali hufanywa na viongozi walio tayari. Ni wale wanaoweza kukiambia chama ukweli na katika njia ya wazi; ndani na nje ya vikao. Hakuna chama kinachoweza kuambiwa mafichoni.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alikuwa ni mtu namna hiyo. Hakukiambia chama chake gizani. Alikiambia hadharani. Akapachikwa jina la “Nabii wa kisiasa.” Unabii haufanywi na kundi, bali hufanywa na mtu au kundi dogo.

Kinachoonekana kwa sasa ndani ya CCM, ni uwepo wa watu wachache wenye uthubutu, lakini usiotokana na uadilifu wao. Ni uthubutu unaotokana na kutumwa na wenye fedha. Pale chama kinapofikia katika hatua hii, kutahitajika mabadiliko makubwa ndani ya chama, yasipopatikana toka ndani, yatatafutwa kwa nguvu nje ya chama.

Hivyo basi, ukiwatazama kwa undani wanachama wa chama hiki waliokwishatangaza nia, utagundua kuwa wamegawanyika katika makundi makubwa manne kwa muktadha na mustakabali wa CCM.

Kwanza, kuna wagombea ambao chama hiki ikidiriki kuwagusa, kitaweza kufutika katika daftari la msajiri wa vyama vya siasa. Kundi hili linaongozwa na aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowasa. Huyu akiguswa chama kitafutika.

Nguvu ya Lowasa inafahamika. Inatokana na ukweli kuwa ndiye aliyemweka madarakani, rais Jakaya Kikwete. Kumgusa Lowasa, ni kumgusa Kikwete.

Aidha, Lowasa ana fedha, tena nyingi. Hii ni kete muhimu katika taifa linalotajwa kuongoza, miongoni mwa nchi zenye rushwa ya hali ya juu. Sifa hii inakubalika pia ndani ya chama chake.

Vilevile, Lowasa ana mtandao ndani na nje ya CCM. Karibu robo tatu ya wajumbe wa NEC wanamuunga mkono yeye. Ana idadi kubwa pia ya wanaomuunga mkono kimya kimya ndani ya Kamati Kuu (CC).

Siyo hivyo tu: Lowasa anamiliki mfumo wa usalama nje ya idara rasmi ya usalama. Mfumo huu umekarabatiwa na magwiji wa usalama walio kazini na wastaafu. Ameutumia mfumo huu kujua mambo mengi ya utawala na watawala.

Katika lindi la ufisadi, ni miongoni mwa wanaotajwa. Ana mali na ana habari. Mtu anayejua mengi, ni hatari kuliko mwenye mali nyingi. Hakuna fisadi mbinafsi. Wengi wao, ni wakarimu; na kwa ukarimu wao, hupata mengi hata kwa kulazimishwa.

Kwa hali ilivyo, Lowasa anapata habari nyingi kuhusu wanaomkamia kuliko wao wanavyopata habari zake. Kikwete analijua hili na ndiyo maana amekuwa mkimya na mgumu wa kukaripia Lowasa. Anajua akimsema, yatamfikia mhusika.

Pili, kuna wagombea ambao chama kikiwagusa, kitayumba. Miongoni mwa ambao chama kikiwagusa bila uangalifu kitayumba, ni pamoja na Fredrick Sumaye na January Makamba.

Kwa mfano, Sumaye ameonyesha msimamo usioyumba dhidi ya rushwa na ufisadi. Katika hili, hamung’unyi maneno. Ujumbe wake haubadilikibadiliki hata kama anabezwa na baadhi ya wenzake ndani ya chama.

Hii ndiyo ajenda yake. Siyo ya chama chake. Ajenda hii inapendwa na wengi; akiguswa bila uangalifu, CCM kitayumba na hata kupasuka.

Hii ni kwa sababu, mbele ya jamii, chama kitaonekana rasmi kuwa ni chama cha wala rushwa, mafisadi na watu wanaogombania madaraka kwa maslahi binafsi.

Naye January ameingia na ajenda ya umri. Pamoja na ajenda hii kubezwa na wengi, lakini ndiyo iliyotumiwa na Kikwete kuingia Ikulu mwaka 2005.

January anajua kuwa wapigakura wengi, ni vijana na analenga kutumia mihemuko yao na umaskini wao, kukiyumbisha chama chake ili kisimchukulie hatua.

Mpaka sasa, CCM hakina mgombea kijana mwenye mvuto kuliko yeye na hakina mgombea mwenye ujumbe kwa vijana zaidi ya ahadi hewa. January amelijua hilo na kuliwahi.

Aidha, uzoefu wake katika mizengwe ya ikulu, usalama na sekretariati ya chama iliyoongozwa na baba yake, vinamvimbisha kichwa kisicho na nywele. Umri peke hauwezi kumvusha; lakini umri pekee utakiyumbisha chama.

Tatu, kuna wagombea ambao CCM ikiwagusa vibaya, chama kitapata homa kali, lakini inayoweza kutibika. Walioko katika kundi ambalo chama kitapata homa, ni pamoja na Samwel Sitta, Harrison Mwakyembe na Steven Wassira.

Sitta ana uthubutu wa kauli zisizopimwa. Anaweza kuvaa bomu na kujilipua. Uzoefu wake katika mtandao, spika wa bunge na sasa bunge la katiba, vinamfanya kuwa maarufu kuliko chama chake.

Kwa upande wa Mwakyembe, yeye ana uthubutu binafsi usiotokana na uthubutu wa dola wala chama chake. Katika taifa ambalo limepooza kwa kukosa uongozi na maamuzi (ombwe), umaarufu wake unaweza kuonekana ni tishio kwa chama chake. Akiguswa bila ungalifu, chama “kitapata homa kali.”

Naye Wassira ndiye ngome ya CCM na serikali kwa sasa. Ana ushawishi na uthubutu wa kauli ndani na nje ya chama. Ni mtu ambaye amejijenga kwa muda mfupi kupitia nafasi yake ya uwaziri na ujumbe wa CC.

Udhaifu wa chama na uongozi wa serikali vimechangia kumpa umaarufu unaoonekana kuwa juu ya umaarufu wa chama chake. Ni kwa sababu hiyo akiguswa bila tahadhari, CCM itapata homa kali.

Nne, kuna kundi la wagombea ambao chama kikiwagusa, hapatakuwa na athari zozote kwa chama wala nchi. Waliomo katika kundi hili, ni Benard Membe, William Ngereja, Dk. Asha-Rose Migiro, Mizengo Pinda na Dk. John Pombe Magufuli.

Hawa wanaweza kuwa turufu nzuri ndani ya chama, lakini urais ni zaidi ya mambo ya chama kimoja. Kwa maneno mengine, udhaifu wa kundi hili ndiyo nguvu ya CCM. Ukimwondoa Membe, hili ni kundi ambalo halijasababisha migawanyiko wowote ndani ya chama; kwa sababu liko kimya na kwa kiasi kikubwa halijajishughulisha kuunda mitandao ya urais.

Yoyote atakayeteuliwa miongoni mwa wagombea hawa, hana madhara kwa chama. Asipoteuliwa pia hana madhara. Membe nimemuunganisha na kundi hili kwa sababu moja tu: Akichukuliwa hatua na kutishia kujitoa katika chama, hakuna uhakika kama kuna wafuasi watakaomfuata.

Udhaifu wa jumla wa kundi hili, ni pale inapoonekana kuwa akiteuliwa mmoja wao, chama kitapata taabu sana kumnadi mbele ya wapigakura.

Hii ni kwa sababu chama chenyewe si maarufu tena na kinaishi kwa kutegemea umaarufu wa watu binafsi na ulinzi wa dola. Kumsimamisha mgombea asiyejiuza kwa sifa zake, ni sawa na kubeba zege lililolala.

Hivyo basi, kwa muktadha wa yote haya, chama hiki CCM kikifanikiwa kunyakua tena mamlaka ya dola mwaka 2015, basi taifa hili litarejea kulekule kwa kuongozwa na mtu anayetumia umaarufu binafsi kuliko umaarufu wa chama na sera. Mungu atuepushe na hilo.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa email:  tutikondo@yahoo.com

error: Content is protected !!