June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbinu za utayarishaji wa chakula cha mtoto

Spread the love

MARA nyingi wazazi wamekuwa wakiwalalamika kuwa mtoto wao hawapendi kula au huwa wanachagua baadhi ya vyakula. Akina mama wengi huwa hawajui chanzo cha tatizo ndio maana huishia kuwalaumu watoto lakini kumbe wazazi wenyewe ndio wameshindwa kutumia mbinu mbalimbali za kutengeneza chakula cha watoto wao na kuwawezesha kuzoea vyakula hivyo.

Kwa kawaida watoto wanapozaliwa chakula wanachokijua wao ni maziwa ya mama tu, na wanapaswa kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee (exclusive breast feeding) kwa miezi sita ya mwanzo, na tunaposema maziwa pekee hapa hapaswi kupewa hata maji ya kunywa zaidi ya maziwa ya mama.

Baada ya miezi sita mtoto anapaswa kupewa vyakula vya nyongeza (chakula cha kulikiza) na hapa ndipo anapoanza kujifunza aina nyingine ya chakula tofauti na maziwa ya mama aliyoyazoea.

Hiki ni kipindi muhimu kwa mtoto kuweza kujifunza ladha na aina tofauti ya chakula. Kumbuka kila chakula atakachoanzishiwa mtoto lazima apewe muda wa kuzoea ladha hiyo kabla ya kuanzisha chakula kingine ili kumfanya mtoto kuzoea ladha ya chakula husika.

Katika kipindi cha kumuanzishia mtoto chakula cha ziada ni muhimu sana kujua mtoto anakula nini na anapata nini kwa kile anachokula, kwani tabia ya ulaji unaofaa hujengwa kuanzia utotoni.

Katika maandalizi ya chakula, chakula cha asili alichokitengeneza mama mwenyewe kwenye mazingira ya nyumbani kinaweza kuwa bora sana kuliko vyakula vya makopo au vilivyotengenezwa viwandani kwani mama anakuwa na uhakika na anafahamu ni chakula gani amempa mtoto wake.

Faida za kutengeneza chakula cha mtoto ni nyingi ikiwa ni pamoja na kujua kwa uhakika kile unachomlisha mtoto wake, ni rahisi ukilinganisha na vyakula vya kununua madukani, unakuwa na wigo mpana wa kuchagua aina ya chakula na ladha tofauti tofauti badala ya kutegemea ladha ya muandaaji kiwandani, hii inamsaidia mtoto kuzoea kula vyakula ambavyo familia inatumia.

Katika maandalizi haya ya vyakula vya mtoto, jambo la msingi kwa mama anayeandaa ni kuhaakikisha ana jipa muda wa kutosha na sehemu nzuri ya kuhifadhia chakula kwa usafi na usalama.

Kuna mbinu nyingi zinazoweza kutumika ili kukifanya chakula cha mtoto kiwe bora zaidi, rahisi kula na kutumika mwilini na pia kuwa na ladha ya kuvutia wakati wa kula.

Moja ya njia hizi ni kuandaa chakula kwa kuponda au kusaga. Kitendo cha kuponda au kusaga chakula hukifanya chakula kiwe bora zaidi, rahisi kula na pia husaidia mmeng’enyo wake tumboni. Vyakula vinavyoweza kupondwa ni pamoja na ndizi, viazi, ubwabwa, nk.

Chakula kilichosagwa
Chakula kilichosagwa

Ni vizuri kutumia maziwa au mchuzi wa nyama, samaki au maharagwe kama maji ya kupondea chakula badala ya maji yenyewe. Pia ikumbukwe unaweza pia kuponda au kusaga nyama au hata samaki na kumpa mtoto badala ya kumpa mchuzi wake tu.

Ni muhimu kukumbuka pia unapoponda chakula cha mtoto unazingatia mlo kamili kwa maana ya kugusa makundi yote ya vyakula kama tulivyoona kwenye mada ya Mlo kamili huko nyuma.

Mbinu ya pili ni Kuongeza vyakula vyenye virutubishi vingi. Ni muhimu kuongeza vyakula venye virutubishi kwa wingi kwenye vyakula hasa vile vya wanga. vyakula vinavyoweza kuongezwa ni pamoja na karanga, maziwa, mbegu mbalimbali zitoazo mafuta zilizopondwa, mafuta au tui la nazi, ili kuongeza ubora wa chakula. Kumbuka tunapotumia karanga tunapaswa kuwa waangalifu na kuzikagua karanga kuhakikisha kwamba zote ni nzima na hazina ukungu.

Mbinu ya tatu ni kuchachusha vyakula (fermentation). Kitaalamu vyakula vilivyochachushwa huyeyushwa kwa urahisi na hatimaye virutubishi kusharabiwa kiurahisi. Aidha vyakula vilivyochachushwa vimeonekana kusaidia uyeyushwaji wa vyakula vingine na ufyonzwaji wa virutubishi kiurahisi. Baadhi ya vyakula hivi ni kama maziwa ya mtindi, togwa na vinywaji vingine vilivyochachushwa ambavyo havina kilevi.

Kuna njia nyingi za kuchachusha nafaka kwa ajili ya kutengeneza uji wa mtoto moja wapo ni. Mojawapo ni uchachushaji wa unga kwa ajili ya kuandaa uji wa mtoto. Uchachushaji huu unafanyika kwa kuchukua unga wa nafaka na kuuloweka kwenye maji (vikombe vitatu vya unga kwa maji vikombe saba), baada ya hapo uweke mchanganyiko huu uchachuke kwa muda wa siku mbili au tatu, halafu mchanganyiko huo uliochechushwa utumike kwa kutengeneza uji kwa ajili ya mtoto wako.

Njia ya nne ya uandaaji wa chakula cha mtoto ni kwa kuotesha nafaka (germination/sprouting). Kama ilivo kwa vyakula vilivyochachushwa, vyakula vilivyooteshwa huyeyushwa kwa urahisi na husaidia uyeyushwaji wa vyakula vingine. mbegu mbalimbali za nafaka na mikunde huweza kuoteshwa na kutumika kama vyakula au pamoja na vyakula mbalimbali.

Nafaka zilizooteshwa
Nafaka zilizooteshwa

Mbegu hizo ni kama mbegu za mahindi, mtama, ulezi, uwele, choroko, kunde, maharage nk. Mbegu zilizooteshwa sio lazima zikakaushwa na kutengenezwa unga, zipo ambazo zinaweza kupikwa mara tu baada ya kuota na kutumiwa kama mboga. kwa mfano maharage, njegere, choroko, kunde n.k.

Uoteshaji nafaka hufanyika kwa kuchukua mbegu za nafaka kwa kuzichambua na kuzisafisha vizuri. Baada ya hatua hii zinapswa kulowekwa kwa muda wa siku moja, baada ya siku moja zitolewe na ziweke kwenye kitambaa safi na kufunikwa, ziachwe kwa muda wa siku mbili mpaka tatu au mpaka zianze kuota, halafu zitoe na zianikwe kwenye jua, zikikauka zisagwe tayari kupata unga wa kutengeneza uji.

Ungana nami katika makala ijayo ili uone ni namna gani unaweza kutengenesa uji wa nafaka zilizooteshwa na kuchachushwa.

Imeandikwa na Juma Nziajose, Mtaalamu wa Lishe na Afisa Tabibu- 0718 962336.

error: Content is protected !!