CHRISTOPHER Wray, Mkurugenzi wa Shirika la Upelelezi la Mareani (FBI) amesema, vitendo vya Serikali ya China ni tishio kwa taifa hilo. Inaripoti mitandao ya kimataifa…(endelea).
Akizungumza katika Taasisi ya Hudson ya mjini Washington, Wray amesema China inaendesha upelelezi na wizi jambo ambalo ni tishio kubwa la Marekani katika siku za mbele.
”China imeanza juhudi za kuhakikisha kuwa ndio taifa la pekee litakalokuwa na uwezo mkubwa zaidi duniani kwa hali na mali,” aliongezea.
Mkurugenzi huyo amesema, China imekuwa ikiingilia masuala mbalimbali ya Marekani kupitia kampeni kubwa ya upelelezi wa uchumi wa Marekani, wizi wa data na fedha.
”Tumefikia wakati ambapo FBI sasa imeanza kufungua kitengo cha kukabiliana na visa vya Ujasusi wa China kila baada ya saa 10. Kati ya visa 5000 vya kukabiliana na ujasusi vinavyoendelea kote nchini, karibia nusu yake vinahusishwa na China,” amesema.
Amemtuhumu Rais wa China, Xi Jinping kwamba ameanzisha mpango kwa jina ‘Fox Hunt’, unaowalenga raia wa China ughaibuni wanaoonekana kuwa tishio kwa Serikali ya China.
”Tunazungumzia kuhusu wapinzani wa kisiasa, watoro na wakosoaji walio na lengo la kufichua ukiukaji wa haki za kibinadamu unaotekelezwa na China,” amesema na kuongeza:
”Serikali ya China inataka kuwalazimisha kurudi nyumbani na mbinu zinazotumiwa na China kufanikisha mpango huo inashtua. Inaposhindwa kumpata mtu inayemtafuta, serikali ya China hutuma mjumbe kutembelea familia ya mtu huyo nchini Marekani. Ujumbe unaotolewa ni ‘Rudi China haraka ama jiue.’
Leave a comment