May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbatia: Waliokamatwa na polisi, waachwe huru

James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi

Spread the love

 

JAMES Mbatia, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, amelitaka Jeshi la Polisi nchini Tanzania, kuwaachia Watanzania waliowakamata kwa tuhuma za kusema Rais John Magufuli mgonjwa. Anaripoti Yusuph Katimba, Dar es Salaam … (endelea).

Rais Magufuli alifariki dunia jana Jumatano tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, mkoani Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi tarehe 18 Machi 2021, wakati akitoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Rais Magufuli, Mbatia amesema, wakati huu sio wa kuoneshana mabavu.

“…polisi walikamata watu, wawaache ili kuleta jamii pamoja, walikuwa wanamuulizia rais wao, rais ni mali ya umma,” amesema Mbatia.

Mbatia ametoa kauli hiyo baada ya kutoa pole kwa mjane wa Dk. Magufuli, Mama Janet Magufuli, Mama Samia Suluhu Hassan ambaye ni makamu wa Rais, majirani wa Tanzania na Watanzania wote.

Mbatia amesema, wenye mamlaka wanapaswa kuonesha namna viongozi wanavyopaswa kuwa, na kwamba wanatakiwa kuwa waadilifu na wenye kusema ukweli.

“Rai yangu kwa wenye mamlaka, waoneshe namna viongozi wanavyotakiwa kuwa waadilifu, waseme ukweli na kuwa wawazi. Hili litatuleta pamoja,” amesema.

Mbatia amewataka viongozi wa kisiasa kurudi na kuwa wamoja, licha ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2020, kuacha chuki.

Rais John Magufuli

Amesisitiza kwamba, kwa sasa kuna chuki iliyosababishwa na kile kilichotokea kwenye uchaguzi mkuu, na kwamba ushahidi wa kutokuwepo kwa umoja wa kitaifa unapatikana katika mijadala kwenye mitandao ya kijamii.

“Ni utamaduni wetu harusi na kifo huileta jamii pamoja. Itoshe kusema huu ni wakati wa kushirikiana na kuleta umoja wa kitaifa.”

“Madhila ya uchaguzi uliopita yameacha chuki, ukiangalia kwenye mitandao utaona chuki ipo. Lolote lile liwalo, Tanzania kwanza mengine baadaye. Sisi tutapita Tanzania itakuwepo,” amesema.

IGP Simon Sirro

Amesema, Tanzania kwa sasa kuna nyufa zilizo wazi, hivyo viongozi wa kisiasa wanapaswa kuweka tofauti pembeni na kuwa wamoja sambamba na kutafuta umoja wa kitaifa.

“Ni jambo la wazi katika kipindi hiki tuna nyufa za wazi, ndio maana tunaitaka jamii kushirikiana. Tujitahidi sisi viongozi licha ya tofauti mbalimbali, tuwe pamoja,” amesema.

Kutokana na msiba wa Dk. Magufuli, Mbatia ameagiza bendera ya chama chake kupepea nusu mlingoti kwa siku 21.

error: Content is protected !!