August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbatia: Rais Magufuli si msafi

Spread the love

RAIS John Magufuli anakabiliwa na tuhuma za ubadhirifu, jambo hilo linamwondoa kwenye orodha ya watu wasafi kama anavyotaka ifahamike hivyo, anaandika Pendo Omary.

James Mbatia, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR- Mageuzi amemtaka Rais Magufuli kujisafisha kutokana na kashfa ya kuhusika katika kuuza nyumba za serikali kabala ya kusafisha watuhumiwa wengine wa ufisadi.

“Rais Magufuli anapaswa kujisafisha mwenyewe kwanza kutokana na kashfa inayomuhusu ya uuzwaji wa nyumba za serikali,” amesema Mbatia.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari, Mbatia amesema “tumeona ni kwa namna gani Rais Magufuli anahangaika kupambana na ufisadi au uhujumu uchumi kwa kutumia nguvu kubwa kwa vidagaa na kuacha mapapa kama wale wa Tegeta ESCROW, Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere ‘Terminal III’, makontena bandarini, IPTL, Richmond na Mradi wa Umeme wa Kinyerezi.

“Hivyo rais anapaswa kujisafisha kwanza kwa kuwa na yeye anatajwa kuhusika katika kashfa ya uuzwaji wa nyumba za serikali,” amesema Mbatia.

Mbatia amesema, katika kufanikisha hayo Rais Magufuli anapaswa kuacha kuongoza nchi kwa matamko badala yake aongoze kwa kufuata Katiba, Sheria na Kanuni za Nchi.

“Demokrasia imeendelea kukiukwa huku uhuru wa kujieleza ukiendelea kudidimizwa. Kutokana na hali hiyo, nchi sasa iko kwenye hali mbaya katika; bunge kuingiliwa, hali ya maisha ya Watanzania kiusalama iko njia panda hususani Zanzibar.

Pia, kuna ukiukwa kwa haki za wananchi kutafuta na kusambaza taarifa na matumizi ya nguvu za dola kupitia Jeshi la Polisi kwa kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa vya upinzani.

Aidha, amesema Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (NEC) imebaini athari za kiuchumi zitokanazo na uamuzi wa viongozi kufuatia matamko mbalimbali ya serikali.

Miongoni mwa athari hizo ni kupungua kwa mzigo bandarini ikiwa ni sambamba na watumiaji wa bandari wakihamia nchi jirani.

error: Content is protected !!