July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbatia: Hatutarudi nyuma kudai katiba mpya

James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi

Spread the love

 

MWENYEKITI wa Chama cha siasa cha upinzani nchini Tanzania- NCCR-Mageuzi, James Mbatia, amesema chama chake hakitarudi nyuma katika harakati za kudai Katiba mpya. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mbatia ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, tarehe 8 Julai 2021, akitoa msimamo wa NCCR-Mageuzi, kuhusu madai ya Katiba mpya, katika mkutano wake na wanahabari uliofanyika ofisini za chama hicho, Ilala jijini Dar es Salaam.

“Haturudi nyuma kwenye misingi ili tupate Katiba, kwa sasa tunazungumzia Katiba na hatutarudi nyuma hasirani. Eti mtusubiri tujenge uchumi, no way,” amesema Mbatia.

Mbatia ametoa kauli hiyo akijibu ombi la Rais Samia kwa Watanzania, akiwataka wampe muda ili asimamishe uchumi wa nchi.

Rais Samia, alilitoa ombi hilo katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari, tarehe 28 Juni 2021, kuhusu siku 100 za utawala wake.

Mbati amesema, NCCR-Mageuzi itashirikiana na makundi mbalimbali, yaliyoanzisha vuguvugu la kudai mchakato wa marekebisho ya Katiba, ufufuliwe upya, baada ya kukwama 2015.

“Napongeza vikundi vyote vinavyojitokeza sasa hivi, ili tuwe na Katiba mpya kwa maslahi ya wote na si maslahi ya kikundi kimoja na kwa kuwa ndiyo tumetoka kwenye uchaguzi, yale yote tuliyofanyiwa kwenye uchaguzi hasira tuliyonayo sasa tusirudi nyuma,” amesema Mbatia.

Miongoni mwa makundi yaliyojitosa katika vuguvugu hilo, ni Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO’s) na vyama vingine vya siasa kama Chadema na ACT-Wazalendo.

Mwenyekiti huyo wa NCCR-Mageuzi, amesema Katiba mpya ni takwa la wananchi, hata kama baadhi ya watu hawaliafiki suala hilo.

“Msimamo wetu NCCR-Mageuzi kwenye suala la Katiba, penda tusipende ni takwa la wananchi wa Tanzania.”

“Bunge ni mtoto wa Katiba, mahakama ni mtoto wa Katiba, Serikali ni mtoto wa Katiba. Kwa kawaida mama anamzaa mtoto, mtoto hamzai mama na mama ni Watanzania, ndiyo wenye Katiba,” amesema Mbatia.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Mwanasiasa huyo amesema, kwa sasa nchi iko katika mgogoro wa Kikatiba, kwa madai kwamba wananchi hawaelewi nini kitakachofuata, baada ya mchakato huo kusimama.

“Tufanye nini na tuko kwenye mgogoro, wataalamu wanatumbia mkiwa kwenye mgogoro wowote mnafanya mazungumzo, tunahitaji muafaka wa kitaifa, tunahitaji meza ya mazunguzo kujua tufanye nini hapa tulipo,” amesema Mbatia.

Mchakato wa Katiba mpya ulianza 2011 chini ya Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, ambapo Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Na. 83 /2011 ilitungwa pamoja na Sheria ya Kura ya Maoni Na. 11/2013.

Mchakato huo uliishia Aprili 2015, katika maandalizi ya wananchi kuipigia kura Katiba pendekezwa baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini (NEC), kuahirisha zoezi hilo kutokana na uandikishaji daftari la wapiga kura kutokamilika.

error: Content is protected !!