April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mbatia awavuruga CCM, Chadema Mbeya   

Spread the love

MWENYEKITI wa chama cha NCCR- Mageuzi, James Mbatia, aliyeko mkoani Mbeya, ameanza kwa kishindo ziara yake mkoani humo, kufuatia maelfu ya watu kujitokeza kutaka kujiunga na chama chake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mbeya … (endelea).

Kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa kujitegemea, Merina Robert, aliyeongozana na msafara wa mwenyekiti huyo wa NCCR- Mageuzi anasema kuwa leo Alhamisi, tarahe 5 Machi 2020, Mbatia amepokea mamia ya wanachama wapya wa chama chake, katika jimbo la Busekero, wilayani Rungwe.

Miongoni mwa waliojiunga na chama hicho na kukabidhiwa kadi na Mbatia, ni pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika jimbo la Busekero, Furaha Mwakalundwa.

Mwingine aliyejiunga na NCCR- Mageuzi na kupokelewa na Mbatia, ni aliyekuwa katibu wa jimbo hilo kupitia Chadema, Anyabwile Mwaisile.

Mbali na viongozi hao wawili wakuu wa Chadema katika jimbo la Busekero, uongozi mzima wa Chadema katika jimbo hilo, nao umetangaza kujiondoa ndani ya chama hicho na kujiunga na NCCR- Mageuzi.

Kushamiri upya na kwa kasi kwa chama cha NCCR- Mageuzi, katika jimbo la Busekero na mkoa wa Mbeya kwa ujumla wake, kumefuatia hatua ya aliyekuwa kada mashuhuri wa Chadema mkoani humo, wakili msomi Boniface Mwabukusi, kuamua kujitenga na chama hicho na kujiunga na NCCR- Mageuzi.

Mwabukusi ambaye alijitosa katika kinyang’anyiro cha uenyekiti wa Chadema, Kanda ya Nyasa, alishindwa katika uchaguzi huo wa mwishoni mwa mwaka jana, huku akiwatuhumu baadhi ya viongozi wake wa juu, akiwamo Freeman Mbowe, kumbeba mmoja wa washindani wake.

Katika uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkali, Mwabukusi alipambana na Peter Msigwa, mbunge wa Iringa Mjini. Msigwa anatajwa ndani ya Chadema, kuwa ni miongoni mwa viongozi vipenzi wa Mbowe.

Mbatia na msafara wake, wanatarajiwa kufanya mikutano miwili mikubwa jimboni Busekero; taarifa zinasema, zaidi ya watu 2500, wameomba kujiunga na chama chake.

Katika ziara hiyo, mbali na Mwabukusi ambaye tayari ameteuliwa kuwa Kamishena wa NCCR- Mageuzi, Mbatia ameongozana na aliyekuwa Mratibu wa Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA), Edward Simbeye.

Simbeye alitangaza kuondoka Chadema wiki iliyopita na kujiunga na NCCCR- Mageuzi, kwa kile alichoita, “ni chama kinachoendesha mambo yake kwa uwazi na kwa kuzingatia utu.”

Alikituhumu Chadema kwa kuendesha siasa za upendeleo, ukabila na uvunjaji wa katiba na taratibu ilizojiwekea na kuongeza kuwa “mipango mingi ya chama hicho, hupangiwa kwenye baa.”

Mbali na wanachama wa Chadema, Mbatia amepokea wanachama kadhaa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika jimbo hilo. Jimbo la Busekero, ni miongoni mwa majimbo mkakati ya NCCR- Mageuzi, katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu.

error: Content is protected !!