May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbatia atoa ya moyoni “Rais Samia anahujumiwa”

James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi

Spread the love

 

MWENYEKITI wa chama cha siasa cha upinzania nchini Tanzania cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia amemwomba Rais wa Taifa hilo, Samia Suluhu Hassan kuwa makini na wasaidizi wake “kwani wanamhujumu sana. Kwa nini wanakiuka maagizo yake.” Anaripoti Patricia Kighono, TUDARCo … (endelea).

Mbatia ametoa kauli hiyo leo Jumamosi, tarehe 28 Agosti 2021, makao makuu ya chama hicho, Ilala jijini Dar es Salaam, mara baada ya Jeshi la Polisi kuzuia mkutano wao wa kamati kuu, uliokuwa ufanyikie ukumbi wa Msimbazi Center.

“Hivi hii nchi inaongozwa na nani? Kama Rais ameruhusu mikutano ya ndani sasa kwa nini kikao chetu polisi wamekizuia? Rais atakuwa anahujumiwa bila yeye kujijua. Kama amri jeshi anaweza kutoa kauli isiyoheshimika, hapana, hapana, hapa haiwezekani,” amesema Mbatia.

“Kutakuwa na kitu, kwa nini hawasikilizani kila mmoja anafanya lake, tumehubiri maridhiano, tumeomba mazungumzo lakini wapi? Nimechukia sana. Kwa nini tumezuiwa kufanya kikao chetu tena wa ndani ambao Rais ameiruhusu?” amehoji Mbatia.

Kutokana na ugonjwa wa corona, Rais Samia alikwisha kuruhusu mikutano ya ndani ya vyama vya siasa ikiwemo ile ya kikatiba kama kamati kuu, baraza kuu au halmashauri kuu ifanyike.

Hata hivyo, leo Jumamosi, NCCR-Mageuzi ilipanga kufanya kikao cha kamati kuu chenye wajumbe wasiozidi 30 katika ukumbi wa Msimbazi Center, lakini hakikufanyika baada ya Jeshi la Polisi kufika ukumbini hapo na kuuzuia.

MwanaHALISI Online linaendelea kuutafuta uongozi wa jeshi la polisi ili kujua sababu za kuuzuia mkutano huo.

Aidha, Mbatia amesema tulikuwa tumekwisha “kulipa gharama zote, tumechukua tahadhari zote za corona, ndiyo maana tumeamua kulipia eneo lile kubwa lakini wametuzuia, kuna agenda ya siri hapa. Sisi tunataka tujadili na kuhamamisha watu kuchanja, lakini wametuzuia.”

Amesema, ofisi ya msajili imepanga kutembelea vyama vya siasa na ndiyo moja ya agenda ya kujipanga lakini “kilichofanyika leo ni hujuma. Msajili akija akakuta shagara baghara asituulize, akawaulize polisi kwa nini wametuzuia wakati amri jeshi mkuu amekwisha kuruhusu mikutano ya ndani.”

Mbatia amesema, wamemwagiza Boniface Mwambugusi, mkuu wa sheria na haki za binadamu “waanze mchakato wa sheria, ikiwemo kuchukua hatua ili…huu usimamishwe kwa amri ya mahakama.”

“Licha ya ugumu wa uchumi, watu wametoka maeneo mbalimbali ya nchi, tumetumia zaidi ya Sh.10 milioni halafu mtu mmoja anakuja kuzuia kufanya mkutano, hii haikubaliki kabisa. This is too much,” amesema Mbatia ambaye wakati wote akizungumza ameonekana kuchukizwa na mwenye hasira

“Tunamshauri Rais Samia, tukutane tuzungumze, wasaidizi wako wanakuhujumu sana, Rais tunakutakia mema sana, lakini unapaswa kujiuliza kwa nini unatoa kauli ya kuruhusu mikutano ya ndani halafu wanaizuia wasaidizi wako,” amehoji Mbatia.

error: Content is protected !!