Spread the love

 

MWENYEKITI wa Chama cha NCCR-Mageuzi James Mbatia amefungua Shauri namba 2 la Kikatiba la mwaka 2022 kuzuia uchaguzi wa Spika, akidai mchakato wa kujiuzulu Spika Job Ndugai haukufuata Katiba, Sheria, kanuni na taratibu. Anaripoti Selemani Msuya, Dar es Salaam … (endelea)

Wakati Mbatia akifungua kesi hiyo leo tarehe 21, Januari 2022, jana Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia Kamati Kuu (CC) yake, kimempitisha Dk. Tulia Ackson kuwa mgombea wa U-Spika wa Bunge la Tanzania kupitia chama hicho.

Spika Ndugai alijiuzulu Januari 6 mwaka huu baada ya kutoa kauli kwamba deni la taifa limekuwa kubwa, hivyo nchi inaweza kupigwa mnada.

Akizungumia uamuzi wa kufungua Shauri hilo la Kikatiba, Mbatia alisema yeye ni muumini wa kusimamia Katiba hivyo ameona atumie haki yake ya Kikatiba kuitetea Katiba ambayo inavunjwa.

Amesema Shauri hilo namba 2 la mwaka 2022 limefunguliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania ambapo linatarajiwa kuanza kusikiliwa Jumatatu ya tarehe 24 Januari 2022 mwaka huu, chini ya majaji watatu.

Mwenyekiti huyo wa NCCR amesema ameamua kuandika historia katika kusimamia Katiba, kutokana na ukweli kuwa yeye ameshakula kiapo zaidi ya mara tatu, cha kuisimia, kuhifadhi, kuilinda na kuitetea Katiba kwa kusema Mwenyezi Mungu amsaidie.

“Hapa kwetu Tanzania Katiba tuliyonayo ndiyo inayoweka utaratibu wa namna bora ya kuifanya Tanzania kuwa sehemu salama na bora kuishi. Tumekuja mahakamani kuiomba Mahakama yetu, iweze pamoja na wengine wanaamini upande wa Mwenyezi Mungu iweze kunisaidia kulinda kiapo change mimi binafsi na viongozi wengine ili tuweze kuheshimu Katiba,” amesema.

Mwenyekiti huyo amesema walichowasilisha mahakamani ni namna Spika Ndugai alivyojiuzulu, jambo ambalo yeye anaamini kuwa mchakato uliotumika umeenda kinyume na Katiba.

“Shauri hili ni dhidi ya Job Ndugai, Katibu wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, tukiomba Mahakama iwalazimishe wafuate utaratibu uliowekwa Kikatiba namna ya kuondoka kwenye nafasi hiyo.

“Hatupo Mahakamani ili kusema Ndugai lazima kumtetea yeye la, sisi tunataka utaratibu wa Kikatiba ufuatwe. Tunaamini utaratibu wa Kikatiba ukifuatwa ndipo Tanzania itakuwa sehemu salama na kuishi,” amesema.

Mbatia amesema anaishukuru Mahakama kupokea shauri hilo na kupangiwa jopo la majaji watatu na litaanza kusikilizwa Jumatatu Januari 24 mwakaa huu saa nne asubuhi.

Mwenyekiti huyo amesema hawezi kuzungumzia mchakato wa kumpata Dk. Tulia kupitishwa kuwa mgombea kwa kuwa anaamini mchakato mzima ni batili, huku akiwataka viongozi wenzake kuacha kiburi hadi kufikia hatua ya kutoheshimu Katiba, Sheria na taratibu.

Aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai

Amesema hatua aliyochukua imelenga kutetea vizazi vijavyo katika kuheshimu Katiba na kwamba iwapo hilo likiachwa lipite madhara yake ni makubwa zaidi kwa nchi na wananchi.

Kwa upande wake Wakili wa Kujitegemea Stephen Msechu ambaye amewakilisha mawakili wenzake 10 alisema wameamua kusimamia shauri hilo baada ya kubaini kukiukwa kwa Ibara ya 149, Ibara ndogo ya 1 (c) imeweka utaratibu mzuri namna ya Spika kujiuzulu ambapo ni kupeleka taarifa Bungeni.

Wakili Msechu amesema pia Ibara ndogo ya 2 ambayo imesisitiza kuwa taarifa ya Spika kujiuzulu inapaswa kupelekwa Bungeni kwa Katibu wa Bunge na si vinginevyo kama ilivyofanyika kwenye mchakato wa kujiuzulu Spika Ndugai.

“Maombi yetu kwa Mahakama ni kutoa tamko kuwa utaratibu wa kujiuzulu Spika Ndugai ulikuwa batili, hivyo kama ulikuwa batili Mahakama itamke kuwa Ndugai bado ni Spika,” amesema.

Wakili Msomi Msechu ametaja jopo la Majaji watatu wataendesha shauri hili ni Jaji John Mgeta, Jaji Dk. Benhajj Shaaban Masoud na Jaji Kisanyo.

Aidha, akizungumzia kwanini shauri hili limefunguliwa na kupangiwa kusikilizwa kwa haraka amesema, hali hiyo imetokana na maombi yao ili kuhakikisha mchakato unaondelea usije kufanyika kabla ya maamuzi hajatolewa.

Amesema mawakili wengi wamejitokeza kushiriki katika shauri hilo kutokana na ukweli kuwa lina maslahi kwa nchi na linatarajiwa kuonesha mwanga mpya wa kusimamia Katiba ya Tanzania.

Uchaguzi wa Spika, unatarajiwa kufanyika Februari mosi mwaka huu, baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa akishika wadhifa huo, Job Ndugai, wiki mbili zilizopita.

2 Responses

  1. Asante ndugu mbatia kutokuwepo mikutano ya hadhara madhara yake ni hayo sasa unapeleka mashtaka mahakami wakati unatambua hautashinda ‘kweli kukosa kazi pia kazi

  2. Huhitaji kuwa mwanasayansi wa roketi kujua barua ilipelekwa kimakosa CCM na nakala kwa Katibu wa Bunge.
    Barua ilitakiwa kupelekwa kwa Katibu wa Bunge na nakala CCM.
    Kupitishwa kwa Dk. Akson, safi sana!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *