MWENYEKITI wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, amesema ili nchi iondokane na upungufu wa sukari, inahitajika uongozi madhubuti katika kusimamia uzalishaji wake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Mwanasiasa huyo ametoa ushauri huo leo Alhamisi, tarehe 2 Novemba 2021, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni kumshukia Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda kutokana na kauli yake aliyoitoa kwamba katu hawezi kutoa vibali vya uagizaji sukari nje ya nchi.
Akizungumza katika kongamano la wafanyabaishara wa Tanzania na Uganda Ikulu jijini Dar es Salaam mapema wiki hii, Rais Samia, alisema nchi itanunua sukari kutoka nchini humo, kama ilivyoombwa na rais wake, Yoweri Museveni.
“Tumeshindwa kujitosheleza kwa sukari bado ngonjera ile ile tunashindana sukari inunuliwe wapi? Tumekosa uongozi,” amesema Mbatia.
Mbatia amesema kuwa, Tanzania ina mazingira mazuri ya kuzalisha bidhaa hiyo, kwani ina ardhi ya kutosha na rasilimali watu, kuliko Uganda ambako nchi inatarajia kununua sukari.
“Tujiulize kwa mfano, Uganda ambao ndiyo wameleta mgororo huu sukari ya Uganda itanunuliwa, rais amesema tutanunua sukari yako Rais wa Uganda, eneo la kijiografia Uganda ni dogo kuliko Tanzania,” amesema Mbatia na kuongeza:
“Malawi wana eneo dogo wanazalisha sukari ya kutosha wauze Tanzania, ukichukua eneo la Uganda na Malawi haifikii eneo la Tanzania, bado halafu tunasema tumeshindwa kuzalisha sukari ya kututosheleza sisi ndani, halafu tunasema kuna uongozi.”
Hivi karibuni Prof. Mkenda alisema hatatoa vibali vya uingizwaji sukari kutoka nje ya Tanzania, kwa ajili ya kuondoa uingizwaji holela wa bidhaa hiyo, ili kulinda soko la wazalishaji wa ndani.
Naye Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliagiza vibali hivyo vizuiwe hadi sukari ya ndani ya nchi itakaponunuliwa kwa ajili ya kulinda wazalishaji wa ndani.
Leave a comment