July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbatia amwomba Rais Samia aweke wazi ripoti BoT

Spread the love

JAMES Mbatia, Mwenyekiti wa chama cha upinzani nchini Tanzania-NCCR-Mageuzi, ameitaka Serikali kuweka hadharani, uchunguzi uliofanyika Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam…(endelea).

Mbatia amesema hayo leo Jumapili, tarehe 6 Juni 2021, alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari, makao makuu ya NCCR-Mageuzi, Ilala jijini Dar es Salaam, kuhusu masuala mbalimbali yanayoendelea nchini.

Amesema, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi maalum Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wa fedha zilizotoka za maendeleo kuanzia Januari hadi Machi, 2021.

“Rais Samia aliagiza CAG na Takukuru wafanye ukaguzi maalum Benki Kuu kuanzia Januari hadi Machi ya fedha zilizotoka za maendeleo. Ni rai yetu ile ripoti iwekwe hadharani kama alivyoagiza Mama Rais ili tujue kulikoni,” amesema Mbatia

Rais Samia Suluhu Hassan

“Aliagiza na ni amri jeshi mkuu, mkuu wa nchi na ripoti hiyo aweke hadharani. Kulikuwa na nini humo ndani. Yalisikika mengi kwenye korido huku. Atuaminishe kuna nini bila kuwa na macho ya makengeza,” amesema Mbatia

Amesema, kutokuwekwa hadharani kwa ripoti hiyo, kutazidisha maswali mengi juu ya nini hasa kimebainika.

Rais Samia alitoa agizo hilo kwa Takukuru na CAG, tarehe 28 Machi 2021, Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma, mara baada ya kumaliza kupokea ripoti za ukaguzi za taasisi hizo.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT)

Alisema, kuna upotevu mkubwa wa fedha zilizokwenda kwenye utekeleaji wa miradi ya maendeleo “tunataka kuziona.”

Tangu agizo hilo lilipotolewa, zimetimia siku 70 ambazo ni sawa na miezi miwili, kukiwa hakuna taarifa zozote kuhusu ripoti hiyo.

error: Content is protected !!