December 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbatia amburuza Selasini kortini, amdai fidia ya Bil. 3

Joseph Selasini (kulia) na James Mbatia

Spread the love

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, amemfungulia kesi Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la chama hicho, Joseph Selasini, katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu, jijini Dar es Salaam, akitaka amlipe fidia ya Sh. 3 bilioni kutokana na madai ya kulichafua jina lake kwa kumtuhumu kuwa mwizi wa mali za chama. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Kesi hiyo imefunguliwa na Mbatia hivi karibuni mahakamani hapo na kupewa namba 184/2022, ambapo imepangwa kutajwa mbele ya Jaji Obadia Bwegoge, tarehe 29 Novemba mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari, leo Alhamisi, tarehe 27 Oktoba 2022, Wakili wa Mbatia, Hudson Mchau, amedai katika kesi hiyo mteja wake amewasilisha maombi matatu, la kwanza mahakama hiyo itamke kuwa tuhuma zilizotolewa na Selasini dhidi ya Mbatia ni za uongo.

Miongoni mwa tuhuma hizo zilizotolewa na Selasini  ni Mbatia kuwa na mambo mabaya ikiwemo wizi wa mali za chama.

Wakili Mchau ametaja ombi lingine ni, imuamuru Selasini kumlipa Mbatia Sh. 3 bilioni, kama fidia ya kumchafua na kumdhalilisha, huku la mwisho likiwa ni kumuamuru Selasini kumuomba radhi hadharani Mbatia.

“Mteja wangu amemfungulia Selasini kesi ya udhalilishaji katika mitandao mbalimbali ya kijamii, akimtuhumu ndugu Mbatia kwa mambo mabaya ikiwemo ya wizi wa mali za chama. Hivyo imepewa namba 184/2022, imepangwa kutajwa tarehe 29 Novemba 2022,” amesema Wakili Mchau.

Wakili Mchau ametoa taarifa hiyo baada ya Mahakama  kuahirisha usikilizwaji wa shauri dogo la madai Na. 459/2022 lililofunguliwa na wajumbe wapya wa Baraza la Wadhamini la NCCR-Mageuzi, wakiongozwa na Beati Mpitabakana na wenzake watano, dhidi ya Mohamed Tibanyendera na wenzake sita.

Shauri hilo limeahirishwa mahakamani hapo na Jaji Edwin Kakolaki, baada ya Wakili wa mjibu maombi, Nashon Nkungu, kuwasilisha ombi la kumpinga Wakili wa mleta maombi, Hassan Ruhwanya, akitaka ajitoe kwa madai ana mgongano wa kimaslahi.

Kwa kuwa ni miongoni mwa washtakiwa katika shauri la msingi Na. 150/2022, lililofunguliwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi-Bara, Angelina Mutahiwa na wenzake, kupinga maamuzi ya kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho, ya kuwasimamisha nyadhifa zao, wakidai kilikuwa batili.

Pia, Wakili Nkungu alimtaka Wakili Ruhwanya kujitoa katika shauri hilo kama wakili, kwani mahakama hiyo katika shauri lingine dogo Na. 384/2022, ilitoa amri ikimtaka ajitoe kama wakili kwa kuwa ni miongoni mwa mshtakiwa katika kesi ya msingi.

Kufuatia ombi hilo, Jaji Kakolaki aliiahirisha kesi hiyo hadi tarehe 7 Desemba 2022, saa 1.15 asubuhi, ambapo Wakili Nkungu atawasilisha hoja zake za kisheria kuhusu ombi lake la kumtaka Wakili Ruhwanya kujitoa.

Katika shauri hilo dogo Na. 459/2022, lililofunguliwa na Mpitabakana na wenzake, wanapinga wajumbe wa zamani wa Baraza la Wadhamini la NCCR-Mageuzi, wakidai sio halali kwa kuwa waliondolewa katika nyadhifa zao na vikao vya chama hicho.

Wanaiomba mahakama hiyo itamke wajumbe wapi ni halali, kati ya wajumbe wapya na wale wajumbe wa zamani walioondolewa pamoja na Mbatia.

Kina Mpitabakana wanaosimamiwa na Wakili Ruhwanya na wengine, walifungua shauri hilo dogo, baada ya Mutahiwa na wenzake kufungua shauri la msingi Na. 150/2022, kupinga uamuzi wa kikao cha halmashauri kuu ya NCCR-Mageuzi, kilichofanyika Mei, 2022 na kuwasimamisha katika uongozi.

Mutahiwa na wenzake wanapinga uamuzi wa kikao hicho kilichosimamiwa na Selasini, wakidai kilikuwa batili kwa kuwa hakikuitishwa kwa mujibu wa katiba ya NCCR-Mageuzi na baadhi ya wajumbe wake walikuwa si halali.

Kwenye shauri hilo la msingi, Mutahiwa na wenzake wanaiomba mahakama itamke kuwa maamuzi ya kikao kile hayakuwa halali hivyo warejeshwe katika nafasi zao.

Mbali na Mutahiwa na Mbatia, wengine waliosimamishwa katika sakata hilo ni wajumbe wa sekretarieti ya uongozi ya NCCR-Mageuzi.

error: Content is protected !!