TUHUMA kwamba siasa za James Mbatia, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, sasa hivi zimepoa, zimemsukuma kusema ‘acheni umbea.’ Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 24 Juni 2020, jijini Dar es Salaam kuhusu tuhuma hizo, amewataka wanachama wake kupuuza maneno aliyoita ya umbea, yanayotoka kwa mahasimu wa chama chake.
“Nawaombeni tuachane na umbea umbea wa mitaani, kuna sifa zinaibuka ibuka, ziko sifa kuu sita za umasikini wa fikra Tanzania, majumngu, fitina, umbea na kusema uongo, unamuona kiongozi yuko kwenye jukwa anasema uongo halafu anataka madaraka,” amesema Mbatia.
Katika siku za karibuni, Mbatia amekuwa akituhumiwa na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwamba anatumika kukiua chama hicho.
Ni baada ya baadhi ya wabunge na madiwani kutoka chama hicho kuhamia NCCR-Mageuzi akiwemo Anthony Komu (Moshi Vijijini) na Joseph Selasini (Rombo).

Mbatia amesema, maneno yanayozushwa juu ya NCCR-Mageuzi (bila kutaja maneno hayo) si kweli na kwamba, kutokana na hekima aliyonayo, ameamua kuyavumilia kwa kukaa kimya.
“NCCR kutokana na utulivu wetu wa ndani tunavumilia sana, wengine wanasema mbona hamjibu, niliongea pale Dodoma, nikasema hekima inasaidia mambo mengi sio lazima ujibu kila kitu, wanaotumia muda kukijele kwenye mitandao, ili kuwanyamazisha wewe fanya mengi mazuri,” amesema Mbatia.
Mbatia amevitaka vyama vya siasa kushindana kwa hoja badala ya kuendekeza chuki na umbea.
“Vyama vya siasa rai yangu, tujitahidi bila kujali kiburi tushindane kwa hoja, na sisi NCCR-Mageuzi tuko tayari kwa mijadala ya vyama vya siasa, tushindane kwa hoja, wewe unakuja utawasilishaje mawazo ya wenzako na sio kudharau wenzako,” amesema Mbatia.
Mbatia mesema, Tanzania itabadilishwa na vitendo na sio maneno.
“Sisi NCCR-Mageuzi mkisema mna maneno zaidi, mkawa na malengo mengi bila matendo ni ndoto za mchana, kuwa na maneno hakuna vitendo ni ndoto za mchana, namna ya kubadili Tanzania ni maneno yetu, dira zetu ziendane na vitendo vyetu,” amesema Mbatia.
Leave a comment