May 15, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mbatia aanza mwaka kwa maneno mazito

James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi

Spread the love

JAMES Mbatia, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi amesema, uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 2020, umelivua nguo Taifa. Anaandika Yusuph Katimba, Dar es Salaam…(endelea).

Katika waraka wake wa Kheri ya Mwaka Mpya 2021, alioutoa kwa wanachama wa chama hicho na Watanzania amesema, Taifa limeingia kwenye aibu kubwa akizungumzia matobo yaliyojitokeza kwenye uchaguzi huo.

“Uchaguzi wa mwaka uliopita umeliacha taifa uchi na kuliaibisha. Mtu anayeachwa uchi anapaswa kujisitiri dhidi ya aibu pindi tu anapogundua yuko uchi,” ameandika kwenye waraka huo.

Kutokana na uchaguzi huo uliolalamikiwa na vyama vya upinzani kwamba uligubikwa na hila, amesema Watanzania walio wengi wamekatishwa tamaa na siasa zinazoendelea ndani ya nchi yao.

 “Uchaguzi huo umeacha makovu mengi mioyoni mwa Watanzania walio wengi. Vivyo hivyo kama Taifa ni muda wetu wa kutafakari kwa kina na kutafuta njia bora ya kujisitiri kutoka kwenye aibu hii ambayo Taifa limeingia na pia kutibu makovu miyoyoni mwetu,” ameandika Mbatia na kuongeza:

“Uchaguzi wa mwaka 2020 ulikuwa uchaguzi usiozingatia matakwa ya ukuaji wa demokrasia na ustawi wake.

“Uchaguzi huo ulijaa ubinafsi na kunufaisha watu wachache katika taifa letu, tofauti kabisa na matarajio ya ustawi wa demokrasia ya nchi ili kukuza maendeleo yetu na maslai ya watu wengi.”

Amesema, vyama na wanasiasa wa upinzani wanapita katika kipindi kigumu huku wengine wakikata tamaa.

“Ninapenda kuwaahidi na kuwahakikishia kwamba, kamwe hatutakata tamaa kabisa,” amesema kiongozi huyo wa NCCR – Mageuzi.

Na kwamba, anajua dhamiri za Watanzania walioshiriki kufikisha Taifa lilipo na kuwataka   waone aibu na kufikiria ustawi wa nchi.

“Tanzania ni nchi yenye heshima yake kimataifa. Kama waasisi wa Taifa letu walivyo heshimu jambo hilo.

“Ni vema kila mmoja kuheshimu heshima ya Tanzania kuliko kuchafua taswira ya nchi yetu kwa mambo yetu ya ndani tunayoweza kuyasimamia wenyewe na mataifa mengine wakaja kujifunza kwetu,” amesema.

Amesema, pamoja na hali ya kisiasa ilivyo, chama hicho kiko imara sana kuliko kipindi chochote cha historia katika maisha ya kisiasa.

“Hakuna hata sehemu moja katika mapambano tutarudi nyuma na kuacha mama yetu Tanzania ateketee kwa namna yoyote.

“Hivyo basi kwa ujumbe wangu huu wale Wana mageuzi wote nchini, tuungane mwaka 2021 kuhakikisha tunatimiza malengo yetu yalivyokusudiwa tangu mfumo wa vyama vingi uanzishwe kwa kipindi kirefu sana kilichopita,” amesema.

Amesema, kama Watanzania wataendekeza majigambo ya walioshinda uchaguzi na walioshindwa, nchi itaendelea kugawika kwa kupandikiza chuki.

“…katika kipindi hiki cha sinto fahamu ya uchaguzi uliopita, kama Taifa la Tanzania kwa wenye busara na wanaoweza kuona ustawi wetu kwa mbali, wanapaswa kukaa pamoja kujadili na kupata muafaka wa kitaifa, hizi tawala  za hapa duniani zinapita tu, na watu wote watapita ila Tanzania itabaki siku zote. Kwa hiyo tulinde nchi yetu ama mboni ya macho yetu na kwa wivu mkubwa.

“Natoa wito kwa viongozi wa vyama vya siasa, Wachungaji, mapadri, maaskofu na mashehe, kusimama kidete upande wa ukweli ili kusema ukweli hatimaye tutaponya taifa letu. Kamwe tusikubali tena kurudishwa katika hali inayo hatarisha amani na umoja wa nchi yetu.”

Amesema, katika vita majeruhi wa kwanza ni ukweli, na kwamba wakati wa vita ukweli huharibiwa vibaya na propaganda.

“Ninawasihi tusikubali propaganda imeze ukweli, tusimamie ukweli daima,” amesema.

error: Content is protected !!