December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbaroni kwa kuiba milioni 60 kisha kujiteka

Jumanne Muliro, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam

Spread the love

 

DEODATUS Thadeo anashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa tuhuma za kujiteka baada ya kudaiwa kuiba kiasi cha Sh. 60 milioni, fedha za kampuni ya China iliyopo Keko jijini humo alikokuwa anafanya kazi kama mhasibu. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 16 Novemba 2022, Kamanda wa Jeshi la Polisi wa kanda hiyo, ACP Jumanne Muliro amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa tarehe 14 Novemba mwaka huu.

Ni baada ya kwenda kuripoti Kituo cha Polisi cha Chang’ombe kwamba ametekwa na majambazi kisha kuporwa fedha hizo kitendo kilichowatia mashaka polisi ambao walianza kufanya uchunguzi wa kina na kubaini taarifa hizo ni za uongo.

“Mtuhumiwa huyu amekamatwa kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kwa mtumishi wa Serikali ambaye ni Afisa wa Polisi, tarehe 14 Novemba 2022 mtuhumiwa alifika Kituo cha Polisi Chang’ombe na kutoa taarifa kwamba amevamiwa na majambazi na kuporwa pesa shilioni 60 milioni ambazo alikuwa amezitoa kwenye benki ya CRDB ya Tazara.

“Alidai alitumwa na kampuni hiyo kwenda kuchukua pesa baada ya kupewa hundi (cheque) tatu na kila hundi ikiwa na thamani ya shilingi milioni 20.

“Aliendelea kudai baada ya kuchukua fedha hizo akiwa mita 100 kutoka benki alikutana na majambazi waliokuwa na Noah nyeusi wakamuingiza ndani ya gari kwa nguvu wakamshambulia wakaenda kumtupa kwenye makutano ya Barabara ya Mbezi na Pugu,” amesema Kamanda Muliro.

Kamanda Muliro amesema “Baada ya kuporwa pesa hiyo alifika Kituo cha Polisi cha Gongo la Mboto kuomba PF3 kwenda kufanya matibabu na baada ya matibabu alienda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Chang’ombe. Makachero wa polisi walichunguza kwa kina taarifa ile na kutilia mashaka,” amesema.

Kamanda Muliro amesema, baada ya Polisi kutilia shaka taarifa za Thadei kutekwa, walimhoji kwa kina na kubaini taarifa hizo zilikuwa za uongo ambapo mtuhumiwa huyo baada ya kubanwa alikiri kuzificha fedha hizo maeneo ya Chanika.

“Baada ya kumhoji kwa kina ilibainika taarifa za kuporwa fedha zilikuwa uongo licha ya kwamba ni kweli alikuwa amechukua pesa milioni 60 ambazo zilikuwa za kampuni ya kichina.

“Alihojiwa kwa kina na baadae alikiri baada ya kuchukua fedha zile alikwenda kuzificha Chanika na baadae alichukua bisibisi akaenda makutano ya barabara na kuanza kujijeruhi na kutengeneza majeraha aliyokwenda nayo Kituo cha Polisi Kidogo kupewa PF3 kwa ajili ya kupata matibabu na baadae kwenda polisi,” amesema Kamanda Muliro.

Kamanda Muliro amesema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakama kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

error: Content is protected !!