August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbarawa awafunga ‘Speed govern’ wafanyakazi

Spread the love

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amewataka watumishi waliopo katika wizara hiyo kupunguza matumizi ya mitandao muda wa kazi, anaandika Happyness Lidwino.

Mbarawa ayasema hayo leo jijini hapa wakati wa kikao cha kwanza kilichojumuisha wafanyakazi hao waliopo wizara hiyo pamoja na viongozi mbalimbali.

Amesema kutokana na kuonekana na uwepo mkubwa wa wafanyakazi wa taasisi mbalimbali ‘kuchati’ muda wa kazi, imemlazimu kama waziri kutoa tamko hilo ili kuhakikisha kuwa watumishi hao wanafanya kazi.

“Suala la kuchati maofisni imekuwa ni ugonjwa ambao unahitaji kuondolewa haraka, na nieleweke kuwa sisemi kuwa tuondoe matumizi ya mitandao lakini kiuhalisia tupunguze kuchati kazini.

“Tumebaini kuwa megabaiti zinazotumika katika taasisi mbalimbali za serikali hazitumiwi katika matumizi halali, asilimia saba pekee ndiyo matumizi halali, asilimia 27 zikitumika kudownload (kupakuwa) vitabu vya shule kwa ajili ya watoto wao.

“Asilimia 20 kudownload video ambazo kimsingi si katika masuala ya kazi, 37 zingine wanatumia katika kutumiana mafaili mengine yasiyo na umuhimu” amesema Mbarawa.

Amesema suala hilo kwa upande wa nchi ya Korea kusini bado wanatafuta mbinu ya kuondoa tatizo hilo mara baada ya kuzidi, sasa na sisi lisituzidi.

Akizungumzia kuhusu mkutano huo uliyowakutanisha wafanyakazi na viongozi wote wa Sekta ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Mbarawa amewataka wafanyakazi kuwajengea Watanzania miundombinu ya kisasa itakayoipeleka Tanzania katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020.

“Tumekutana hapa leo na wafanyakazi wote ili kufahamiana maana tangu wizara hii iunganishwe ni mara yetu ya kwanza kukutana, sasa tunahitaji wafanyakazi kuwa spidi kubwa ya kufanya kazi katika awamu hii, tufanye kazi kweli ili wizara hii iwe mfano wa kuigwa na wizara nyingine.

“Wizara hii ina jumla ya taasisi 29 ambazo zinahitaji kufanya kazi kwa ushirikiano na wizara na kuhakikisha tunafikia malengo mahususi, sasa tufahamu kuwa wizara yetu ndiyo itakayofikisha watanzania kufikia uchumi wa kati kwa kuboreshewa miundombinu, hivyo ni jukumu letu kuwajibika inavyotakiwa ” alisema Profesa Mbarawa.

Akizungumzia mikakati ambayo wanatarajia kuwa nayo kama wizara Profesa huyo alisema wanatarajia kuwa na mfumo wa upatikanaji wa mafaili kwa njia ya kieletroniki (Electronic files system) litakalokuwa kwenye mtandao na kuhakikisha mahitaji yote yanayohitajika kufanyiwa kazi kupitia faili hilo yanatekelezwa kwa wakati.

error: Content is protected !!