August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mbarawa awabana Wachina ‘Airport’ Mwanza

Professa Makame Mbarawa, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Spread the love

PROFESA Makame Mbarawa, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ameiagiza Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group (BCEG) inayofanya ujenzi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza, kuhakikisha inakamilisha kazi ndani ya miezi sita ijayo, anaandika Moses Mseti.

Uwanja huo ambao ulianza upanuzi tangu mwaka 2012, wakati Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela inatengwa kutoka Jiji la Mwanza, mpaka sasa kazi ya upanuzi uliofanyika hauzidi asilimia 20.

Prof. Mbarawa ametoa agizo hilo jana mara baada ya kufanya ukaguzi katika uwanja huo ikiwa ni mwendelezo wa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa hivi karibuni jijini Mwanza la kumtaka mkandarasi kuendelea na ujenzi huo baada ya kusitisha kwa kukosa pesa.

Hata hivyo, Mbarawa amesema, kazi hiyo inaweza kukamilika kwa haraka iwapo wasimamizi watafanya kazi kwa uadilifu na kujituma kutokana na uwanja huo kuchukua muda mrefu bila kukamilika.

“Mkandarasi mshauri unatakiwa kuhakikisha unasimamia kazi kwa uadilifu, kikubwa ni kutopeleka madai yasiyo ya kweli huku serikali ikijipanga kulipa deni lote ili uwanja huo uweze kukamilika ndani ya miezi sita ijayo,” amesema Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa aliyekagua uwanja huo pamoja na Barabara ya Furahisha yenye urefu wa kilomita 5, akitokea mkoani Kagera kuangalia madhara yalitokana na tetemeko la ardhi, amesema kazi kubwa zilibaki katika uwanja huo kwa sasa ni umaliziaji wa jengo (tower) na kuweka zege.

Amesema, licha ya kazi hizo ambazo zinaendelea kufanywa na mkandarasi, nyingine zilizobaki ni kumalizia lami pamoja na kuhamisha mto ambao ulikuwa unakatisha katikati ya barabara ya kurukia ndege.

Amesema, gharama za upanuzi wa uwanja huo kutoka urefu wa kilomita 3.3 hadi kufikia kilomita 3.8 katika njia ya kurudia ndege, jengo la mizigo na tower, unagharimu Sh. 105 bilioni.

“Uwanja huu ukikamilika utasaidia kuimarisha uchumi wa Mkoa wa Mwanza pamoja na usafirishaji kwa mikoa ya jirani pamoja na nchi za Kenya, Rwanda, Burundi na Uganda na kusafirisha mazao ya ziwani,” amesema.

David Matovolwa, Kaimu Meneja wa uwanja huo, amesema kukamilika kwa uwanja huo kutasaidia ndege kubwa kutua pamoja na kuwekwa mafuta na kuruka kule ziendako bila wasiwasi.

Akizungumzia maendeleo ya uwanja huo, mkandarasi mshauri, Salem Munis amesema, watajkitahidi kuhakikisha uwanja huo unakamilika ndani ya kipindi cha miezi sita ijayo kama ilivyoagizwa na Waziri Mbarawa.

Katika hatua nyingine, Prof. Mbarawa alikagua daraja la waenda kwa miguu la Furahisha pamoja na barabara inayojengqwa njia nne kutoka Furahisha hadi Uwanja wa Ndege wa Mwanza na kuridhishwa na maendeleo yake.

error: Content is protected !!