September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mazungumzo KKKT Konde yaahirisha kesi hadi 31 Mei

Askofu Dk Edward Mwaikali akiwa mahakaman akijadiliana na mwanasheria wake Waili Williamu Mashoke katika Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeyaa

Spread the love

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya imeahirisha kesi namba 3/2022 na kesi namba 14/2022 inayohusu mgogoro wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Konde hadi tarehe 31 Mei 2022 ili kupisha mazungumzo baina ya pande mbili zinazopingana. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Uamuzi wa kuahirisha kesi hiyo umetolewa leo Jumatano tarehe 18 Mei 2022 na Jaji James Karayemaha wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya baada ya kupokea maombi ya wakili wa upande wa wadai ambao ni Askofu Edward Mwaikali ombi lililowakilishwa kupitia wakili wake William Mashoke.

Wakili Mashoke aliomba kuhairishwa kusikilizwa kwa shauri hilo ili kupisha mazungumzo baina ya pande mbili zinazopingana ambapo pia mazungumzo hayo yenye nia njema yanahusisha Serikali.

Alisema mgogoro ni nyeti na unahusisha waumini wa Kanisa hilo ambalo lina waumini wengi hivyo anaiomba mahakama iridhie kusogezwa mbele kwani mazungumzo tayari yameanza na hata hivi punde mteja wake alikuwa safarini jijini Dodoma kufanya mazungumzo kutatu mgogo huo.

Kwa upande wa utetezi ambao uliwakilishwa na mawakili Dk. Daniel Palangyo, Emmanuel Clarence na Benjamin Mbembela awali ulipinga kuahirishwa mazungumzo hayo kwani wanatumia gharama kubwa kuiendesha kesi wameiomba mahakama kuendelea na kesi.

Aidha, Wakili Pallangyo kwa niaba ya wenzake alisema wao hawana taarifa zozote za kuwepo mazungumzo nje ya mahakama hata hivyo mleta maombi ya kuahirisha kesi awali ndiye aliomba kuahirishwa kwa kesi.

Hata hivyo, upande wa wajibu maombi ulisema wao ndiyo walioleta notisi ya kupinga maombi haya hivyo aliiomba mahakama iruhusu kuendelea kusikiliza kesi hiyo hata kwa njia ya maandishi baina ya pande mbili.

Wakili anayewatetea wadaiwa namba sita hadi ishirini na tisa ambapo Mkuu wa KKKT Dk Fredrck Shoo ni mshitakiwa wa kwanza, wakili Emmanuel Clarence alisema hana pingamizi juu ya ombi lilowasisiliswa na upande wa mdai ili kupisha mazungumzo.

Hata hivyo, baada ya majadiliano yalidumu kwa takribani dakika 20, Wakili William Pallangyo alikubaliana na upande wa mdai ili mazungumzo yaendelee baina ya pande hizo mbili.

Jaji Karayemaha baada ya kuzisikiliza pande mbili alikubaliana na hoja kusogeza mbele siku ya kusikiliza kesi hiyo ili kupisha mazungumzo kwa lengo la kuleta amani ndani ya kanisa hilo.

Alisema kufanyika kwa mazungumzo baina ya pande zinazopingana kwa maslahi mapana ya Kanisa na Taifa kwa ujumla kwani mgogoro huu una athari kubwa hata kwa madhehebu mengine ya Kikristu.

Jaji Karayemaha alisema mgogoro huu kwa njia ya mazungumzo nje ya mahakama itakuwa suluhisho pekee ya kuumaliza mgogoro huu na kuleta amani kwa waumini wenyewe na jamii inayowazunguka.

“Wito wangu kwa Wakili Pallyango na wenzake kukubali ombi la upande wa pili maana cha msingi ni kuleta amani suluhu ndani kutoka rohoni na ndiyo dhamira ya mahakama pia kuona kesi zinaisha mapema kwa njia ya amani,” alisema Jaji Karayemaha.

Baada kauli hiyo Jaji Karayemaha aliarisha keshi mpaka 31 Mei 2022 kupisha mazungumzo baina ya pande hizo mbili zinazopingana.

Upande wa wa mdai ulifungua kesi ndogo namba 14/2022 kupinga zuio la kuapishwa uongozi mpya uliochaguliwa tarehe 22 Machi 2022 na pia kesi namba 3/2022 ya madai ya gharama za uendeshaji wa kesi.

Msingi wa kesi zote mbili ni kutokana na mgoro uliodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja kutokana na uamuzi wa kuhamisha makao makuu ya Dayoyosisi Konde.

Hata hivyo, mgogoro huo ulichochewa zaidi baada ya kufanyika uchaguzi wa kumuondoa Dk Mwaikali uliofanyika katika Ushirika wa Uyole na kusimamiwa na Askofu Shoo na kumchagua Geoffrey Mwakihaba kuwa Askofu Mteule hali iliyosababisha upande wa Dk Mwaikali kufungua kesi Mahakama Kuu ya kuukata mkutano huo kwamba si halali.

error: Content is protected !!