July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mazrui kampeni meneja wa Maalim Seif Zanzibar

Spread the love

MAALIM Seif Shariff Hamad amemteua Nassor Ahmed Mazrui, msaidizi wake mkuu katika shughuli za siasa ndani ya Chama cha Wananachi (CUF), kuwa kiongozi wa timu ya kampeni ya kutafuta urais wa Zanzibar. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Mazrui ameteuliwa kushika jukumu hilo akisaidiwa na Mansour Yussuf Himid ambaye tangu mwishoni mwa mwaka jana, ndiye mkuu wa mkakati wa kumpatia Maalim Seif ushindi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25.

Akitangaza uteuzi huo leo kwenye mkutano na viongozi waandamizi wa chama hicho na wagombea wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi, Maalim Seif alisema timu ya kampeni itakuwa na matawi mawili, moja likiweko nyumbani kwao kisiwani Pemba.

Kwa upande wa Pemba, Maalim Seif amemteua Hamad Masoud Hamad, mwakilishi wa miaka mingi wa Ole, ambaye anatetea kiti hicho, kuwa msaidizi mkuu wa Mazrui katika timu hiyo.

Katika uchaguzi mkuu wa 2010, timu ya kampeni ya Maalim Seif ilijumuisha watu wapatao 60, sehemu wakiwa Unguja na wengine Pemba mtaa wa Jadida, ambako wahisani walimjengea nyumba ya kisasa ya kuishi.

Mazrui kwa sasa ndiye Naibu Katibu Mkuu wa CUF, na yeye akiwa anagombea tena kiti cha uwakilishi cha jimbo la Mtopepo, lililobuniwa hivi karibuni na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Mazrui ni mwanasiasa aliyejipatia umaarufu wa haraka tangu alipojiunga na CUF mwaka 2010, na katika uchaguzi mkuu mwaka huo, akagombea uwakilishi kiti cha jimbo la Mtoni. Alishinda na katika uundaji wa serikali, aliteuliwa miongoni mwa mawaziri saba kutoka CUF wa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Hamad naye alikuwamo katika Baraza la Mawaziri la kwanza la Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, akishika sekta ya Miundombinu na Mawasiliano.

Alikuja kujiuzulu katika hatua ya uwajibikaji kufuatia janga la kihistoria la kuzama kwa meli ya mv Spice Islander ya mfanyabiashara wa Kizanzibari, kwenye mkondo wa Nungwi, na kusababisha vifo vya watu wengi.

Ajali hiyo iliyoripotiwa kupoteza maisha ya zaidi ya watu 200, ilitokea alfajiri ya siku ya Jumamosi, tarehe 10 Septemba 2011, wakati meli hiyo ikiwa safarini kwenda Pemba, kutoka bandari kuu ya Zanzibar, Malindi. Meli hiyo ilitengenezwa mwaka 1967 nchini Ugiriki kwa jina la Marianna.

error: Content is protected !!