January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mazombi wateketeza Hits FM Radio

Spread the love

MGOGORO wa kisiasa Zanzibar unaendelea. Ungedhani kwa asili yake, hasa kwa kuwa unahusu wanasiasa wanaogombania haki ya kuongoza serikali, uwahusishe wao tu wanasiasa. Sivyo ilivyo. Anaandika Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Wananchi wanaathirika. Kwa hakika wananchi masikini wanaumia na mgogoro huu. Bali hali inavyozidi huku isijulikane ni lini mgogoro utatulizwa, vyombo vya habari navyo vinaguswa.

Majira ya saa 7.15 usiku wa kuamkia leo, kundi la watu waliovalia unifomu za kiaskari, wakiwa wamejifunika nyuso zao kwa soksi, na kushikilia silaha za jadi kama mapanga, mikuki, marungu na mapande ya nondo, walivamia kituo cha redio binafsi na kuteketeza kwa moto studio yake.

Zaidi ya watu 16 waliruka ukuta wa geti na kuingia ndani ya uwanja wa jengo zilipo ofisi za Hits FM Redio, eneo la Mnara wa Mbao, Migombani, mjini Zanzibar na kuharakia mpaka sehemu ya nyuma ya jengo kwenye studio kuu na chumba cha kutengenezea vipindi.

Ndani ya studio, wakati huo vipindi vikiwa vinaendelea, walimkuta Ali Abdalla akitangaza kipindi cha burudani, na kumtaka aondoke kutangaza.

“Hapo nilivowaona tu nikajua kuna jambo kubwa linatokea, sikubishana nao, kwa kuhofia wangeniumiza, niliacha kutangaza na kuondoka kwenye kiti cha kutangazia,” anasema Ali, mtangazaji kijana aliyejiunga na Hits FM Redio miezi minne iliyopita.

Ali anasema aliwekwa chini ya ulinzi, akapigwa mapanga mara kadhaa kwa kutumia upande wa ubapa; akaamriwa kulala chini, akafungwa mikono kwa nyuma, askari mmoja akamchomeka matambara kinywani.

Akaongozwa nje ya studio huku akiwa amefungwa kitambaa usoni asione kinachotendeka. Akawa anasikia kelele za wavamizi wakielekezana cha kufanya.

“Nasikia vishindo huku na kule, nikaanza kusikia vitu vinavunjwa hivi. Vishindo vikubwa vinaendelea, nikawa nasikia sauti za watu kama wanakimbia. Baada ya muda nikasikia kimya kizito, nikahisi labda wameondoka. Nikaendelea kidogo kutulia, nilipojiridhisha kuwa wameshaondoka, nikajiinua mpaka kufanikiwa kujizongoa. Nikajizoa na kutoka nje ya jengo.”

Wavamizi walichoma moto chumba cha studio na cha kutengenezea vipindi, baada ya kuvimwagia petroli. Studio iliharibika kabisa, hakuna kilichonusurika na moto, lakini chumba cha kutengenezea vipindi hakikushika moto kutokana na kikwazo cha baridi kali iliyokuwa ndani.

Wavamizi waliruka ukuta baada ya kushindwa kufungua geti. Hakuna mlinzi aliyeibuka walipokuwa wanatoa amri ya kufunguliwa mlango. Walinzi walikuwepo wawili kutoka kampuni ya Island Security Group, lakini walijificha waliposikia kundi la watu wanavamia. Walijibanza pembeni mwa eneo la uwanja wa jengo. Walipoona wavamizi wamepita na kufukuzia nyuma ya jengo kwenye studio, wakaruka ukuta pembeni na kutoka nje. Walikwenda nyumba ya jirani kuomba msaada wa askari wa JKU wanaolinda nyumba ya serikali anayoishi Spika wa Baraza la Wawakilishi. Hawakusaidiwa.

Wakatoka nje barabarani na kwenda kwenye geti la nyumba ya Rais mstaafu wa pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi ambako walinzi ni askari polisi wa FFU. Wakajieleza na kupata msaada wa kupigiwa simu kituo cha polisi ambako askari kadhaa walikuja kutoa msaada wakati wavamizi walishakimbia.

“Sijui hasa kwa nini wametuvamia na kuchoma kituo chetu. Hatuan chuki na mtu yeyote zaidi ya kufanya kazi zetu kwa uadilifu. Hatuandami mtu yeyote wala kikundi chochote, tunajiona tunaofanya kazi wanayoitaka wasikilizaji wetu. Ni bahati mbaya tumehujumiwa namna hii,” ndivyo alivyosema mtangazaji Abdalla alipozungumza na mwandishi wa habari hizi.

Mkuu wa Utangazaji wa Hits FM, Juma Ayoub amesema, “hatuna bifu na mtu yeyote, tulichotendewa ni uonevu tu na ni jambo la kusikitisha sana. Itachukua muda mpaka turudi hewani.”

Moza Salum, Mhariri wa Hits FM, amesema “inasikitisha unapoona migogoro ya wanasiasa inasababisha vyombo vya habari kuhujumiwa. Wamehujumu wasiohusika na mambo yao. Hii ni hatari kwa kweli.”

Waandishi na wafanyakazi wa kituo hicho wameeleza kusikitishwa na kilichotokea. Mmoja alisema, “Waliokuja walijiandaa kwa sababu asiyejua tulivyo hapa kazini hawezi kujua zilipo studio zetu. Labda wametumwa kuhujumu chombo cha habari hiki.”

Mmiliki wa kituo hicho, Mohamed bin Jabir amesema wafanyakazi wapatao 22 wakiwemo waandishi na watangazaji na wahandisi wataathirika kwa kukosa cha kufanya mpaka matangazo yatakaporudi.

Hakujua kwa uhakika itachukua muda mrefu kiasi gani. Anasikitika uharibifu huo umefanywa siku chache baada ya kufunga vifaa vipya vya studio katika mpango wa kuongeza ufanisi wa shughuli za utangazaji.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, ACP Mkadam Khamis Mkadam alifika kukagua uharibifu uliofanyika, akifuatana na kundi la wasaidizi wake. Maofisa wa serikali kutoka taasisi mbalimbali, ikiwemo Tume ya Utangazaji Zanzibar – Zanzibar Broadcasting Commission (ZBC) – walifika kujionea uharibifu.

Oktoba 27 mwaka huu, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Tume hiyo, ilikifungia kituo cha radio cha Swahiba (Swahiba FM Radio) kwa madai ya kutangaza matangazo yanayokwenda kinyume cha sheria.

Kituo hicho kilirusha baada ya kurekodi taarifa aliyoitoa saa kadhaa kabla, Maalim Seif Shariff Hamad kuhusu matokeo ya uchaguzi akisema alikuwa anaelekea kushinda. Alitangaza hivyo mbele ya waandishi wa habari, wakiwemo wa vituo vya redio na televisheni waliorusha moja kwa moja matangazo wakati wa mkutano wa waandishi.

Kituo cha Swahiba FM kinaendeshwa na kampuni inayomilikiwa na Chama cha Wananchi (CUF). Hata CCM wanaendesha kituo kiitwacho Bahari FM ambacho kinaendelea na matangazo yake, huku kikisikika kutoa taarifa za uchochezi. Siku chache baada ya Swahiba FM kufungiwa, watu waliokataa kujitambulisha ni nani na wanatoka wapi, walifika usiku na kuhoji walinzi na wafanyakazi waliokuwepo. Waliondoka bila ya kuleta madhara.

Juni 29, askari waliofunika nyuso zao wakiwa na gari ya moja ya vikosi vya ulinzi vya SMZ walivamia kituo cha redio cha Coconut FM kinachomilikiwa na kampuni ya Clouds Entertainment ya jijini Dar es Salaam na kutishia usalama wa wafanyakazi waliowakuta nje ya jingo eneo la Mnara wa Mbao, Migombani.

Uvamizi huo unaofahamika hapa kufanywa mchana na askari wa moja ya vikosi vya SMZ, unatajwa kuwa ulifanywa kwa lengo la kumshambulia mwandishi Ali Mohammed ambaye siku chache kabla, alirusha kipindi maalum cha kujadili mwenendo wa vitisho uliokuwepo wakati Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ikiendelea na kazi ya kuandikisha wapigakura.

Mwandishi huyo aliondoshwa kazini kwa kile wengi walichokieleza kuwa “ni matokeo ya vitisho vya uongozi wa serikali dhidi ya mmiliki wa kituo.” Inasemekana alipewa sharti kumtimua au akubali kituo kifungwe.

Askari wa vikosi vya SMZ waliopewa jina jipya la Mazombi, baada ya Janjaweed lililozoeleka muda mrefu, wanalaumiwa kwa kuendesha vitendo vya mashambulizi dhidi ya raia hasa kwenye maeneo wanayohisi yanakaliwa zaidi na wafuasi wa upinzani.

Hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na matukio hayo ambayo Kamanda wa Polisi Mkadam aliahidi uchunguzi unafanywa wa kujua waliohusika. Hata hivyo, polisi wamekuwa wakishuhudiwa kuandamana na askari hao wa vikosi vya SMZ kwa mtindo wa kuwapa hifadhi wakati wanapofanya mashambulizi mitaani.

error: Content is protected !!