Friday , 29 March 2024
Home Habari Mchanganyiko Mazombi wamchoma mchuuzi
Habari Mchanganyiko

Mazombi wamchoma mchuuzi

Spread the love

ASKARI wa kikosi cha Valantia (KVZ) wanaojulikana kwa umaarufu kama “mazombi” wamemjeruhi mchuuzi wa bidhaa za mkononi kwa kumpiga, kumchoma moto na kumtelekeza kambini kwao bila ya kumpatia matibabu, anaandika Jabir Idrissa.

Taarifa zilizofikia MwanaHALISI Online, zimesema kwamba mazombi hao waliokuwa wameshuka kwenye lori aina ya Fuso, eneo la Mchangani, katikati ya mji wa Zanzibar, walimkamata Abdulla Ahmed Juma, mwenye umri wa miaka 29 na kumshambulia kwa kumchangia hadi kumchoma moto.

Kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo, lililotokea mwanzoni mwa wiki hii, askari waliokuwa kundi walimkamata Abdulla akiwa na bidhaa mbalimbali mkononi akitembeza baada ya kukosa eneo la kufanyia biashara kutokana na alikokuwa kuvunjwa na serikali eneo la makontena Michenzani mjini Zanzibar.

Baada ya kumkamata, baadhi ya askari walianza kumshambulia kwa kumpiga, wengine wakampekua na hatimaye kuchukua bidhaa zake zote na kumrusha kwenye gari huku wakiwa wamemfunga kitambaa, kwa lengo la kumzuia kuona anakopelekwa.

Lakini kaka yake aitwaye Nadir Ahmed, akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu leo, amesema ndugu yake aliporwa bidhaa zake pamoja na fedha taslimu kiasi cha Sh. 800,000 na kushambuliwa kwa askari hao kuchangiana.

Nadir akieleza kulingana na maelezo ya mashuhuda, amesema ndugu yake baada ya kushambuliwa na kunyang’anywa kila alichokuwa nacho, ikiwemo pia simu ya mkononi aina ya G01, alichomwa moto mikononi na miguuni.

“Abdulla alipelekwa mpaka kwenye kambi ya Valantia pale Gymkhana. Akawekwa bila ya kupatiwa matibabu. Hawakumpa huduma yoyote ya tiba ilhali wamemshambulia watakavyo na kumchoma moto. Labda walikusudia kumfanyia vibaya zaidi ya walivyofanya,” alisema.

Alisema baada ya kupata taarifa kutoka kwa mtu ambaye hawezi kumtaja ambaye alimtambua ndani ya kambi, kwa kuwa yeye hakuwepo, jamaa zao walifuatilia na walipopata uthibitisho, walifanya mawasiliano na viongozi wa kikosi cha Valantia ili kuomba wakabidhiwe ndugu yao.

Kwa mujibu wa maelezo yake, walikabidhiwa ndugu yao baada ya kutoa Sh. 100,000. Walimpeleka kutibiwa kituo cha afya na baadaye kufanikiwa kupata fomu ya polisi ya kupata matibabu (PF3) kwenye kituo cha Polisi cha Muembemadema, yalipo makao makuu ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi.

Nadir alisema wametakiwa kuirudisha fomu hiyo kituoni baada ya Abdulla kupatiwa matibabu.

Tukio hilo ni mfululizo wa matukio ya uvamizi wa raia unaofanywa na makundi ya askari vijana ndani ya vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Baadhi ya wakati makundi hayo huvamia na kushambulia wananchi hasa kwenye maeneo yanayokaliwa na wafuasi wa upinzani, huku wakisindikizwa na askari wa Jeshi la Polisi. Ni matukio ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara lakini viongozi wa serikali wamekuwa wakikanusha.

Machi mwaka huu, mazombi walivamia baraza ya Taveta, inayodhaminiwa na mwakilishi wa Pangawe, Suleiman Mchukucha, na kuwajeruhi watu kadhaa akiwemo mzee Abdalla Pavu mwenye umri wa miaka ya 72.

Hivi karibuni, ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni Yussuf ambaye pia ni mbunge wa Kikwajuni mjini Zanzibar, alisema hakuna matukio ya aina hiyo kwa kuwa jeshi la polisi halina taarifa nayo.

Alisema badala yake anachojua kuna wahalifu ambao hulalamika wanapodhibitiwa na polisi.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Mtandao watetezi wa haki za mazingira Tanzania waundwa

Spread the loveMTANDAO wa watetezi wa haki za mazingira nchini Tanzania, umeundwa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga kuongoza usambazaji wa mitungi ya gesi 10,000 ya Taifa Gas

Spread the loveNaibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameahidi kuongoza kwa ufanisi...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wafanyabiashara, wawekezaji China waridhia kuwekeza bil. 800 katika sekta 5 nchini

Spread the loveUJUMBE wa wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa kutoka Jimbo la Changzhou...

Habari Mchanganyiko

Bil. 4.42 kumaliza uhaba maji kata 2 Musoma Vijijini

Spread the loveWANANCHI wa kata za Busambara na Kiriba, Jimbo la Musoma...

error: Content is protected !!