May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mazishi ya Magufuli: Dk. Shein akumbusha machungu uchaguzi mkuu 2015

Aliyekuwa rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein

Spread the love

 

RAIS Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amesema, aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Pombe Magufuli (61), alikuwa mshauri wake katika mgogoro wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015. Anaripoti Mwandishi Wetu, Chato…(endelea).

Dk. Shein amesema hayo leo Ijumaa tarehe 26 Machi 2021, mara baada ya kumalizika kwa misa takatibu ya mazishi ya Dk. Magufuli, iliyofanyika uwanja wa mpira wa miguu wa Magufuli, wilayani Chato Mkoa wa Geita.

Dk. Magufuli amefariki dunia tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam, alikokuwa anapatiwa matibabu ya ugonjwa wa mfumo wa umeme wa moyo. Mwili wake unazikwa leo nyumbani kwao Chato.

“Dk. Magufuli nilikuwa namuamini sana, katika muungano alinitia moyo sana, hasa baada ya matukio yaliyotokea baada ya uchaguzi mkuu. Kaniambia bwana wee chapa kazi watu wataona wenywe,” amesema Dk. Shein.

Rais huyo mstaafu wa Zanzibar amesema, katika enzi za uhai wake, Dk. Magufuli hakuwahi kumshauri vibaya.

“Nimejitahidi kufanya hivyo kufuata mfano wake, kufuata ushauri wake na hakunishauri vibaya hata siku moja,” amesema Dk. Shein.

Katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, kuliibuka mgogoro baina ya Dk. Shein na aliyekuwa mpinzani wake wa karibu katika kinyang’anyiro cha kiti cha urais wa Zanzibar, Hayati Maalim Seif Shariff Hamad, baada ya matokeo ya uchaguzi huo kufutwa.

Katika uchaguzi huo, Dk. Shein aligombea kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku Maalim Seif aliyefariki dunia tarehe 17 Februari 2021, alikuwa mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF).

Uchaguzi huo ulifutwa na Jecha Salim Jecha, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kwa maelezo kwamba mchakato wake ulikuwa na dosari. Kisha akaitisha uchaguzi wa marudio, ambao Maalim Seif alisusa kushiriki.

Baada ya uchaguzi huo wa marudi kuitishwa, Dk. Shein alishinda uchaguzi huo, na kuunda Serikali huku CUF wakisusia kushiriki uchaguzi huo.

error: Content is protected !!