December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mazingira ‘tata’ yagubika uchaguzi Burundi

Spread the love

TAIFA la Burundi kesho Jumatano tarehe 20 Mei, 2020, linaingia kwenye uchaguzi ‘peke yake.’ Hakuna waangalizi wa kimataifa wala Umoja wa Afrika. Utawala wa nchi hiyo umegomea mwangalizi yoyote, umepanga kujichunguza wenyewe. Inaripoti mitandao ya kimataifa…(endelea).

Rais Pierre Nkurunziza aliyedumu madarakani kwa miaka 15, sasa anajiandaa kumpisha rais mpya.

Ikiwa hivyo, nchi hiyo itajenga historia mpya ya kukabidhi madaraka kwa njia ya amani tangu ilipopata Uhuru 1962.

Amani inayozungumzwa ni ile ya rais kutoka madarakani na kumpisha mwenzake, si amani inayotokana na Warundi kuamua nani awaongoze.

Tayari mazingira ndani ya Burundi yanaakisi kwamba, uamuzi wa nani arithi kiti cha Nkurunziza umeishafanyika.

Malalamiko kutoka vyama vya upinzani, wachambuzi wa kisiasa na mataifa mengine yanamuweka Nkurunziza kwenye lawama iwapo machafuko yatatokea.

Wakati Burundi ikiwa katikati ya tishio kubwa la mlipuko wa ugonjwa wa corona, baada ya uchaguzi kutokana na mikusanyiko isiyojali tahadhari, wagombea wawili – Evariste Ndayishimiye (CNDD-FDD) na Agathon Rwasa (CNL) – ndaio wanaopewa nafasi kubwa.

Kwenye uchaguzi huo, wagombea saba wanasaka nafasi ya kutumikia taifa hilo ngazi ya rais.

Chama tawala anachotoka Rais Nkurunziza (CNDD-FDD), bendera yake inapeperushwa na Jenerali mstaafu Evariste Ndayishimiye (52).

Ndayishimiye ambaye aliwahi kuwa kamanda wa waasi nchini humo, ameshika madaraka kadhaa ikiwa ni pamoja na Waziri wa Ulinzi, kuongoza Idara ya Masuala ya Kijeshi lakini pia Katibu Mkuu wa chama hicho.

Mpinzani wake mkubwa Rwasa (56), ambaye naye aliwahi kuongoza kundi la waasi wa Kihutu la FNL, kwa muda mrefu amekuwa mpinzani wa Nkurunziza.

Mara kadhaa amekuwa akipinga uamuzi uliokuwa ukifanywa na Nkurunziza, pia amesusia uchaguzi mkuu wa 2010 na 2015 kwa madai ya kutokuwa huru na haki.

Madai hao, yamejitokeza tena kuelekea uchaguzi mkuu kesho, huku kukiwa na vitendo vya vurugu, unyanyasaji dhidi ya vyama pinzani.

“Vurugu na ukandamizaji vimekuwa ishara kuu ya siasa nchini Burundi tangu mwaka 2015, wakati huu tunakaribia uchaguzi, kuna maradhi ya corona, vyote hivyo vinazidisha hofu,” amesema Lewis Mudge, Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Hakiza Binadamu Afrika ya Kati na kuongeza:

“Hakuna shaka kuwa, uchaguzi huu utafuatana na dhuluma zaidi, kwani maofisa wa Burundi na wanachama wa Imbonerakure (chama tawala), wanatumia vurugu bila chochote kushinikiza chama tawala kibaki madarakani kwa namna yoyote ile.”

Rais Pierre Nkurunziza

Zaidi ya watu milioni tano, wanatarajiwa kupiga kura. Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 12 asubuhi na kufungwa saa 10 jioni.

Matokeo ya majimbo yanatarajiwa kupatikana kuanzia tarehe 26 Mei na matokeo ya mwisho yanatarajiwa kuwa tarehe 4 Juni 2020.

Prof. Karuti Kanyinga kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi ameiambia Aljazeera “kwa Burundi, uchaguzi unafanyika ilimradi tu kujiwekea hadhi.”

“Jeshi na chama tawala haviwezi kuruhusu mtu mwingine yeyote atangazwe kuwa mshindi, upinzani watagomea matokeo na yanaweza kujitokeza yale ya 2015.”

Amesema, kutokana na tatizo la virusi vya corona duniani, endapo machafuko yatatokea, haliya Burundi itakuwa mbaya zaidi kwa kuwa mataifa hayo yapo ‘bize’ kupambana na corona.

Wiki iliyopita, serikali ya nchi hiyo ilifukuza maofisa wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa madai ya kuingilia kwenye mapambano yao dhidi ya virusi vya corona.Taifa hilo lililo na watu milioni 11, tayari limetangaza maambukizi ya virusi vya corona 42 na kifo kimoja.

Burundi inashika namba 160 kati ya nchi 180 kwa uhuru wa vyombo vya habari kwamaripota wasio na mipaka. Hata hivyo, uchaguzi huo utafanyika bila kuwepo kwa waangalizi wa nje.

Abdullahi Halakhe Boru, mchambuzi wa masuala ya siasa amesema, kutokana na mazingira yalivyo, chama cha serikali ‘lazima kishinde.’

“Burundi imebaki yenyewe, Umoja wa Afrika haupo, wachunguzi wa kimataifa hawapo, watashinda tu,” Halakhe Boru ameiambia Al Jazeera.

Wagombea saba wanaingia kwenye mtanange wa kumrithi Nkurunziza. Rais huyo amekaa pembeni kutoka na shinikizo kutoka ndani na nje ya taifa hilo.

Uamuzi wa Nkurunziza kugombea urais mwaka 2015 (ikiwa ni kipindi cha tatu) 2015, kulizua sintofahamu na kwamba kilikwenda kinyume na Katiba ya taifa hilo.

Baada ya jaribio la mapinduzi la Mei 2015 kushindikana, maelfu ya wananchi wa taifa hilo walikimbilia mataifa jirani wakihofia machafuko.

Burundi haijawa salama, utawala wa Nkurunziza kwa muda mrefu umetuama katika tuhuma za kuangamiza wapinzani wake.

error: Content is protected !!