January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mazingira bado tete-Waziri

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge

Spread the love

WAKATI Tanzania inajiandaa kuadhimisha siku ya mazingira duniani, bado changamoto zinazoathiri mazingira zimeendelea kuongezeka. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Dk. Binilith Mahenge, Waziri wa Nchi- Ofsi ya Makamu wa Rais (Mazingira), amesema maadhimisho hayo yatafanyika 5 Juni mwaka huu.

Katika ngazi ya kitaifa maadhimisho hayo yatafanyika mkoani Tanga na kidunia yatafanyika jijini Milan nchini Italia ambapo ujumbe wa mwaka huu ni; “Ndoto bilioni saba. Dunia moja. Tumia rasilimali kwa uangalifu”.

“Ujumbe huu unahimiza jamiii kutambua umuhimu wa utumiaji endelevu wa rasilimali tulizonazo kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho kwa kuzingatia ongezeko la watu duniani lililofikia watu bilioni saba kwa sasa,”amesema.

Kwa mujibu wa Dk. Mahenge, mkoa wa Tanga umechaguliwa kutokana na changamoto za mazingira zinazoukabili ikiwa ni pamoja na uvuvi usio endelevu, kupotea kwa bioanuai kutokana na uharibifu wa mazingira ya ardhi na vyanzo vya maji, kilimo kisicho endelevu, uchafuzi wa mazingira na uharibifu wa miundombinu.

Changamoto nyingine ni mmomonyoko wa fukwe, kuzama kwa baadhi ya visiwa kama vile Maziwe kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

“Kulingana na ripoti ya mazingira nchini ya mwaka 2014, hali inaonesha takribani asilimia 61 ya ardhi ya Tanzania imeharibika, hususani katika maeneo kame ya mikoa ya Dodoma, Shinyanga, Singida, Simiyu, Geita na Kilimanjaro,” ameeleza Mahenge.

Aidha, kasi ya ukataji miti na uharibfu wa misitu inaongezeka, ambapo hekta 400, 000 za misitu hupotea kila mwaka.

“Kumekuwa na matukio ya vifo vya wanyama kutokana na uhaba wa maji na malisho, uchomaji moto ovyo ambapo kati ya mwaka 2000 na 2011 kumekuwepo na matukio 1,123,000 ya vifo yaliyoripotiwa mikoa ya Rukwa, Kigoma, Tabora, Mbeya, Ruvuma, Lindi na Morogoro,” amefafanua Mahenge.

Ameongeza kuwa zaidi ya asilimia 90 ya kaya mijini hutumia vyoo vya shimo, ambavyo huchangia uchafuzi wa vyanzo vya maji, ubora na kiasi cha mtiririko wa maji kwenye mifumo ikolojia vimepungua.

Katika kuondokana na changamoto hizo serikali na jamii imetakiwa kuhakikisha inalinda na kutunza mazingira hasa kwa kuzingatia utekelezaji wa sera, sheria, kanuni, mipango, miongozo ya kitaifa na kutoa elimu ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira.

error: Content is protected !!