August 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maxence Melo amaliza siku 7 ‘kifungoni’

Maxence Melo, Mwanzilishi wa Mtandao wa Jamiiforum

Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemuachia kwa dhamana Maxence Melo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Jamii media inayomiliki mtandao wa Jamii Forums baada ya kushikiliwa kwa takribani siku saba, anaandika Faki Sosi.

Melo alishikiliwa kwa siku nne kabla ya kufikishwa mahakamani 16 Desemba mwaka huu, alipopandishwa kizimbani na kusomewa kesi tatu tofauti chini ya mahakimu watatu tofauti jambo lililosababisha akose dhamana katika kesi yake ya tatu mara baada ya mdhamini kuchelewa kufika.

Mapema leo Mbele ya Hakimu Godfrey Mwambapa ‘bosi’ huyo wa Jamii Forums amekamilisha masharti ya dhamana baada ya kudhaminiwa na wadhamini wawili waliosaini hati ya Sh. 5 milioni kila mmoja.

Melo ameshitakiwa kwa kesi tatu ambazo alisomewa mbele ya mahakimu watatu tofauti.

Kesi Na. 456 yenye shtaka moja alilosomewa mbele ya Thomas Simba, Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo ambapo alidaiwa kuzuia taarifa za upelelezi wa Jeshi la Polisi kati ya tarehe Mosi Aprili na tarehe 13 Desemba, 2016 huko Mikocheni, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Kesi nyingine ya pili ni Na. 457 mbele ya Hakimu Godfrey Mwambapa, ambapo Melo anadaiwa kati ya tarehe 10 Mei na tarehe 13 Desemba 2016 akiwa Mikocheni Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam alikwamisha kazi ya Jeshi la Polisi kwa kutotoa taarifa za kiupelelezi kwa jeshi la polisi.

Kesi ya tatu kwa Melo ni Na. 458 iliyosomwa mbele ya Hakimu Victoria Nongwa, Melo anadaiwa kumiliki mtandao wa Jamii Forums bila ya kusajiliwa hapa nchini Tanzania na kuwepewa msimbo wa (.co.tz), ikiwa ni kinyume cha sheria.

Kesi hiyo itatajwa tena tarehe 29 Desemba, mwaka huu.

error: Content is protected !!