April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mawakili wajifungia kusaka mwarobaini wa kesi za utakatishaji fedha

Spread the love

BAADHI ya mawakili nchini Tanzania, wamefanya semina ya mafunzo ya kuepuka kujihusisha na makosa ya utakatishaji fedha na uhujumu uchumi, pindi wanapotekeleza majukumu yao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Semina hiyo iliyofanyika jana tarehe 24 Januari 2020 jijini Dar es Salaam, imeandaliwa na Kampuni ya Mawakili ya LawAge Consult, kwa kushirikiana na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC).

Akizungumza kuhusu semina hiyo, Wakili Steven Msechu, amesema wamechukua hatua hiyo baada ya kuona ongezeko la mawakili wengi kuunganishwa katika kesi za wateja wao, wanaotuhumiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi na utakatishaji.

“Hii ni semina yetu ya kwanza inayohusu namna ya kuepuka makosa ya utakatishaji fedha kwa mawakili. Kwa miaka kama mitatu hivi wanasheria wengi wamekuwa wakijikuta wanaunganishwa kwenye makosa ya utakatishaji fedha.

Makosa ambayo unakuta ni mteja wake labda ametuhumiwa kutenda lakini na yeye ameunganishwa kwenye kesi.  Kwa sababu labda kuna vitu fulani alitakiwa avifanye wakati anahudumia, wateja lakini hakuvifanya, “ amesema Wakili Msechu.

Wakili Msechu ameeleza kuwa, mawakili wanahofu juu ya makosa hayo, kwa kuwa, hadi sasa kuna mawakili 10 wako mahabusu wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha.

“Kwa hiyo kwa namna moja au nyingine, wakili anajikuta anamsaidia mteja wake kutenda kosa la utakatishaji fedha ama kwa kujua au kwa kutokujua. Tukaona wenzetu mawakili zaidi ya 10 wako ndani wanakabiliwa na hizi tuhuma za kutakatisha fedha, kitu ambacho mawakili tunalalamika na kuhofia,” amesema Wakili Msechu .

Wakili Msechu amesema kwa sasa, baadhi ya mawakili wameanza kukwepa kushughulika na kesi zenye viashiria vya utakatishaji fedha, hasa kesi zinazohusu masuala ya ardhi.

“ Wakati mwingine  mawakili wanaamua kutozifanya kwa mfano,  kazi za masuala ya ardhi ni kazi zinazopitisha fedha nyingi. Baadhi ya  wanasheria wameamua kazi hizi hatuzifanyi. Zimepelekea mawakili wengi kuambiwa wanatakisha fedha,” amesisitiza Wakili Msechu.

Aidha, Msechu ametoa wito kwa wanasheria nchini kutoa taarifa kwa mamlaka husika, pindi wanapohisi wateja wao wana fedha nyingi ambazo vyanzo vyake vina mashaka, au pindi wanapokutana na miamala ya fedha yenye mashaka.

“Sisi amwkaili tunatakiwa tukikutana na muamala kutoka wa wateja wetu ambao unatutia shaka, vyanzo vyake vya mapato havijulikani. Tunatakiwa kutoa taarifa kwa vyombo vinavyosimamia usalama wa fedha,” amesema.

Maudhui ya semina hiyo ilikuwa ni kuangalia njia rahisi kwa mawakili kuhudumia wateja wao, pasina kujiingiza katika makosa ya utakatishaji fedha na uhujumu uchumi, kugundua na kutoa taarifa kwa mamlaka za kuchunguza fedha.

Pamoja na kujadili changamoto za kiutendaji wanazokutana nazo mawakili wakati wanashughulikia kesi hizo.

error: Content is protected !!