Tuesday , 23 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mawakili waandamizi 15 wa Serikali wahenya kumzuia Lissu
Habari za SiasaTangulizi

Mawakili waandamizi 15 wa Serikali wahenya kumzuia Lissu

Alute Mungwai
Spread the love

SAA karibu 12 zilizoandamana na vipindi viwili vya mapumziko vilivyochukua jumla ya dakika kumi hivi, zilimtosha Jaji Sillius Matupa wa Mahakama Kuu kutamka kuwa anafunga usikilizaji wa shauri na kutaka wahusika wakutane saa 8 mchana Jumatatu ijayo kusikiliza uamuzi. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Ni uamuzi unaohusu ombi la mwanasiasa machachari nchini, Tundu Antipas Lissu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), anayepigania ubunge wa Singida Mashariki ambao anadai amevuliwa kinyemela mwishoni mwa Juni mwaka huu.

Lissu anaendelea na matibabu nchini Ubelgiji kutokana na kushambuliwa kwa mfululizo wa risasi 38, miaka miwili iliyopita akiwa anatoka kuhudhuria kikao cha bunge mjini Dodoma. Kwa sababu hiyo, ombi lake hilo limewasilishwa kwa njia ya uwakilishi unaofanywa na kaka yake, Alute Mughwai ambaye pia ni mwanasheria na wakili.

Katika shauri hilo linalovutia mamilioni ya Watanzania kote nchini, Lissu anaomba kibali cha Mahakama Kuu ili afungue kesi ya kutaka uamuzi huo wa kuvuliwa ubunge, utenguliwe na arejeshwe kutumikia wananchi.

Ombi lake linamhusu Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Spika Ndugai ndiye alitoa tangazo rasmi la uamuzi wa kumvua Lissu ubunge mnamo tarehe 28 Juni 2019.

Wakati kikao cha mahakama kilianza saa 4 asubuhi jana Ijumaa, ndani ya ukumbi uliokuwa umefurika wasikilizaji, wakiwemo wale waliotoka jimboni kwao mkoani Singida, Jaji Matupa alitia tamati kunako saa 3 usiku akisema “tukutane hapa saa 8 mchana Jumatatu ambapo nitatoa uamuzi wa ombi.”

Jaji Matupa aliweka nukta, baada ya kuwa amemaliza kusikiliza maelezo ya muwasilisha ombi na mjibu (wajibu) ombi hilo ambao kwa pamoja na waliwakilishwa na jopo la wanasheria 15 chini ya uongozi wa Wakili Mkuu wa Serikali, Dk. Clement Mashamba.

Upande wa muwasilisha ombi ulichukua nafasi ya kutoa maelezo ya umuhimu wa kutolewa idhini ya mahakama kuu ya kufungua kesi, kwa wakili Peter Kibatala kujenga nguvu ya ombi linalolalia hoja kuwa si kweli kwamba Spika wa Bunge hajui kutokuwepo kwa Lissu bungeni.

Hoja kuu ya pili ya Lissu kwa mujibu wa hati ya kiapo iliyoko mahakamani, ni ya kupinga sababu ya kuvuliwa ubunge wake ya kwamba “hakujaza fomu ya maelezo ya mali zake kwa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma.”

Ndani ya ombi la Lissu, akiwakilishwa na kaka yake, Mughwai, anaomba pamoja na mambo mengine, mahakama itoe amri ya kuzuiwa kitendo cha kuapishwa kwa Miraji Mtaturu, mbunge mteule aliyetangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi baada ya tume hiyo kuendesha utaratibu wa kuziba nafasi aliyoiacha Lissu kufuatia uamuzi wa kuvuliwa ubunge.

Mtaturu ambaye ni mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alitangazwa mshindi bila ya kupigiwa kura kwa kuwa ni pekee aliyerudisha fomu ya kuomba kugombea; waombaji wengine 12 wakitajwa kuwa hawakurudisha fomu zao.

Serikali kupitia wanasheria wake, ilijielekeza kwenye kupinga kusikilizwa kwa shauri hilo kwa ikielezwa kuwa ombi halikukidhi vigezo vya kisheria kwa hoja kuwa maombi hayakuambatanishwa na uamuzi uliowahi kutolewa na mahakama yoyote.

“Maombi haya hayajakidhi vigezo kisheria kwa sababu hakuna uamuzi wowote wa kimahakama ulioambatanishwa utakaoweza kuisaidia mahakama kuyapitia ili kujielekeza kwenye kesi hizo,” amedai Wakili Abubakari Mrisha.

Aliibua hoja kuwa kwenye kiapo cha Alute, aya ya tisa (N-S) Na. TL 12, ni ripoti za magazeti ya Nipashe na Mwananchi ambayo si uamuzi uliofanywa na Bunge.

Hoja nyingine iliibuliwa na Wakili wa Serikali Lucas Malunde akidai kuwa alichokifanya Spika ni kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa NEC ya kuwepo nafasi wazi ya kiti cha ubunge kwa sababu hakuwepo na hatekelezi majukumu ndani ya Bunge kama alivyofanya kwa mujibu wa kifungu cha 37(3).

“Aya ya 9(O) kwenye waombaji wanaomba tamko la uamuzi wa Spika wa Bunge, hakuna tamko lolote la kumvua ubunge Lissu lililotolewa na spika ndiyo maana hakuna uamuzi uliotolewa na Spika Ndugai,” alidai Wakili Malunde.

Malunde alidai taarifa hiyo ilitangazwa kwenye gazeti la serikali – Government Notice (GN) – hivyo hakutoa tamko la kumvua ubunge na kwamba Lissu hakujiuzulu wala hajafa.

“Hakuna mahali Spika alitoa tamko… alitoa taarifa ambayo inapopelekwa gazeti la serikali inakuwa mali ya serikali inayosambazwa, na mtu yeyote anaweza kuipata akihitaji,” alidai Wakili Malunde.

Alidai maamuzi ya kutostahili kuendelea na ubunge hayatolewi na Spika bali Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoelekeza kuwa mbunge atakosa sifa ya kuendelea na nafasi hiyo atakapokosa kuhudhuria vikao vitatu mfululizo vya bunge bila ya ruhusa ya Spika.

Hoja ya nne iliwasilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, George Mandepo ikigusia hati ya kiapo na nyaraka ya nguvu ya kisheria vilivyoendana na ombi lililowasilishwa na muombaji Mughwai vimekiuka Sheria ya Viapo Na. 8 Sura ya 12 ielezayo kuwa kiapo kitolewe mbele ya msimamizi wa viapo.

Kwenye hoja hiyo, upande huo unadai nyaraka ya mamlaka ya kisheria (Power of Attorney) ilisainiwa tarehe 9 Julai, 2019 nchini Ubelgiji; tarehe 18 Julai 2019 ikisainiwa na Mughwai pasina kuonesha kwa namna gani kiapo hicho kilitoka Ubelgiji na kufikia Dar es Salaam na baadaye jijini Arusha.

Wakili Mkuu Mandepo amedai sheria inaruhusu madai kufunguliwa na mtu binafsi au mwakilishi ambaye ana nguvu kisheria. Kwa hivyo, maombi yaliyopo mahakamani yamewasilishwa na Lissu kupitia mwakilishi wake ambaye ni Mughwai.

Alidai katika kuomba ridhaa ya kuwasilisha maombi yanatakiwa kusainiwa na muombaji au mwakilishi wake pamoja na kuambatanisha hati ya kiapo na muhuri wa wakili.

“Katika maombi haya yanaonesha kuwa Julai 9, mwaka huu Lissu alisaini kiapo hicho akiwa nchini Ubelgiji na muhuri wa wakili Sadolf Magai alisaini kwa anuani ya Dar es Salaam,” amedai Wakili Mkuu Mandepo.

Amedai ipo sheria inayosimamia maombi inayoeleza kiapo kinatakiwa kutolewa mbele ya msimamizi wako.

Wakili Mkuu Mandepo amedai kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria za Tanzania kwa sababu kiapo kilichowasilishwa kimesainiwa na muhuri wa Tanzania wakati kiapo kilisainiwa nchini Ubelgiji hivyo, si halali na maombi yaliyowasilishwa pia si halali.

Amedai wanashangaa Julai 9, mwaka huu siku ambayo kiapo kiliandaliwa huko Ubelgiji hakioneshi ni kwa namna gani kilifika jijini Arusha hivyo si kiapo cha kweli.

“Kiapo hiki kimebeba uongo kwa sababu moja: wakili Sadolf hajaleta hati ya kiapo mahakamani wala maelezo ya kuthibitisha kuwa alikwenda Ubelgiji na hakuna kumbukumbu kwamba wakili huyo aliidhinishwa kufanya kazi nchini Ubelgiji wakati aliapishwa na Jaji wa Tanzania,” alidai Wakili Mkuu Mandepo.

Kwenye hoja hiyo, upande huo ulijikita katika utaratibu wa kuandaa hati ya kiapo uliotekelezwa nchini Ubelgiji na Wakili Magai mwenye leseni ya kufanya kazi ya uwakili Tanzania amepata wapi mamlaka ya kumuapisha mtu aliyekuwa Ubelgiji.

Hoja ya tano: kuwa kwenye kiapo hicho “kuna maelezo ya uongo” kwenye aya ya 3, 4, 5, 6 na 8… mlalamikaji amemuandikia barua Lissu ilhali yeye ndiye aliyeandikiwa barua na Spika.

Hoja ya sita: Wakili Mkuu wa Serikali Dk. Mashamba amedai muombaji amechanganya maombi mawili tofauti kwenye ombi moja, kitendo kilichosababisha mahakama kuu nchini kuondoa kesi Na. 31/2018 aliyofungua Zitto Kabwe, Salum Bimani na Joran Bashange kwa hoja kuwa ‘ombi moja lilishika maombi mengi tofauti.’

Wakili Mkuu wa Serikali Dk. Mashamba alidai kuwa pingamizi wanazotoa zina mambo manne ya msingi, likiwemo la kuona kama mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza maombi hayo kama yalivyoletwa.

Pia alidai wameangalia iwapo muombaji ana uwezo wa kufanya hivyo na kama maombi hayo yameletwa mahakama sahihi kimamlaka.

Dk. Mashamba alidai wanaangalia kama nafuu zilizoombwa kwenye mahakama hiyo ni sahihi kuletwa mahakamani au la.

Akiwasilisha pingamizi hizo katika hoja ya kwanza, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abubakari Mrisha alidai mjibu maombi ameweka pingamizi la pili kwa lengo la kuonesha kuwa maombi yaliyowasilishwa hayakidhi matakwa ya kisheria.

Amedai yapo mambo sita ya kuzingatiwa kwa mleta maombi: kuhakikisha maombi yanaletwa ndani ya miezi sita baada ya maamuzi; mahakama kuona haja ya kusikiliza maombi hayo na maombi kuletwa kwa nia njema na siyo kwa lengo la kupotosha au kwa manufaa binafsi.

“Kati ya hayo, jambo moja pekee kwamba maombi haya yako ndani ya muda lakini mengine yamekosekana. Maombi haya hayakidhi kwa sababu hakuna maamuzi yoyote yaliyoambatanishwa katika maombi ili (mahakama) iweze kuyapitia na kuona kama kuna haja ya kuilazimisha mamlaka iliyotoa maamuzi kuyaondoa,” alidai Wakili Mrisha.

Akigusa kesi kama hiyo aliyofungua Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, dhidi ya Spika wa Bunge, Ndugai, wakili Mrisho alidai hakuna maamuzi yaliyoambatanishwa ili mahakama iweze kuyapitia na kutoa uamuzi.

Amedai Kanuni za Bunge zinaelekeza kuwa mbunge muathiriwa na maamuzi ya Spika, anatakiwa kuwasilisha pingamizi kwa Katibu wa Bunge ambaye ndiye atawasilisha pingamizi kwa spika.

Mrisho alidai kisheria walipaswa kuambatanisha maamuzi wanayolalamikia na kwamba katika kiapo kilichoandaliwa na Mughwai wameambatanisha nakala za magazeti ya Mwananchi na Nipashe ambayo kimsingi “hawawezi kuyaita maamuzi.”

“Sheria ya Uchaguzi inamtaka Spika kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwamba kuna kiti bungeni kiko wazi na kisha (tamko) inawekwa kwenye tangazo la serikali… tunaomba maombi haya yatupiliwe mbali kwa gharama,” amedai Wakili Mrisho.

Wakili Kibatala akijibu hoja hizo alianza na hoja ya kuambatanisha maombi sambamba na uamuzi wa Mahakama akieleza kuwa kifungu cha 5(2) cha Sheria ya Viapo, hakishurutishi kuwekwa nakala za uamuzi wa mahakama mbalimbali.

“Sio kwa bahati mbaya mleta maombi na kwamba si mara zote muombaji atalazimishwa kuleta maombi; ingekuwa ni sharti la lazima sheria ingeweka wazi bila ya kumung’unya maneno.”

Wakili Kibatala ameitaja kesi Na. 9 ya mwaka 2018 ya Bernad Msoza dhidi ya mwanasheria mkuu wa serikali iliyokuwa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga.

Hoja nyengine amedai kwenye Sheria ya Uchaguzi, kifungu 37(3) ambamo imeelezwa mazingira ya mbunge akijiuzulu au akipoteza maisha au sababu nyingine, spika atatangaza pia kumuandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutokana na uamuzi huo.

Akijibu hoja ya nyaraka ya mamlaka ya kisheria, ameeleza kuwa kiapo na nyaraka hizo hazina tatizo kisheria kwa kuwa muapaji ambaye ni Lissu, ameapishwa na Wakili Magai ambaye ameidhinishwa kuwa ni Kamshina wa viapo nchini.

Wakili Kibatala alieleza kuwa kisheria, kwa sasa Mtaturu si mbunge bali “mbunge mteule” asiyeweza kushiriki shughuli yoyote ya kibunge mpaka atakapoapishwa.

Kuhusu hoja ya walalamikiwa kuwa Lissu arudi bungeni kukata rufaa, wakili Kibatala aliita ni “hoja mfu” kwa kuwa “Lissu hawezi kurudi bungeni kutokana na yeye kuwa si mbunge sasa.”

Jeremiah Mtobesya, wakili mwengine wa mlalamikaji, alieleza kuwa mahakama itafikia uamuzi kwa kujipitisha kwenye Kanuni ya Bunge Na 5 fasili ya 2, 3 na 4 inayomuelekeza mbunge asiyeridhishwa na uamuzi wa spika kukata rufaa mahakamani.

Ameeleza kuwa walalamikiwa wanaingia kwenye kiapo na nyaraka za mamlaka ya kisheria ambazo “hazikutakiwa kuingiliwa kwa sasa kwa sababu ni sehemu ya ushahidi.”

Mawakili wengine waliosaidiana na Kibatala ni Omari Msemo na John Mallya.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Rais Samia aridhishwa utendaji mabalozi, awapa neno

Spread the loveRais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amewapongeza mabalozi  wanaowakilisha ...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

NMB yadhamini Mkutano Mkuu ALAT, kufunguliwa na Samia

Spread the loveBENKI ya NMB, imekabidhi hundi yenye thamani ya Sh. 120...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mipango na uwekezaji kutumia bilioni 121.3, mradi wa Bagamoyo wapewa kipaumbele

Spread the loveWIZARA ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, imeliomba Bunge...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mbunge ataka kasi uzalishaji walimu ipunguzwe akidai hakuna ajira

Spread the loveMBUNGE wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi, ameishauri Serikali ipunguze kasi...

error: Content is protected !!