December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mawakili wa Mbowe wamkataa shahidi, waweka pingamizi tena

Spread the love

 

MAWAKILI wa utetezi katika mashtaka ya ugaidi yanayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu, wamepinga kupokelewa kwa barua inayomthibitisha askari mpelelezi, DC Ricardo Msemwa, kuwa ndiye aliyepokea kitabu cha mahabusu, kutoka kwa Msajili wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni Halfan Hassan Bwire, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya ambao walikuwa ni makomandoo wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Mawakili hao wa utetezi, wameweka pingamizi hilo leo Ijumaa, tarehe 12 Novemba 2021, mbele ya Jaji Joachim Tiganga, anayeisikiliza baada ya Msemwa kuiomba mahakama ipokee barua hiyo kama sehemu ya ushahidi wa jamhuri.

Ni katika kesi ndogo ya kupinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu, Ling’wenya, yasipokelewe kama sehemu ya ushahidi wa jamhuri, katika kesi ya msingi inayomkabili Mbowe na wenzake.

Mawakili wa utetezi walipinga kielelezo hicho wakidai, shahidi aliyeomba barua hiyo ipokelewe hana uwezo wa kufanya hivyo kisheria, kwa madai nyaraka hiyo ililengwa mahususi kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), jijini Dodoma na kuwa Msemwa siyo mtumishi wa ofisi hiyo hivyo barua hiyo haimhusu.

Pia, walidai shahidi huyo katika ushahidi wake, hakusema barua hiyo imemfikiaje na au kueleza uwepo wa jina lake katika nyaraka hiyo.

Hata hivyo, mawakili wa jamhuri waliiomba mahakama hiyo itupilie mbali pingamizi hilo, kwa madai shahidi alijenga msingi ulioonesha kuhusika na nyaraka hiyo.
Mawakili hao wa jamhuri walidai, katika ushahidi wake shahidi alielezea namna alivyokabidhiwa barua hiyo na Msajili wa Mahakama Kuu, Divisheni ya makosa ya rushwa na Uhujumu Uchumi.

Pia, aliieleza mahakama hiyo, katika barua hiyo kuna jina na cheo chake.

Kitabu hicho cha mahabusu ni kile kinachoonesha taarifa za washtakiwa wawili katika kesi ya msingi, Ling’wenya na Adam Kasekwa, kuwa walifikishwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, tarehe 7 Agosti 2020, baada ya kukamatwa mkoani Kilimanjaro, tarehe 5 Agosti 2020 kwa kosa la kula njama za kufanya vitenso vya kigaidi.

Mara ya kwanza kitabu hicho kilipokelewa mahakamani hapo, kama sehemu ya ushahidi wa jamhuri katika kesi ndogo ya kupinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili, Kasekwa.

Ambapo kiliwasilishwa na DC Msemwa akitoa ushahidi katika kesi hiyo ndogo.

Hoja nyingine ambayo utetezi waliibua ni wakati shahidi huyo akiendelea kutoa ushahidi wake, kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi Peter Kibatala alidai, shahidi akiwa kizimbani alikuwa na simu, diary pamoja na kalamu.

Kibatala alimwomba Jaji Tiganga wajiridhishe kama shahidi huyo wa pili wa jamhuri haandiki chochote “na kama ameingia na vitu visivyoruhusiwa kizimbani tunaomba aondolewe kuwa shahidi.”

Kibatala aliomba mawakili wa pande zote mbili watoke wakamkague, kabla hata hawajaenda kumkagua, Msemwa yeye mwenyewe alionesha diary, kalamu, karatasi pamoja na simu.

Wakili huyo alisema, vitu hivyo viwekwe chini ya uangalizi wa mahakama kwanza kama kesi hiyo itaendelea.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Jumatatu tarehe 15 Novemba 2021, ambapo Jaji Tiganga atoa uamuzi wa masuala hayo mawili na watuhumiwa wamerudishwa rumande kwani kesi inayowakabili haina dhamana.

error: Content is protected !!