August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mawakili wa Chadema wapinga hoja tano za kina Mdee

Wakili wa Chadema, wakiongozwa na Peter Kibatala (katikati) wakiwa mahakamani

Spread the love

 

MAWAKILI wa pande mbili (waleta maombi na wajibu maombi) katika kesi ya Halima Mdee na wenzake 18 wameibua mvutano Mahakamani ikiwa kama hoja tano zilizowasilishwa na waleta maombi ya kutaka kufungua kesi ya kupinga kuvuliwa uanachama wa Chadema zina mashiko. Anaripoti Regina Mkonde Dar es Salaam … (endelea).

Mvutano huo umeibuka leo Alhamisi tarehe 30, Juni 2022, baada ya Mdee na wenzake 18, kupitia mawakili wao wakiongozwa na Wakili Ipilinga Panya, kuwasilisha hoja hizo wakiiomba Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu ya Dar es Salaam, ifanye mapitio ya kimahakama juu ya mchakato uliotumika kuwafukuza uanachama wa Chadema.

Akijibu hoja za mawakili wa kina Mdee, Wakili wa Chadema, Peter Kibatala, ameiomba mahakama hiyo iikatae hoja ya wabunge hao iliyodai wamefungua maombi ndani ya muda.

Amedai yalifunguliwa nje ya muda kisheria kwa kuwa yalipaswa kufunguliwa ndani ya miezi sita tangu walipofukuzwa uanachama tarehe 27 Novemba 2020.

“Uwepo wa haki ya kukata rufaa au uwepo wa rufaa kukata rufaa haiiondolei mahakama haki yake ya kufanya mapitio. Suala hilo ni kutegemeana na suala husika lililopo mbele ya mahakama, mahakama haiwezi kutoa ruhusa sababu maombi hayo yako nje ya muda,” amedai Wakili Kibatala.

Kuhusu hoja ya kina Mdee kwamba maamuzi ya Chadema kuwafukuza yalikuwa ya umma, Kibatala aliipinga akidai Bodi ya Wadhamini ya Chadema siyo ya umma na kwamba maamuzi yake siyo ya umma.

“Hakuna uhusiano wa chombo hicho na taasisi nyingine za Kiserikali. Chama cha siasa hakuna uhusiano wa moja kwa moja, isipokuwa chenyewe kinakuwa regurated (dhibitiwa). Hata ndoa inakuwa regurated (inadhibitiwa) lakini kukitokea mgogoro huwezi kumleta mmeo au mkeo kwenye mapitio ya mahakama,” amedai Wakili Kibatala.

Wakili Kibatala alijibu hoja ya mawakili wa kina Mdee iliyodai wametinga mahakamani baada ya kukosa njia mbadala ya kupata haki yao, alijibu akidai katiba ya Chadema imetoa njia mbadala kwa mwanachama aliyefukuzwa kuomba uanachama upya.

“Mwanachama aliyefukuzwa uanachama anaruhusiwa kuandika barua kwenda ngazi iliyomfukuza uanachama, kueleza sababu za kuomba kurudishiwa uanachama,” amedai Wakili Kibatala.

Katika hoja ya kina Mdee iliyodai kulikuwa na upendeleo wakati wa uamuzi wa rufaa zao, Wakili Kibatala amedai wakati wajumbe hao wanashiriki kikao cha Baraza hilo, hawakuomba watolewe.

“Hoja ya kwamba wajumbe hao waliingia kamati kuu na kwa mujibu wao kulikuwa na upendeleo na kwamba maamuzi uliingiliwa, ukiangalia namba ya wajumbe 28 hawawezi wakabadilisha maamuzi ya bodi kubwa . Lakini pia, wanachama Chadema walijiunga kwa hiari na suala hilo liliwekwa katika katiba ya Chadema, wana elimu kuhusu huu mchakato wa ndani na walikubali kwa hiari yao,” amedai Wakili Kibatala.

error: Content is protected !!