MAWAKILI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wameiomba Mahakama Kuu, Masjala Kuu, jijini Dar es Salaam, wafunge maswali ya dodoso kwa baadhi ya wabunge viti maalum, waliofungua kesi mahakakani hapo kupinga uamuzi wa kuvuliwa uanachama. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Ombi hilo limewasilishwa leo tarehe 6 Machi 2023, mahakamani hapo mbele ya Jaji Cyprian Mkeha, na Wakili wa Chadema, Hekima Mwasipu, wakati Mbunge wa Viti Maalum, Jesca Kishoa, alitarajiwa kendelea kuulizwa maswali ya dodoso na mawakili wa chama hicho.
Awali, Wakili Mwasipu aliieleza mahakama hiyo kuwa, kesi ilipangwa kuja kuendelea kwa Kishoa kumalizia kuulizwa maswali ya dodoso kuhusu malalamiko yake ya kufukuzwa Chadema kinyume cha Sheria, lakini aliomba mahakama hiyo wafunge kumuuliza maswali hayo.
Kishoa alianza kuulizwa maswali hayo Novemba mwaka jana. Mbunge huyo alitanguliwa na baadhi ya wabunge ambao walihojiwa maswali ya dodoso kuhusu hati zao za viapo, akiwemo Nusrat Hanje na Hawa Mwaifunga.
Katika hatua nyingine, Wakili Mwasipu aliiomba mahakama hiyo wafunge maswali ya dodoso kwa wabunge waliosalia, akiwemo Halima Mdee, Ester Bulaya na Esther Matiko.
Wakili huyo wa Chadema alidai kuwa, wameamua kufunga maswali hayo baada ya kutafakari kwa kina na kubaini kwamba hawana maswali ya ziada kwa wabunge hao.
Baada ya kuwasilisha ombi hilo, Jaji Mkeha alikubali wafunge maswali ya dodoso.
Awali, Chadema waliomba kuwahoji maswali ya dodoso wabunge hao viti maalum, dhidi ya hati zao za viapo walivyowasilisha wakati wanafungua kesi ya kupinga kufukuzwa Chadema.
Katika kesi hiyo Na. 36/2022, mawakili wa Chadema waliwahoji maswali kadhaa wabunge hao, juu ya malalamiko yao ya kufukuzwa bila kupewa nafasi ya kujitetea, pamoja na mchakato huo kufanyika kwa upendeleo.
Mawakili hao katika nyakati tofauti, waliwahoji baadhi ya wabunge hao kwa nini hawakuitikia wito wa kwenda mbele ya vikao vya maamuzi kwa ajili ya kujitetea, ambapo walijibu wakidai kwamba, waliomba kuongezewa muda ili kujipanga kujibu pamoja na kutuliza hasira za Wanachadema zilizotokana na uamuzi wao wa kuapishwa kuwa wabunge viti maalum.
Katika mahojiano hayo, wabunge waliohojiwa walidai wao si wasaliti na wala hawakujipeleka bungeni jijini Dodoma kama inavyodaiwa, bali walikwenda kwa mujibu wa sheria baada ya majina yao kuteuliwa na vigogo wa Chadema.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 9 Machi mwaka huu.
Leave a comment