July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mawakili Chadema, Jamhuri wavutana mbele ya hakimu

Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imepanga kesho tarehe 18 Oktoba 2019, kutoa uamuzi mdogo kwenye kesi ya uchochezi inayowahusu Freeman Mbowe na wenzake wanane. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Ni baada ya upande wa mashtaka (Jamhuri), uliopinga shahidi wa kwanza wa Chadema kutoa ushahidi wake, kwenye kesi inayowakabilidili viongozi hao wa Chadema.

Pingamizi hilo liliwasilishwa na upande wa washtakiwa tarehe 15 Oktoba 2019 ambapo leo tarehe 17 Oktoba 2019, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesisitiza kumpinga shahidi huyo wa kwanza.

Benson Kigaila, Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzi wa Chadema ambaye ndiye shahidi wa kwanza, amekataliwa na mawakili wa Jamhuri ambao wamedai, washtakiwa waanze kujitolea ushahidi wenyewe.

Hata hivyo, upande wa utetezi kupitia wakili Peter Kibatala umepinga hoja ya Jamhuri kuwa, hakuna sheria maalum inayolazimisha utetezi uanzishwe na mshtakiwa, na kwamba washtakiwa watatoa ushahidi wao mwisho.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, amesema kuwa atatoa uamuzi kesho saa 6 asubuhi.

Kwenye kesi hiyo ya uchochezi namba 112/2018, washtakiwa ni Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Dk. Vicent Mashinji, Katibu Mkuu-Taifa; John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu – Bara na Salumu Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu -Z’Bar.

Wengine ni Ester Matiko Mbunge wa Tarime Mjini; Halima Mdee, Mbunge wa Kawe; Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini; John Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini na Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini.

error: Content is protected !!