January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mawakala wa ajira wagomea Serikali

Gaudensia Kabaka

Spread the love

MAWAKALA Binafsi wa Huduma za Ajira, wameendelea kukiuka agizo la Serikali la kutokodisha wafanyakazi na badala yake kampuni wanazozifanyia kazi ndizo zinatakiwa kuingia nao mikataba. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Serikali kupita Wizara ya Kazi na Ajira, iliweka zuio hilo baada ya kupokea malalamiko ya wadau mbalimbali kuhusu utaratibu wa udalali wa kukodisha wafanyakazi katika makampuni unaofanywa na baadhi ya mawakala hao.

Baada ya kufanya uchunguzi wa kina, wizara ilibaini kuwa utaratibu wa kukodisha wafanyakazi unaofanywa na baadhi ya Wakala Binafsi wa Huduma za Ajira ni kinyume cha Sheria ya Huduma za Ajira Na. 9 ya Mwaka 1999 [Sura 243 kama ilivyorejewa Mwaka 2002].

Kwa mujibu wa Kifungu 4 cha Sheria hii, majukumu ya msingi ya Wakala wa Huduma za Ajira ni kuwaandaa na kuwaunganisha watafuta kazi na waajiri kwa kutoa mafunzo na ushauri elekezi kwa watafuta kazi, kutafuta fursa za ajira na kutoa taarifa za soko la ajira. 

Hivyo, mawakala hawapaswi kuwaajiri wafanyakazi waliowatafutia kazi kwa niaba ya waajiri wengine. Kufanya hivyo, ni ujanja unaotumiwa na baadhi ya waajiri na mawakala kwa lengo la kukwepa kodi na kujipatia faida kwa kukwepa kutoa haki za msingi za wafanyakazi kwa mujibu wa Sheria za Kazi.

Baadhi ya makampuni yanayokodisha wafanyakazi yamefanyiwa uhakiki na Mamlaka ya Mapatao (TRA) na kubainika kukwepa kodi ya mapato ya ajira (PAYE) na kodi ya mapato ya kampuni kinyume na Kifungu cha 7 cha Sheria ya Kodi ya Mapato ya Mwaka 2004 [Sura 332 kama ilivyorejewa Mwaka 2008].

Pia uchunguzi huo umebaini athari mbalimbali kwa wafanyakazi wanaoajiriwa kwa utaratibu huo ambapo wanakosa haki ya hifadhi ya jamii kama vile likizo ya uzazi na matibabu kinyume na sheria mbalimbali za mifuko ya hifadhi ya jamii.

Agizo la serikali lilitolewa 27 Januari 2014, ambapo mawakala hao walitakiwa kukamilisha utaratibu wa kuwaunganisha wafanyakazi waliowakodisha ili waingie mikataba na makampuni wanayoyafanyia kazi ndani ya mwezi mmoja.

Pia, ndani ya kipindi hicho mawakala hao, walitakiwa kuwasilisha taarifa za utekelezaji kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi na Ajira kabla au ifikapo 28 Februari 2014.

Hadi kufikia tarehe ya mwisho, maombi ya mawakala 56 yalikuwa yamewasilishwa kwa kamishna wa kazi, ambapo baadhi ya mawakala walikuwa wametimiza masharti yote na wengine wakiomba kuongezewa muda.

Ukiwa ni zaidi ya mwaka mmoja, uchunguzi wa MwanaHALISIOnline umebaini kuwa, mawakala wengi wameendelea kufanya ujanja wa ama kuwaachisha kazi waajiriwa kwa kisingizio cha vitengo vyao kufutwa katika makampuni husika au kuwahamishia katika makampuni mengine.

Deloitte ni mojawapo wa mawakala hao, ambaye analalamikiwa na wafanyakazi aliokuwa amewakodisha kwa kampuni ya Petrobras kisha kuwaachisha kazi ghafla baada ya agizo la serikali kutoka.

Wafanyakazi hao ambao walikuwa katika vitengo mbalimbali vya uhandisi, uhasibu na madereva, wameliambia MwanaHALISIOnline kuwa “Deloitte  alituambiwa vitengo vyetu vinafutwa Petrobras, hivyo tukalipwa mafao ya kuchisha kazi.”

“Agizo la serikali lilitaka tufunge mikataba moja kwa moja na makapuni tunayoyafanyia kazi, sasa wanakwepa na kutuachisha kazi. Lakini wako baadhi ya madereva wameondolewa Petrobras na kupelekwa kampuni ya KK Security.”adai mmoja wa wafanyakazi hao ambaye amefungua malalamiko katika Makahama ya Kazi.

Kwa mujibu wa nyaraka zilizopo, mwaka 2013, Deloitte aliingia mkataba wa wa kufanya kazi ya uwakala wa ajira wa Petrobras – kampuni ya uchimbaji mafuta ya Brazil inayofanya kazi zake hapa nchini.

Kufuatia agizo la serikali, Deloitte ilisitisha udalali kwa Petrobras huku ikishidwa kuwaunganisha wafanyakazi wake waingie mikataba moja kwa moja na kampuni hiyo.

Kwa mfano; 9 Aprili 2014, Joseph Eshun – Mkurugenzi wa Deloitte alimwandikia barua ya kumwachisha kazi Hamis Mrisho – aliyeajiliwa na wakala huyo kufanya kazi ya udereva Petrobras.

Sehemu ya barua hiyo iliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza, inatafsirika “kufuatia maelekezo ya Wizara ya Kazi na Ajira kwa mawakala wa ajira binafsi na taasisi zinazosaidia kufanikisha ajira ya 27 January 2014, tumelazimika kuvunja mkataba wako wa kazi na kampuni yetu.”

“Barua hii inatimiza matakwa ya barua ya wizara kwamba usitishwaji wa ajira yako ufanywe miezi mitatu baada ya tarehe ya barua ya awali. Siku yako ya mwisho ya kufanya kazi ni 28 Aprili 2014 kwa mujibu wa mkataba wa sasa,” inasomeka.

Mrisho anasema, “baada ya kupewa barua ya kusimamishwa kazi, Petrobras hawakuniajili wala Deloitte hawakufanya jitihada zozote niweze kuajiriwa na Petrobras.”

Anaongeza kuwa, Petrobras walimwambia kama anataka kazi kwao, aende kampuni ya KK Securty aajiriwe huko kisha atakuwa anafanya kazi Petrobras huku akiwa hana utaalam wowote wa masuala ya ulinzi.

Leonard Akaro-mhasibu mkuu wa KK Securty, ameliambia MwanaHALISIOnline kuwa “Sisi tuna mkataba wa kutoa huduma za ulinzi Petrobrass. Walituomba tuwapatie madereva ambao wana ujuzi wa masuala ya ulinzi. Hivyo kipaumbele tulitoa kwa madereva waliokuwa wanafanya kazi Petrobras. Tuliwafanyia mafunzo ya ulinzi”.

“Mpaka sasa madereva 6 wa kampuni ya Petrobras hawaajaajiriwa. Sisi tunaofanya kazi za ndani ndio tumeajiriwa. Huu ni uonevu,” anasema mtoa taarifa wetu ndani ya ofsi za Petrobras.

Alipotafutwa msemaji wa Wizara ya Kazi na Ajira, Ridhiwan Wema kuhusu baadhi ya mawakala kukaidi agizo la serikali, amesema “hizi taarifa hatujazipata. Nashukuru kwa kutuletea.Tutazifanyia kazi.”

Wema amesema “hadi kufikia 13 Aprili mwaka huu, mawakala 96 walikuwa tayari wameidhinishwa kufanya kazi ya uwakala kuanzia 13 Machi 2015 hadi 12 Machi 2016. Na watalipa ada ya usajili ya mwaka Sh. 300,000.”

“Changamoto kubwa iliyopo ni kwamba wizara ina uhaba wa watendaji wa kitengo cha ukaguzi. Nchi nzima wapo maafisa takribani 98. Ni zaidi ya mara tatu ya mahitaji. Hatuna uwezo wa kufika kila mahali, hivyo tunaomba watu wenye taarifa watupatie tutazifanyia kazi,”amesema Wema.

Makampuni ya Deloite na Petrobras hayakuwa tayari kutoa ufafanuzi. Badala yake kila walipotafutwa walipiga chenga za kutana mwandishi aende ofisini kwao na alipofika aliambiwa msemaji ametoka.

error: Content is protected !!