Saturday , 25 March 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Maumivu ya wapinzani, vigogo 2020
Habari za SiasaMakala & UchambuziTangulizi

Maumivu ya wapinzani, vigogo 2020

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa
Spread the love

SAFARI ya kuhitimisha siku 365 za mwaka 2020 inaelekea ukingoni huku ikiwa imeshuhudia machozi na damu kwa wanasiasa hususan wa upinzani, wanaharakati pamoja na waandishi wa habari. Anaandika Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Mwaka 2020 umekuwa mgumu kwa wanasiasa wakubwa wa vyama vikuu vya upinzani nchini, mwaka ambao umeacha kovu na kumbukumbu katika historia ya maisha yao ya kupigania demokrasia.

Ni mwaka ambao umeshuhudia viongozi waandamizi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania- Chadema wakihukumiwa na kulazimika kutumia mamilioni kujinasua na kifungo gerezani.

Safari hii ya siku 365, zitahitimishwa zikiacha kumbukumbu kwa Mwandishi wa Habari, Erick Kabendera kusota mahabusu kwa kesi ya uhujumu uchumi na kumfanya kutoshiriki maziko ya mama yake mzazi, Verdiana Mjwahuzi.

Mwaka 2020, umeshuhudia aliyekuwa Kamshina wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake, wakitoka katika kuta za gereza, baada ya kuwamo humo kwa miezi 52 na siku 25.

MwanaHALISI Online, limezichambua baadhi ya kesi na matukio mbalimbali yaliyojili kuanzia Januari – Desemba 2020.

Vigogo Chadema

Tarehe 10 Machi 2020, viongozi waandamizi wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wao, Freeman Mbowe, walihukumiwa kulipa Sh. 350 Milioni kwa pamoja au kwenda jela miezi mitano kila mmoja baada ya kukutwa hatiani katika makosa 12 kati ya 13 waliyoshtakiwa Februari 2018.

Hukumu hiyo ya kesi namba 112 ya mwaka 2018, ilitolewa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Mbali na Mbowe, wengine ni; Jonh Mnyika (Katibu Mkuuwa Chadema), Salumu Mwalimu (Naibu Katibu Mkuu-Zanzibar) na Dk. Vicent Mashinji (aliyekuwa katibu mkuu ambaye baadaye alihamia Chama Cha Mapinduzi).

Halima Mdee

Wengine ni wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho, John Heche na Mchungaji Peter Msigwa. Pia, Esther Matiko, Ester Bulaya na Halima Mdee walikuwa miongoni mwa waliohukumiwa ambao kwa sasa wamekwisha fukuzwa uanachama ndani ya Chadema.

Mamilioni hayo, yalichangwa na wananchi kwa njia mbalimbali na kuwawezesha kutoka na kuendelea na harakati zao za kisiasa huku Dk. Mashinji ambaye yeye alilipiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wakati Chadema kinaendelea na mchakato wa kuwaondoa viongozi gereza la Segerea, aliyekuwa mwenyekiti wa baraza la wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee akiwa na kina Bulaya, Boniface Jocob aliyekuwa Meya wa Manspaa ya Ubungo na wafuasi 25  walikamatwa maeneo ya gereza la Segerea kwa tuhuma za kufanya vurugu.

Mdee, Bulaya, Msigwa na Heche Kisutu

Mdee, Bulaya na Jesca Kishoa, aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Bawacha walijeruhiwa maeneo mbalimbali ya miili yao na kuwafanya kulazwa siku kadhaa hospitalini kwa matibabu zaidi.

Mdee na wenzake hao, walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, tarehe 23 Machi 2020  na kushtakiwa kwa makosa saba kwenye kesi ya jinai namba 61 ya mwaka 2020  likiwemo la kufanya vurugu gereza la Segerea na kuhalibu mali za gereza hilo.

Watuhumiwa hao wote walipewa dhamana na kesi yao inaendelea huku Chadema kikijitenga kuwatetea Mdee, Bulaya na Kishoa ambao tarehe 27 Novemba 2020, walifukuzwa ndani ya chama hicho.

Zitto atiwa hatiani

Miezi miwili baadaye, Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam, mbele ya hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi, Zitto Kabwe kiongozi wa ACT-Wazalendo alihukumiwa mahakamani hapo kwa tuhuma za kutoa lugha za kichochezi.

Zitto aliyekuwa mbunge wa Kigoma Mjini, alikuwa akituhumiwa kwa makosa ya uchochezi kwenye kesi namba 327 ya mwaka 2018.

Tarehe 29 Machi 2020, ikiwa ni siku ya hukumu, Zitto alifika mahakamani akiwa tayari amejiandaa kwa kunyoa kipara. Hakimu Shaidi alimtia hatiani Zitto lakini ikamwachia kwa sharti la kutotoa au kuandika uchochezi katika kipindi cha mwaka mmoja.

Kubenea akamatwa

Miongoni mwa matukio yaliyotikisa mwaka 2020, ni kukamatwa kwa aliyekuwa Mbunge wa Ubungo, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Saed Kubenea.

Kubenea alikamatwa katikati ya kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika tarwehe 25 Oktoba 2020 akidaiwa kuingia nchini Tanzania kupitia mpaka wa Namanga jijini Arusha kwa njia za panya akiwa na fedha taslimu dola za Kimarekeani 8,000, Shilingi za Kenya 491,700 na Sh.71,000 za Tanzania.

Saed Kubenea, Mbunge wa Ubungo

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka Tanzania (DPP), Biswalo Mganga ilisema Kubenea alikamatwa mkoani Arusha tarehe 5 Septemba 2020, akitokea kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya, maeneo ya Namanga.

Taarifa hiyo ya DPP iliyotolewa tarehe 7 Septemba 2020, ilidai Kubenea alikamatwa katika gari la abiria akiwa na fedha hizo.

Wakati Kubenea anakamatwa, alikuwa Mgombea Ubunge Kinondoni jijini Dar es Salaam, kupitia Chama cha ACT-Wazalendo katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020.

Kufuatia sakata hilo, DPP Mganga alimfungulia Kubenea kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha,

kwa tuhuma za kuingia nchini Tanzania kinyume na Sheria ya Uhamiaji, pamoja na kuingiza fedha za kigeni nchini, bila kutoa tamko kinyume na kanuni za utoaji tamko la fedha mpakani za mwaka 2016.

Kubenea alisota mahabusu mkoani Arusha kwa zaidi ya siku 10 hadi alipoachiwa kwa dhamana ya Sh. 14

Kubenea ambaye kitaalum ni Mwandishi wa habari, alipandishwa mahakamani tarehe 7 Septemba 2020 na tarehe 11 Septemba 2020 alipata dhmana na kesi yake inaendelea.

Kabendera ahukumiwa

Miezi sita ya Mwandishi wa Habari nchini Tanzania, Erick Kabendera kuwa kizuizini katika gereza la Segerea jijini Dar es Salaam ilihitimishwa tarehe 24 Februari 2020, baada ya kuhukumiwa katika mashtaka yaliyokuwa yanamkabili likiwemo la utakatishaji fedha.

Kabendera alipandikwa kwa mara ya kwanza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, tarehe 5 Agosti 2019 kwa kosa la kukwepa kodi na kutakatisha fedha Sh. 172.24 milioni.

Tarehe 24, Februari 2020, Hakimu Mkazi Mkuu Janeth Mtega, alimuhukumu Kabendera baada ya kukiri mashtaka yake kwa njia ya majadiliano na Mwendesha Mashataka wa Serikali ya Tanzania (DPP) kulipa faini ya Sh. 250,000 kwa kosa la kukwepa kodi.

Katika shitaka la kutakatisha fedha, Hakimu Mtenga alimhukumu kulipa faini ya Sh. 100 milioni na kulipa faini ya Sh. 172 milioni kwa kosa la kukwepa kodi.

Kabendera akiwa gerezani, mama yake mzazi, Verdiana Mjwahuzi (80) alifariki dunia 31 Desemba 2019.

Kabendera aliwasilisha maombi mahakamani hapo kuomba kibali cha kwenda kuaga mwili wa mama yake katika Kanisa Katoliki Chang’ombe, hata hivyo maombi hayo yalitupiliwa mbali kwa kuwa mahakama hiyo haikuwa na uwezo wa kusikiliza maombi hayo.

Mwili wa mama yake, ulizikwa tarehe 7 Januari 2020, kijiji cha Kashenge, Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera huku picha ya Kabendera akibubujikwa machozi ndani ya mahakama, ikiwekwa kwenye moja ya kiti kuonyesha ushiriki wake huku yeye akiwa gerezani.

Mwandishi wa habari mwingine ambaye amekutwa na kadhia ni, Angellah Kiwia wa Gazeti la Jamhuri ambaye tarehe 12 Mei 2020 alipandishwa mahakama ya Kisutu yeye na wenzake na kusomewa mashtaka ya uhujumu uchumi na kutishia kuua ambapo mpaka sasa yupo mahabusu kutoka na shauri hilo kuwa halina dhamana.

Kesi za Jamii Forum

Katika kesi kadhaa ambazo zilikuwa zinamkabili Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Forum, Maxence Melo zilitolewa hukumu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Tarehe 8 Aprili 2020, Melo alihukumiwa kulipa faini ya Sh. 3 milioni ama kutumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani baada ya kukutwa na hatia ya kuzuia jeshi la polisi kufanya kazi yao ya uchunguzi.

Maxence Melo

Pia, mahakama hiyo, ilimuachia huru Mike Mushi, mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo ya jinai namba 456 ya 2016 ambaye ni mwanahisa mwenzake. Aliachiwa huru baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha shtaka dhidi yake.

Melo alilipa faini na kuachiwa huru.

Tarehe 17 Novemba 2020, Mahakama hiyo ilimuhukumu Melo kwenye kesi nyingine ya kuzuia jeshi la Polisi kutekeleza majukumu yake na kutakiwa kutofanya kosa lolote ndani ya mwaka mmoja.

Hukumu hiyo ya kesi namba 458 ya mwaka 2016, ilitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Huruma Shaidi aliyemkuta na hatia ya kuzuia jeshi la polisi kuzuia upelelezi uliokuwa ukifanyika

Wakati akitoa hukumu hiyo iliyokuwa inawakabili Melo na mwenzake Mike Mushi, Hakimu Shaidi alimwachia Mushi kutokana na kutokuwa na kosa lolote.

Kwenye shauri hilo, mabosi hao wa Jamii forums walishitakiwa kuendesha Mtandao wa Jamii Forum bila kutumia kikoa cha Tanzania mathalan;-www.habari.tz).

Katika kesi ya msingi, washtakiwa walidaiwa kuzuia jeshi la Polisi kufanya uchunguzi, kinyume na Sheria Namba 22 cha Sheria ya Makosa ya Mtandano Namba 14 ya mwaka 2015.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo, kati ya Aprili Mosi, 2016 na 13 Desemba  2016 katika maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Kitilya na wenzake

Siku 1,608 za aliyekuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake, zilihitimishwa tarehe 26 Agosti 2020 na Mahakama Kuu kitengo cha uhujumu uchumi kwa kuwahukumu kwenda jela miezi sita au kulipa faini Sh.1.5 bilioni.

Kiwango hicho ni fidia na kila mmoja kulipa Sh.1 milioni baada ya kukiri kutenda kosa la kuisababisha hasara serikali na utakatishaji fedha.

Kitilya ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Ushauri wa Uwekezaji, Huduma za Uwezeshaji na Upatikanaji wa Fedha na wenzake, Shose Sinare, Sioi Solomon, Bedason Shallanda na Alfred Misana walikuwa wanakabiliwa na mashataka 58 ambayo yalifutwa na kubakiza moja la kuisababishia hasara serikali.

Washtakiwa hao, walidaiwa kutenda kosa hilo kati ya Machi 2013 na Septemba 2015 wakati wa mchakato wa mkopo wa dola za Marekani milioni 550 kwa Serikali ya Tanzania kutoka benki ya Standard ya Uingereza.

Aidha, wanadaiwa kula njama za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu ili waweze kujinufaisha wenyewe na washirika wao.

Kitilya na wenzake, walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza tarehe 1 Aprili 2016 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na hadi wanatoka tarehe 26 Agosti 2020, walikuwa wamekaa mahabusu siku 1,608 sawa na miaka minne, miezi minne minne na siku 25. 

Endelea kufuatilia MwanaHALISI Online na MwanaHALISI TV kwa habari mbalimbali

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Rais Samia aagiza iundwe kamati ya pamoja ya Mawaziri mradi wa BBT

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amewaagiza mawaziri kuunda kamati...

Makala & Uchambuzi

Ruth Zaipuna: Sekta ya kibenki imeimarika maradufu miaka miwili ya Dk. Samia

Spread the loveTarehe 19 ya mwezi Machi, ni siku muhimu sana kwa...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Miaka miwili ya Rais Samia, TMA yaimarika, yatoa utabiri kwa usahihi

Spread the loveMACHI 19, 2023 Rais Samia Suluhu Hassan anatamiza miaka miwili...

Habari za Siasa

Rais Samia apangua makatibu tawala mikoa, ateua Kamishna DCEA

Spread the loveALIYEKUWA Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Gerald...

error: Content is protected !!