July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mauji ya kikatili yashamiri Bukoba

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Henry Mwaibambe

Spread the love

MATUKIO ya watu wasiofahamika kuua raia wema kwa kuwacharanga mapanga na kisha kutelekeza miili yao, yanazidi kujirudia katika Kata ya Kitendaguro, Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera. Anaandika Mwandishi wetu (endelea).

Ikiwa ni miezi michache tangu kuuawa kikatili kwa watu watatu, Jeshi la Polisi mkoani humo linawashikilia watu 12 kwa tuhuma za mauaji ya watu wengine wawili kwa kuwacharanga mapanga vichwani katika kata ya Kitendaguro.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Henry Mwaibambe amesema kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Machi 9 mwaka huu, na kuwataja waliouawa kuwa ni Emani Gilidi (35) mkazi wa Kanazi na Evarist Maliseli (30).

Amesema kabla ya Gilidi kuuawa, alikuwa anakunywa pombe za kienyeji katika nyumba moja ndipo kukatokea ugomvi wa kupigana kati yake na wenzake.

“Baada ya ugomvi kuisha, marehemu aliamua kuondoka eneo hilo, lakini kabla hajafika mbali akavamiwa na watu wasiojulikana, wakamcharanga mapanga sehemu ya kichwa hali iliyopelekea kutokwa na damu nyingi na kusababisha kifo chake,” amesema.

Kwa mujibu wa kamanda, watuhumiwa waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo ni wale aliokuwa kigombana nao marehemu ambapo baadhi walikutwa na majeraha madogo, hivyo uchunguzi bado unaendelea.

Kuhusu kifo cha pili cha Maliseli, Kamanda amesema kuwa mwili wake ulikutwa barabarani ukiwa umecharangwa kichwani huku akiwa na jeraha kubwa kisogoni.

Amesema upelelezi wa kina unaendelea kufanywa na jeshi la polisi huku wananchi wakiombwa kutoa taarifa na ushirikiano pindi wanapoona matukio kama hayo.

error: Content is protected !!