JESHI la Polisi mkoani Tabora, limedai mauaji ya mtoto Nyanzobhe Mwandu (4), yaliyotokea tarehe 16 Juni 2021, yalipangwa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Mauaji hayo yalitokea katika Kijiji cha Kombe, Kata ya Usinge mkoani Tabora, ambapo sasa kauli ya polisi kwamba mauaji hayo yalipangwa, imezua utata.
Taarifa za awali zilieleza, tukio hilo la kinyama lilifanywa na baadhi ya Askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Hifadhi ya Wanyamapori (TAWA), waliokuwa wakitekeleza operesheni ya kuwaondoa wananchi wanaodaiwa kuvamia eneo la hifadhi ya Kijiji ya Ngitiri, mkoani humo.
Akizungumza na MwanaHALISI Online kwa simu, leo tarehe 21 Juni 2021, Kamanda wa Jeshi la Polisi Tabora, Safia Jongo, amesema tukio hilo lina utata, kwa madai kwamba ushahidi wa awali unaonesha, lilitengenezwa na baadhi ya watu ili kuzuia operesheni hiyo.
“Hilo tukio ni kweli limetokea, lakini lina utata mkubwa sana kulingana na ushahidi ambao umekusanywa, kulihusisha hilo tukio na operesheni za nyuma. Ushahidi unalenga kwamba, ni tukio la kutengeneza kusitisha operesheni,” amedai Kamanda Jongo.
Kamanda Jongo amedai kuwa, imekuwa desturi operesheni hiyo ikifika katika kijiji hicho, kutokea matukio ya mauaji.
“Huyo mwenye mji wake unaosemekana umechomwa, imekuwa ikijirudia kila zoezi linapofanyika. Ikifika kwenye huo mji tukio kama hilo linajirudia, ilishawahi kutokea askari watatu waliuawawa kinyama. Ambao walikuwa kwenye operesheni. Kila operesheni inapofika kwenye huo mji, mauaji yanatokea,” amedai Jongo.
Kufuatia utata wa tukio hilo, Kamanda Jongo amesema Ofisi ya Waziri Mkuu imeunda tume kwa ajili ya kuchunguza undani wa tukio hilo.
“Uchunguzi haujakamilika, tume ya waziri mkuu ilikuja kwa ajili ya uchunguzi, kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, pia imeunda tume kwa ajili ya uchunguzi. Uchunguzi uikikamilika tutatoa taarifa,” amesema Kamanda Jongo.
Hata hivyo, Kamanda Jongo amesema baadhi ya wananchi wa kijiji hicho na Askari Polisi wa TAWA, wamehojiwa kuhusiana na tukio hilo.
“Watu wanahojiwa, ikiwemo wananchi na maafisa wa TAWA, lakini ushahidi uliopo mpaka sasa, asilimia kubwa lile tukio limetenegezwa ili kusitisha operesheni,” amesema Kamanda Jongo.
Aidha, Kamanda Jongo amesema, operesheni ya kuondoa watu katika maeneo hayo inaendelea kufanyika.
Taarifa kutoka baadhi ya wananchi wa kijiji hicho zinadai kuwa, Mwandu alifariki dunia kwa kuteketea kwa moto akiwa ndani ya nyumba. Moto huo unadaiwa kuanzishwa na Askari Polisi wa TAWA wakishirikiana na Kituo cha Polisi cha Igalagala.
Leave a comment