May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mauaji Polisi Dar yamuibua Askofu Gwajima

Askofu Josephat Gwajima

Spread the love

 

MBUNGE wa Kawe, mkoani Dar es Salaam (CCM), Askofu Josephat Gwajima, amefanya maombi maalum ya kuwaombea Askari Polisi, katika Kanisa lake la Ufufuo na Uzima, lililopo Ubungo mkoani humo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar ea Salaam…(endelea).

Askofu Gwajima akiwaongoza waumini wa kanisa hilo, wamefanya maombi hayo leo Jumapili, tarehe 29 Agosti 2021, siku chache tangu tukio la mauaji ya Askari Polisi watatu na mlinzi mmoja wa Kampuni ya Ulinzi ya SGA,  kutokea maeneo ya Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Kinondoni mkoani humo.

Mauaji hayo yalifanywa na Hamza Mohammed, Jumatano ya tarehe 25 Agosti 2021, ambaye baada ya kutekeleza mauaji hayo aliuawa katika majibizano ya risasi baina yake na Polisi.

Kufuatia tukio hilo, Askofu Gwajima amesema maombi hayo yanalenga kumuomba Mungu awatie nguvu Askari Polisi,  katika majukumu yao ya kuilinda nchi.

” Leo tutafanya maombi maalum kuwaombea Polisi wasife moyo,” amesema Askofu Gwajima.

Askofu Gwajima amesema, kipindi hiki Watanzania wanatakiwa kuungana katika kuliombea Taifa, ili matukio ya mauaji yasitokee tena.

“Nakumbuka wakati ule kuna shida Kibiti tuliomba hapa Mungu akatusaidia,  hiyo ndiyo kusaida nchi. Panapofika jambo kama hili tunaungana kuiombea nchi,” amesema Askofu Gwajima.

Mbunge huyo wa Kawe amesema, huu si wakati wa kufurahia madhila yaliyowafika Polisi waliouawa na kujeruhiwa katika tukio hilo.

“Kuna watu wanachekelea wakomeshwe unajua mshahara wa Polisi wewe? Maaskofu wako wabaya na wazuri, maimamu wako wabaya na wazuri, maaskari wako wazuri na wabaya, huwezi kuhukumu wote hili jambo sio zuri. Hili jambo sio zuri halitakiwi kuzungumziwa, hebu imagine kuna Polisi ameuawa ameacha mtoto, dada, mama, kuna mjane, kuna mtoto hakupenda azaliwe na Polisi lakini analia,” amesema Askofu Gwajima.

Askari Polisi waliouawa katika tukio hilo ni, Miraji Khatib Tsingay, Emmanuel Keralya na Kangae Jackson. Mlinzi aliyeuawa ni Joseph Mpondo.

Askofu Gwajima ametoa pole kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Inspekta Jenerali wa Polisi nchini, IGP Simon Sirro, kufuatia tukio hilo.

“Leo lazima niseme haya sababu naipenda Tanzania,  tukio limetokea nchini mwetu  Askari Polisi walishambuliwa na wanne waliuawa hili tukio lilinisikitisha na natoa pole kwa jeshi  na rais,  tukio la huzuni sana sababu kazi ya Polisi kulinda raia na mali zake,  Polisi akiuswa maana yake hatuna walinzi si jambo zuri,” amesema Askofu Gwajima.

error: Content is protected !!