May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mauaji mwanafunzi Chuo Kikuu Iringa yaibuka bungeni

Spread the love

 

MBUNGE wa Nkasi Kaskazini mkoani Rukwa (Chadema), Aida Khenani, amelifikisha bungeni tukio la mauaji ya aliyekuwa Mwanafunzi wa Uandishi wa Habari, katika Chuo Kikuu cha Iringa, Marehemu Petronila Mwanisawa (22). Anaripoti Regina Mkonde Dar es Salaam … (endelea).

Tukio hilo la kusikitisha , lilitokea Alfajiri ya tarehe 2 Juni 2021, maeneo ya Semtema, Kata ya Kihesa katika Manispaa ya Iringa, ambapo inadaiwa chanzo chake ni wivu wa mapenzi.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma, leo Ijumaa tarehe 4 Mei 2021, Khenani ameiomba Serikali ichukue hatua kukomesha mauaji hayo, yanayosababishwa na wivu wa mapenzi.

“Ni vizuri Serikali ikaliangalia jambo hili, leo tunapoona adui wa kwanza wa kumaliza maisha ya wanawake ni mahusiano ya kimapenzi, iwe kwenye ndoa au mahusiano ya kawaida. Ni vizuri jambo hili likaangaliwa vizuri,” amesema Khenani.

Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoani Iringa, linamshikilia Prudence Patrick (21), anayedaiwa alikuwa mpenzi wa Mwanisawa, kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo.

Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi hilo, Mwanisawa alinyongwa kwenye chumba cha mtuhumiwa huyo, alikokwenda usiku wa kuamkia siku ya tukio, kwa ajili ya kuchukua Sh. 500, fedha aliyokuwa anamdai Patrick.

Inadaiwa kuwa, baada ya Patrick kutekeleza mauaji hayo, alichukua simu ya Mwanisawa kisha kuwajulisha wazazi wake, kwamba binti yao amefariki dunia. Ndipo wazazi wa mwanafunzi huyo walipolijulisha Jeshi la Polisi, juu ya tukio hilo.

Baada ya kutoa taarifa hiyo, mtuhumiwa huyo alijaribu kutoroka kuelekea mkoani Dodoma, lakini Jeshi la Polisi liliwahi kumkamata, kilomita chache kutoka nyumbani kwake, alikofanyia tukio hilo.

Patrick anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Iringa, hadi upelelezi wa tukio hilo utakapokalimilika na kufikishwa mahakamani.

error: Content is protected !!