August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mauaji msikitini

ACP Ahmed Msangi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza

Spread the love

NDANI ya Msikiti wa Rahma ‘Masjid Rahma’ mkoani Mwanza mauaji yametokea, watu watatu waumini wa msikiti huo wamepoteza maisha, anaandika Moses Mseti.

Watatu wakiwa wamepoteza maisha huku mmoja akiwa amejeruhiwa vibaya. Tukio hilo limetokea jana kwenye msikiti huo uliopo Ibanda Relini, Mtaa wa Utemini katika Kata ya Mkolani wilayani Nyamagana. Watu hao waliouawa kwa kukatwa katwa mapanga na kundi la watu zaidi ya 15.

Watu waliouawa katika tukio hilo ni Ferouz Elias, Imamu wa msikiti huo, Mbwana Rajab na Khamis Mponda ambaye ni dereva bodaboda. Aliejeruhiwa ni Ismail Abeid, mwanafunzi wa Shule ya Kiislam ya Jabar iliopo Nyasaka jijini humo.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo saa 2:30 usiku wakati waumini wa msikiti huo wakiendelea na Swala ya Isha.

Wakati swala hiyo ikiendelea, ghafla kundi hilo la watu waliingia msikitini hapo na kuanza kuhoji “kwanini mnaswali wakati wenzetu wamekamatwa na wanashikiriwa na polisi” kauli ambayo ilifuatana na mashambulizi hao.

Mashuhuda wa tukio hilo ambao hawakutaka kutajwa majina yao (yamehifadhiwa) wamesema kuwa, yawezekana chanzo cha mauaji hayo kinatokana na kuwepo kwa misikiti miwili ambayo ina uhasama wa muda mrefu.

Shuhuda moja amesema, “unajua katika eneo hili kuna msikiti miwili (anaionesha). Hawa kwa muda mrefu wapo katika uhasama sasa hili ndilo linaweza kuwa tatizo.

“Misikiti hii kama unavyoona ipo katika pori na ipo nje ya jiji na wakati wanatekeleza mauaji hayo, suala hili linatupatia wasiwasi mkubwa sana,” amesema.

Shuhuda huyo amesema, wauaji hao walikuwa na silaha za moto aina ya SMG pamoja na mabomu ya moto ya kutengeneza na kwamba, walirusha mabomu hayo lakini hayakuleta madhara yoyote.

Shekh Hussein Ibrahim, Mwenyekiti wa Baraza la Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Wilaya ya Nyamagana amelaani kitendo hicho.

Amesema, vitendo vya namna hiyo havikubaliki katika Dini ya Kiislam na kwamba, Waislam wote wanapaswa kulaani matukio ya namna hiyo.

“Nilipata taarifa saa tatu usiku na niliondoka na nilipofika eneo la tukio nilikutana na watu watatu waliokuwa wamejeruhiwa na watu waliokuwa wamekufa tuliwachukua na kuwapereka Bugando (Hospitali ya Rufaa ya Bugando) kwa ajili ya kuifanyia uchunguzi zaidi,” amesema Shekh Hussein.

Amesema kuwa, kufuatia tukio hilo Bakwata wameanza kuandaa mpango wa kuzuia na kudhibiti matatizo hayo katika maeneo yao (misikitini).

Ahmed Msangi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi (Sacp) amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Amesema kwamba, katika tukio hilo watu watatu wanashikiliwa na polisi mkoani humo kwa ajili ya mahojiano.

“Polisi hivi sasa tunaendelea na upelelezi wa tukio hilo na ninawaomba wananchi wawe watulivu katika kipindi hiki, polisi tunaendelea kuchunguza na pindi tutakapomaliza tutatoa taarifa kamili,” amesema Msangi.

error: Content is protected !!