October 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Matundu’ uchaguzi serikali za mitaa yasirejeshwe 2020

Mshauri Mwelekezi wa TYC, Zatwa Nyingi 

Spread the love

JOTO la Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020, linapamba moto ndani ya vyama mbalimbali vya siasa nchini Tanzania. Anaandika Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Tayari Rais John Magufuli amelifunga Bunge la 11 kwenye hotuba yake aliyoitoa tarehe 16 Juni 2020. Utaratibu wa kuvunja Bunge kisheria, unatoa fursa ya kuanza kwa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge, wawakilishi na Urais wa Tanzania na ule wa Zanzibar.

Katika hotuba yake iliyozidi saa mbili, Rais Magufuli alielezea mafanikio ya serikali aliyounda baada ya kuingia madarakani tarehe 5 Novemba 2015. Pia aligusia uchaguzi huo.

“Serikali, tumejipanga kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu, kama ilivyokuwa chaguzi zilizopita, unakuwa Huru na Haki. Navisihi vyama vya siasa na wanasiasa, kujiandaa vizuri kushiriki katika uchaguzi huo.

“Aidha, nawasihi wagombea kuepuka matusi na vurugu. Kama nilivyosema, sisi sote ni wamoja. Hivyo, tubishane kwa hoja kwa kushindanisha Ilani zetu…Nahimiza vyama kutoa fursa za kutosha kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu,” alisema Rais Magufuli.

Wakati Rais Magufuli akisisitiza fursa sawa, Uhuru na Haki katika uchaguzi huo, shirika lisilo la Kiserikali la Tanzania Youth Coalition (TYC), limekuwa likiomba kufanyika kwa majadiliano na wadau wote wa uchaguzi huo ili kujenga umoja na ushirikiano.

TYC linalofanyakazi chini ya mwamvuli wa Ushiriki Tanzania, lilitoa wito huo hivi karibuni wakati wakitoa tathimini ya utafiti walioufanya kwa Wilaya za Ubungo na Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Utafiti huo, ulilenga kuangazia jinsi wanawake, vijana na wenye ulemavu walivyoshiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika tarehe 24 Novemba 2019.

Akiwasilisha utafiti huo mbele ya waandishi wa habari hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Mshauri Mwelekezi wa TYC, Zatwa Nyingi amesema, katika uchaguzi huo wa serikali za mitaa, baadhi ya vyama havikushiriki jambo lililosababisha wagombea wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupita bila kupingwa.

Walemavu wakicheza mpira

Amesema, ili yasije kujirudia ya uchaguzi wa serikali za mitaa katika uchaguzi mkuu ujao, ni wakati kwa wadau wa uchaguzi kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), vyama vya siasa na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kushirikiana kwa pamoja.

“Tungependa sana, tunapoingia katika uchaguzi ujao, tumejeruhiana kwa namna moja au nyingine, makundi ya watu wenye ulemavu, vijana, wanawake, NEC, Tamisemi na vyama vya siasa wakae pamoja wajadiliane ili kuwa na uchaguzi shirikishi,” amesema.

Amesema, katika utafiti huo mdogo, wamebaini makundi ya wanawake, vijana na wenye ulemavu yamekuwa hayapewi kipaumbele, “na kama wanashirikishwa, wanapewa ushirikiano dakika za mwisho hali inayowafanya wasifanikiwe kuwa washiriki makini.”

Nyingi amesema, waliamua kufanya utafiti huo Kigamboni na Ubungo kwa sababi ni wilaya mpya ambazo zinawakirisha maeneo mengine nchini.

Walemavu

Amesema, makada mbalimbali wa vyama vya siasa pamoja na asasi za kiraia, wanapaswa kuhakikisha wanatoa elimu kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu ili kuwahamasisha umuhimu wa kushiriki kwenye uchaguzi ikiwemo kugombea  kwenye nafasi kama za udiwani, ubunge na Urais.

Mshauri huyo anasema, baadhi ya maswali waliyouliza katika utafiti huo ni jinsi makundi hayo ya wanawake, vijana na wenye ulemavu walivyoshirikishwa kwenye uchaguzi huo kuanzia awali, kupata taarifa za ushiri pamoja na kupewa msukumo na vyama vya siasa.

Nyingi amesema, waliohojiwa ni 20, wenye ulemavu 20 vijana na wanawake 20.

“Lengo lilikuwa kujua ushiriki wao katika uchaguzi wa serikali za mitaa na jinsi ya kuhakikisha changamoto zilizojitokeza hazijirudii katika uchaguzi mkuu ujao,” amesema Nyingi.

Amesema, jambo lingine ambalo walilibaini katika utafiti huo, ni njia ya mawasiliano inayotumika hususan kwa watu wenye ulemavu.

“Watu wenye ulemavu, wanapendekeza kuwepo na wakalimani watakaowasaidia kuwasiliana na jamii au katika mikutano ya kampeni kuwepo na wakalimani ambao watawasaidia kujua nini kinazungumzwa,” anasema Nyingi

Amesema, kutoshirikishwa kuanzia mwanzo wa michakato ya uchaguzi na wakati mwingine, ukifika mwisho ndiyo wanaanza kushirikishwa jambo ambalo wanaona siyo sahihi.

“Watu wenye ulemavu walisema, walishindwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za kutaa kutokana na changamoto ya rasilimali fedha za kutumia katika kampeni,” anasema.

Mshauri huyo amesema, changamoto ya fedha iliyoelezwa na wenye ulemavu ndiyo inawakumba wanawake na vijana kwenye chaguzi.

“Wanawake walilalamika jinsi ambavyo nguvu ndogo ya kuwasaidia katika uchaguzi wa serikali za mitaa ilivyokuwa, ikiwemo elimu ya uraia ya kuwajengea uwezo wa kushiriki kwenye uchaguzi huo,” amesema.

Walemavu

Amesema, makundi yote ya vijana, wanawake na wenye ulemavu hawakuridhika na jinsi walivyoshirikishwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.

“Vyama vya siasa, vinahitaji kutoa elimu ya uraia kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu na kuweka kipaumbele katika mipango na mikakati yake kuanzia ngazi za awali kabisa,” amesema Nyingi na kuongeza:

“Inahitajika kufanyika kwa mabadiliko ya sheria za vyama vya siasa, ili kuweka demokrasia na ushirikishaji wa makundi hayo.”

Amesema, TYC inashauri vyama vya siasa, asasi zinazojishughulisha na utetezi wa haki za binadamu na wadau wengine wa uchaguzi kushirikiana kwa pamoja ili kuweka usawa katika chaguzi.

Lenin Kazoba, Mkurugenzi wa TYC, amesema, lengo ni kuona namna gani ushiriki wa wanawake, vijana na wenye ulemavu unakuwa mkubwa katika chaguzi mbalimbali.

“Kipi cha kujifunza ili tusirudie makosa ambayo yaliyojitokeza kwani ushiriki wa vijana katika vyama vya siasa, umekuwa mfinyu. Vivyo hivyo, kwa wanawake na wenye ulemavu,” amesema.

Kazoba amesem, bado kuna nafasi kubwa kwa makundi haya kushirikishwa kuanzia hatua za mwanzo kabisa za uchukuaji fomu na urejeshaji ili kuwa na uwiano sawa katika uchaguzi pasina ubaguzi wa aina yoyote.

Rose Reuben, Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa Ushiriki Tanzania inayounda mashika 23 amesema, makundi hayo ya wanawake, vijana na wenye ulemavu yanapaswa kupewa kipaumbele kama wengine bila ubaguzi wowote.

“Vyama vya siasa ndiyo chanzo cha kupatikana kwa washiriki wa uchaguzi, kwa hiyo ni wakati sasa wa kutoa fursa kwa makundi yote, kwa usawa bila kubagua ili tuwe na viongozi wanawake, vijana na wenye ulemavu,” amesema Rose.

error: Content is protected !!