January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Matumaini yaanza kuchomoza Mto Nile

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda

Spread the love

SERIKALI imetoa wito kwa nchi wanachama wa Bonde la Mto Nile kuridhia mkataba wa matumizi ya maji yatokayo Mto Nile kwa kuwa, kufanya hivyo wataweza kuondoa umaskini uliopo kwenye nchi hizo. Anaandika Dany Tibason kutoka Dodoma … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda juzi mjini hapa  wakati akifungua Mkutano wa 23 wa Mwaka wa Mawaziri wa Maji kutoka Nchi zinazopitiwa na Bonde la Mto Nile.

Nchi hizo ni Uganda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Misri, Ethiopia, Sudan Kusini pamoja na Tanzania.

Pinda amesema, kama nchi zote 11 zitakubali kusaini mkataba wa matumizi ya maji yatokayo Mto Nile, zitaweza kuondokana na umaskini uliopo kwa kuwa, maji ni kiunganishi muhimu katika jamii.

“Huu ni mkutano wa kawaida, hapa zinakutana jumla ya nchi 11 lengo likiwa ni kujadiliana kuhusiana na matumizi ya Mto Nile. Jambo la kufurahisha nchi tatu zimeisha saini mkataba huo ambazo ni sisi Tanzania, Ethiopia na Rwanda na nadhani zote zitakubali kusaini mkataba huo.

Amesema, mwanzo watu wa Misri walikataa kusaini mkataba huo wa matumizi ya maji yatokanayo Mto Nile wakitaka uendelee kutumika mkataba wa mwaka 1927 waliosaini na Waingereza unawabana wengine ikiwemo Tanzania na kuwa, kwa sasa wanaelekea kwenye kukubaliana.

“Ila lazima tukiri maji yanaweza kutuondolea umasikini tulionao kwani tunaweza kuiendesha mitambo kwa kupitia maji, umeme, pia na utunzaji wa mazingira,” anasema Pinda.

Pinda amesema, kwa sasa wanakabiliwa na changamoto ya jinsi ya kuuendesha umoja huo pamoja na kuusimamia ili kuhakikisha haki ya kila nchi inapatikana katika matumizi ya maji.

Waziri wa Maji wa Tanzania, Jumanne Maghembe amesema, mkataba huo unajumla ya vifungu 44 vilivyokubaliwa huku kifungu cha 14, B kikikataliwa na Misri.

Amesema, kifungu hicho kinasema ‘tumia maji ilimradi usiathiri nchi nyingine’ huku Misri wakitaka kuendelea kuwepo kifungu cha mwaka 1927 kinachoeleza kutumia maji ilimradi yanazingatia haki za zamani.

Maghembe amesema, kifungo hicho kilisainiwa na Nchi za Misri na Uingereza huku Misri ikitakiwa kutumia maji yatokayo Mto Nile kwa asilimia 87.

“Misri walikuwa wanataka utumike mkataba wa mwaka 1927, sisi tukakataa lakini kwa sasa tunaelekea katika makubaliano mazuri na sisi ni wadau wakubwa wa Mto Nile,” amesema Maghembe.

error: Content is protected !!