September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Matokeo ya rais 2020 kutangazwa Dodoma

Mwenyekiti wa NEC, Semistocles Kaijage

Spread the love

MATOKEO ya urais Tanzania Bara katika Uchaguzi Mkuu 2020, kwa mara ya kwanza yatatangazwa jijini Dodoma. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Kauli hiyo imetolea leo tarehe 22 Julai 2020 na Jaji Semistocles Kaijage, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC) wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la NEC katika eneo la Njedengwa, jijini humo.

Kwenye uzinduzi wa jengo hilo uliohudhuriwa na Rais John Magufuli na viongozi mbalimbali, Jaji Kaijage amesema, jengo hilo limekamilika kwa asilimia 89.

         Soma zaidi:-

Miongoni mwa waliohudhuria uzinduzi huo ni pamoja na Mama Samia Suluhu Hassan; Dk. Bashiri Ally, Katibu Mkuu wa CCM; James Mbatia, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi na Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF).

Vyama vya upinzani vyenye nguvu – Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha ACT-Wazalendo – havikuwa na mwakilishi yeyote.

Jaji Kaijage kwenye uzinduzi huo amemshukuru Rais Magufuli kwa uamuzi wake wa kukubali ombo la NEC la kuwa na ofisi zake.

“Kule Dar es Salaam tulikuwa tumepanga. Ningependa kwa niaba ya Tume ya Uchaguzi kushukuru kwa kukubali kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi huu,” amesema Jaji Kaijage.

Amesema, jengo hilo lilianza kujengwa na Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA), baada ya kuingia mkataba na taasisi hiyo tarehe 29 Juni 2017 na kwamba, mradi huu ulipangwa kuwa na awamu mbili ukigharimu jumla ya Shilingi bilioni 2.332.

“Kutokana na changamoto za utekelezaji na kuchelewa kukamilika, tarehe 24 Novemba mwaka jana tulivunja mkataba na wakala wa majengo.

“Tuliingia mkataba mpya na SUMA JKT, mkataba huu ulitarajiwa kukamilika tarehe 24 Aprili mwaka huu. Makandarasi aliongezewa muda na mpaka sasa limekamilika kwa asilimia 89,” amesema Jaji Kaijage.

Amesema, uzinduzi huu unaashiria kuanza rasmi kwa huduma za ofisi hiyo Dodoma kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

error: Content is protected !!